022-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuosha Miguu Miwili Pamoja Na Vifundo

6- Kuosha miguu miwili pamoja na vifundo([1])

 Kuosha miguu miwili ni lazima kwa jamhuri ya Maulamaa wa Ahlus-Sunnah kutokana na Neno Lake Allaah Mtukufu:

« وأرجلكم إلى الكعبين »
« Na miguu yenu hadi kwenye vifundo viwili »([2]).

Ni kwa kutia “fat-hah” juu ya “arjulakum” kuunganishia kwenye viungo vinavyooshwa.
Na kila aliyehadithia sifa ya wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amethibitisha kwamba aliosha miguu miwili hadi kwenye vifundo viwili. Na kati ya yaliyoelezewa ni yale yanayomhusu ‘Uthmaan yanayosema: “..Kisha akaosha miguu yake miwili hadi katika vifundo mara tatu….”.([3]) Na vifundo viwili hujumuishwa katika kuoshwa, kwani ikiwa mpaka unatokana na jinsi ya chenye kuwekewa mpaka, basi nao huingia kama ilivyotangulia. Na  Hadiyth ya Ibn ‘Amri (Allaah Amridhie) inaonyesha juu ya haya. Anasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikawia nyuma katika safari. Kisha alituwahi nailhali alasiri imekurubia kumalizika wakati wake. Tukaanza kutawadha huku tukipaka miguu yetu. Hapo akanadi kwa sauti kubwa:  
((ويل للأعقاب من النار))
((Ole wao na moto kwa (kutoosha) visigino)).
Alisema mara mbili au tatu.([4])

Ama yale yaliyopokelewa ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipaka (miguu) katika wudhuu wake, linalochukuliwa ni kupaka juu ya khufu mbili, nalo ni jambo ambalo yeye aliliruhusu. Suala hili Maraafidha na Mashia wengi wamekwenda kinyume nalo wakisema kuwa ni lazima kupaka miguu miwili badala ya kuosha. Na lililo sahihi kutumiwa ni la kwanza. Abdur-Rahmaan bin Abi Layla anasema: “Maswahaba wote wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wamekubaliana juu ya kuosha miguu miwili”.([5])


KUPACHANYISHA VIDOLE VYA MIGUU NA MIKONO

Vidole na sehemu zilizo kati yake, ni sehemu ya mahala pa faradhi. Kwa hiyo ni lazima zioshwe. Nakama haitowezekana kuoshwa ila kwa kupachanyishwa, basi ni lazima kufanya hivyo. Na kamaitawezekana, basi itapendeza kama itakavyokuja.
([1]) Vifundo viwili : Ni mifupa miwili iliyochomoza katika pambizo mbili za mguu. 
([2]) Surat Al-Maaidah : 6
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (158) na Muslim (226).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (161) na Muslim (241).
([5])“Fat-h Al-Baariy” (1/266) na “Al-Mughniy” (1/120).

0 Comments