021-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupaka Masikio Mawili

4- Kupaka masikio mawili

Ni lazima kupaka masikio mawili pamoja na kichwa, kwani masikio ni sehemu ya kichwa. Imepokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

(( الأذنان من الرأس ))
((Masikio mawili ni sehemu ya kichwa ))([1])

Hadiyth hii ni dhaifu marfuu kwa kauli yenye nguvu. Lakini hata hivyo imethibiti kwa watangu wema wengi akiwemo Ibn ‘Umar.([2])

Na kuna Hadiyth zinazolitolea hilo ushahidi. Ni kama ile inayoashiria kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipaka kichwa chake na masikio yake mara moja.([3]) Hadiyth hizi ni nyingi zilizonukuliwa toka kwa Aliy, Ibn ‘Abbas, Ar-Rubayyi’i na ‘Uthmaan. As-Swan’aaniy anasema: “Wote wamekubaliana kuwa kuyapaka masikio na kichwa ni mara moja tu” yaani kwa maji hayo hayo kama inavyoonekana kutokana na tamko la “mara moja”. Kwa vile, lau kamamasikio yangekuwa yanatekewa maji mapya, basi kusingelithibitishwa ya kuwa “yeye alipaka kichwa na masikio mara moja”. Na kama itachukulika kwamba mapendeleo ni kuwa yeye hakukariri kuyapaka bali aliyatekea maji mapya, basi huo ni uwezekano wa mbali”.([4])
Ninasema: Na kama atateka maji mengine ya kupaka masikio, basi hapana ubaya. Kwani hilolimethibiti toka kwa Ibn ‘Umar.([5])  


UZINDUSHI
Hakuna usheria wowote wa kuosha shingo wakati wa kutawadha, kwa vile hakuna Hadiyth yoyote sahihi iliyopokelewa toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikiligusia hilo.([6])

 
([1]) Hadiyth Dhaifu: Ina njia nyingi na zote zina kasoro. Pia pamehitalifiwa katika kuifanya ni Hadiyth Hasan kwa vikundi vyake. Na Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy Allaah Amrehemu katika Kitabu chake cha “Asw-Swahiyhah” amesema kuwa huenda Hadiyth hii ikapanda kufikia ngazi ya Hadiyth Mutawaatir kwa baadhi ya Maulamaa!! Shaykh wetu Allaah Amhifadhi ameitolea maelezo ya kichambuzi katika “Al-Nadharaat” na akatilia nguvu udhaifu wake, nalo ni jambo sawa kabisa. Na Shaykh Mash-huur Hasan Allaah Amhifadhi amesema kuwa ni dhaifu baada ya utafiti mzuri alioufanya pambizoni mwa Kitabu cha “Al-Khilaafiyyaat” kilichotungwa na Al-Bayhaqiy (1/448).
([2]) Isnad yake ni nzuri: Imetolewa na Ad-Daar Qutniy (1/98), Ibn Abuu Shaybah (1/28) na wengineo.
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (133), At-Tirmidhiy (36), An-Nasaaiy (1/74), Ibn Maajah (439) na wengineo. Ina njia mbalimbali za kuifanya kuwa sahihi zilizonukuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas. Na asili yake iko kwa Al-Bukhaariy (157) kwa ufupi. Pia ina ushahidi toka kwa Hadiyth ya Ar-Rubayyi’i binti Mu’awwidh. Imetolewa na Abuu Daawuud (126), At-Tirmidhiy (33) na Ibn Maajah (418). Vilevile imenukuliwa toka kwenye Hadiyth ya Al-Miqdaam.     
([4])“Subul As-Salaam” (1/49).
([5]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Abdurraaziq (29) na Al-Bayhaqiy (1/65).
([6])“Majmuu’I Al-Fataawa” (1/56) na “Zaad Al-Ma’ad” (1/49). Tizama “As-Silsilat Adh-Dha’iyfah”(69-744).

0 Comments