023-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupangilia

7- Kupangilia


Nako ni kuvitwaharisha viungo vya wudhuu kimoja baada ya kingine kwa mpangilio ambao Allaah Ameamrisha katika aya tukufu. Ataosha uso, kisha mikono miwili, kisha atapaka kichwa, halafu ataosha miguu miwili. Mpangilio huu ni wajibu katika kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili. Na hayo ndiyo madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Hanbali, Abu Thawr, Abu ‘Ubayd na Adh-Dhahiriya.([1]) Wajibu huu wameutolea hoja kwa haya yafuatayo:

1- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ametaja katika aya faradhi za wudhuu kimpangilio pamoja na kutenganisha miguu miwili na mikono (ambavyo ni lazima vioshwe) kwa kichwa ambacho ni lazima kipakwe. Na Waarabu hawakitenganishi kitu na chenziye ila kwa faida fulani. Na hapa aya inaashiria ulazima wa kupangilia. ([2])

2- Ni kwamba kila aliyehadithia kuhusu wudhuu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ameuelezea ukiwa umepangika.([3]) Na kitendo chake hicho kinafasiri Kitabu cha Allaah Mtukufu.

3- Ni kwa yale yaliyohadithiwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha kimpangilio kisha akasema:

(( هذا وضوء لا يقبل الله الصلاة إلا به))


((Huu ni wudhuu, Allaah Haikubali Swalah ila kwao)).


Lakini hii ni Hadiyth dhaifu.([4])

Ama Maalik, Ath-Thawriy na wenye rai,([5]) wao wanasema kuwa kupangilia ni jambo lililosuniwa na wala si wajibu. Hoja yao ni:

1- Kwamba kiunganishi kihusishi “و waw” katika aya, hakihukumii mpangilio. Jibu la haya, liko katika yaliyotangulia.

2- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa Aliy na Ibn Mas’ud kwamba wamesema: “Sijali ni kwa kiungo gani nilichoanzia”.([6]) Hili linajibiwa kwa yale aliyoyasema Al- Imam Ahmad kama ilivyo katika “Masuala ya mwanawe Abdullaah” (27-28):
“Bila shaka ina maana ya kushoto kabla ya kulia. Na hakuna ubaya kuanza kwa kushoto kwake kabla ya kulia kwake, kwani matoleo yake toka katika Qur-aan ni mamoja. Allaah Mtukufu Anasema:

 « فاغسلوا وجوهكم وأيديكم إلى المرافق وامسحوا برءوسكم وأرجلكم »


« Basi osheni nyuso zenu na mikono yenu hadi kwenye vifundo, na mpake vichwa vyenu, na (mwoshe) miguu yenu ».([7])

Kwa hiyo, hapana ubaya kuanza kushoto kabla ya kulia”.
Ninasema: “Na ingawa ubora ni kuanzia kulia kwa ajili ya kufuata Sunnah. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.


 
([1])“Al-Majmuu’i” (1/433), “Al-Mughniy” (1/100) na “Al-Muhalla” (2/66).
([2] Ni sawasawa ilivyo katika “Al-Mughniy” (1/100).
([3]) Maswahaba 20 wamehadithia sifa ya wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam wakinukulu toka kwake. Wote wameuelezea kwa mpangilio isipokuwa katika Hadiyth mbili dhaifu ambazo Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi katika kitabu cha “Tamaam Al-Minnah” (uk.85).
([4]) Hadiyth Dhaifu : Tazama katika “Al-Irwaa” (85).
([5])“Al-Mudawwanah” (1/14), “Al-Mabsuut” (1/55) na “Sharhu Fat-h Al-Qadiyr” (1/30).
([6]) Kaulipokezi ya Aliy. Imetolewa na Ahmad katika kitabu cha “Al’Ilal” (1/205), Ibn Abu Shaybah (1/55) na Ad-Daarqutniy (1/88), sanadi yake ni dhaifu. Pia kaulipokezi ya Ibn Mas’ud iliyotolewa na Al-Bukhaariy katika kitabu cha “Al-Taariykh” (1650) na Abu ‘Ubayd katika “Attwahuur”(325) kwa sanadi nzuri kwa tamko la: “Akitaka ataanza kushoto kwake katika wudhuu” kama alivyosema Imaam Ahmad.
([7]) Surat Al-Maaidah : 6.

0 Comments