020-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupaka kichwa

3- Kupaka kichwa

Allaah Mtukufu Anasema:
 « وامسحوا برءوسكم »
« Na pakeni vichwa vyenu »([1])

Maulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kuwa kupaka maji kichwani ni lazima. Lakini hata hivyo wamehitalifiana juu ya kiasi kinachotosheleza upakaji huo katika kauli tatu:

Kauli ya kwanza:
Ni lazima kupaka kichwa chote maji sawasawa kwa mwanamke au kwa mwanamume.
Haya ni madhehebu ya Maalik na Dhaahir. Pia ni madhehebu ya Ahmad na kundi la wenzake, Abu ‘Ubayd na Ibn Al-Mundhir. Na Ibn Taymiyah([2]) ameuridhia msimamo huu. Ushahidi wao ni haya yafuatayo:

1- Ni Neno Lake Allaah Mtukufu:
   « وامسحوا برءوسكم»
« Na pakeni vichwa vyenu »
Hapa “ب baa” ni ya kuambatisha (si ya usehemu). Kwa hiyo makadirio ya aya yanakuwa ni:
 « وامسحوا رءوسكم»
Hii ni kama kuosha uso katika tayammamu, kwani vyote katika Qur-aan Tukufu vimekuja kwa tamko moja. Allaah Anasema:
« فامسحوا بوجوهكم»
« Na mwoshe nyuso zenu »([3]) yaani uso wote.

2- Ni kwamba jambo hili limefasiriwa na Sunnah iliyonukuliwa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kuwa, yeye alipotawadha, alikuwa akipaka kichwa chake chote. Na kati ya yanayothibitisha hili, ni Hadiyth ya Abdullaah bin Zayd aliyesema: “Alitujia sisi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tukamtolea maji katika ndoo yashaba. Akatawadha; akaosha uso wake mara tatu, akaosha mikono yake mara mbili hadi katika vifundo, akapaka maji kichwani kwa kupeleka mkono mbele na nyuma na akaosha miguu yake miwili”.([4]) Na katika tamko jingine “akapaka kichwa chake chote”.

3- Ni Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu’ubah aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya khufu zake, mbele ya utosi wake na juu ya kilemba chake”.([5])
Na lau kama ingetosheleza kupakasa mbele ya utosi, basi asingelipukusa juu ya kilemba. Kwa hivyo, hilo limeonyesha kuwa ni lazima kueneza (kichwa kizima).

Kauli ya pili
Inatosheleza kupaka sehemu ya kichwa.
Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy.([6]) Lakini pamoja na hivyo, wao wamehitalifiana juu ya kiasi kinachotosheleza. Wamesema ni nywele tatu, au robo ya kichwa au nusu!! Na hoja yaoni:

1 Ni kwamba “ب baa” katika Neno Lake Allaah Mtukufu:
  « وامسحوا برءوسكم»
« Na pakeni vichwa vyenu » ni ya usehemu na wala si ya kuambatisha.

2- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuwa alipaka katika utosi wake.

Kauli ya tatu:


Ni lazima kupaka kichwa chote kwa mwanamume basi, si kwa mwanamke.
Ni riwaya iliyonukuliwa toka kwa Ahmad. Amesema: “Ninataraji kupaka maji kichwani kwa mwanamke kuwe ni sahali zaidi. ‘Aaishah (Allaah Amridhie) alikuwa akipaka mbele ya utosi wake.

Ibn Qudaamah anasema: “Na Ahmad ni katika mabingwa wa Hadiyth. Na hatolei dalili kwa tukio la kitu ila kama limethibiti kwake kwa Uwezo wa Allaah”.([7])

Ninasema (Abuu Maalik): “Ninaloliona lenye nguvu katika hayo yaliyotangulia ni kuwa ni lazima kupaka maji kichwa chote wakati wa kutawadha kutokana na nguvu ya hoja zake. Ama wale waliosema kuwa “ب baa” katika aya ni ya usehemu, basi hilo Siybawayhi amelikanusha katika sehemu kumi na tano katika kitabu chake. Na Ibn Burhan amesema: “Mwenye kudai kwamba “ب baa” inaonyesha usehemu, basi atakuwa amewaletea mabingwa wa Lugha jambo wasilolijua”.([8])

Mbali ya hivyo, hakuna Hadiyth yoyote sahihi toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayoeleza kuwa yeye alifupishia kupaka baadhi ya kichwa chake tu. Lililothibiti ni kuwa yeye alipokuwa akipaka utosi wake, alikamilishia juu ya kilemba.([9])
Ama mwanamke, mimi siijui dalili yoyote ya kumbagua yeye na mwanamume katika hilo. Lakini inajuzu kwake kupaka maji juu ya mtandio wake. Na lau kama amepaka utosi wake pamoja na mtandio wake, basi hilo litakuwa ni bora ili kuepukana na mvutano. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.


FAIDA
Ikiwa kichwa kimepakwa hina ghafi au mfano wake, itajuzu kupaka maji juu yake. Kwani imethibiti toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba yeye alikuwa akikipaka kichwa chake hina akiwa katika ihramu yake na hakuwa akijisumbua kuitoa kwa ajili ya wudhuu (kama itakavyokuja katika mlango wa hija). Na ikiwa ataweka kichwani mwake kitu kama hicho, basi atakifuatilizia. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.   
([1]) Surat Al-Maaidah : 6
([2]) “Al-Mudawwanah” (1/16), “Al-Mughniy” (1/92), “Atw-Twahuur” (uk. 358), “Al-Awsat” (1/399) na “Majmuu’i Al-Fataawa” (21/123).
([3])  Surat Al-Maaidah : 6.
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (185) na Muslim (235).
([5]) Imetolewa na Muslim (275), Abuu Daawuud (150) na At-Tirmidhiy (100). Hadiyth hii imezungumziwa mengi. Na Al-Albaaniy Allaah Amrehemu amesema kuwa ni sahihi.
([6])“Al-Mabsuut” (1/8), “Al-Majmuu’i” (1/399) na “Al-Mughniy” (1/92).
([7])“Al-Mughniy” (1/93).
([8])“Nayl Al-Awtaar” (1/155) na “Al-Mughniy” (1/87).
([9])“Majmuu’i Al-Fataawa” (21/122), “Ahkaam Al-Qur-aan” cha Ibn Al-‘Arabiy (2/571) na “Subul As-Salaam” (1/107).

0 Comments