024-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuandamisha

8- Kuandamisha


Ni kufuatilizia uoshaji wa viungo vya wudhuu kwa namna ambayo kisikauke kiungo kabla hajaingia kiungo kingine katika muda wa kiwango cha kawaida.
Ash-Shaafi’iy katika kauli yake ya zamani na Ahmad katika “Al-Mash-hur” wanasema kuwa ni lazima kuandamisha. Pia Maalik anasema hivyo hivyo isipokuwa yeye ametofautisha kati ya aliyefanya kusudi ya kutofautisha na kati ya mwenye udhuru. Na haya ndiyo aliyoyachagua Shaykh wa Uislamu.([1])
Ulazima wa kuandamisha unafahamishwa na Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattaab kwamba mtu mmoja alitawadha akaacha sehemu ndogo ya kucha katika miguu yake. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwangalia kisha akamwambia:


(( إرجع فأحسن وضوءك ))
(( Rejea ukatawadhe vizuri)).


Akarejea kisha akaswali.([2])


Na katika riwaya iliyopokelewa na baadhi ya Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu mmoja akiswali nailhali juu ya mguu wake kuna sehemu nyeupe ya ukubwa wa (mviringo) dirham haikupata maji. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha atawadhe upya na aswali tena.([3])

Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya wanasema kuwa kuandamisha si lazima. Nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad, na pia ni madhehebu ya Ibn Hazm.([4])Wamesema:

1- Kwa vile Allaah Mtukufu Amewajibisha kuosha viungo. Kwa hiyo mwenye kuviosha, atakuwa amefanya wajibu wake, ni sawasawa awe ameviosha kiholela bila mpangilio au akaviosha kwa mpangilio uliopangika.

2- Ni kwa yale aliyoyahadithia Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar alitawadha sokoni, akaosha uso wake na mikono yake na akapaka kichwa chake. Kisha aliitwa kwenda kuswalia maiti, akaingia msikitini, kisha akapaka juu ya khufu zake na akaswali.([5])

3- Wameifanya kuwa ni dhaifu, Hadiyth yenye amri ya kutawadha na kuswali upya.

4- Wameliawilisha neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Rejea ukatawadhe vizuri)) kwamba makusudio yake ni kukamilisha kuosha sehemu ambayo haikupata maji mguuni.

Ninasema: “Hukumu ya mvutano wa yaliyotangulia ni Hadiyth ya Khaalid bin Mi’idaan yenye amri ya kutawadha tena na kuswali upya aliyoinukuu toka kwa baadhi ya Maswahaba wa Mtume. Aliyeifanya kuwa ni sahihi, amesema ni lazima. Na kama si hivyo, basi hoja zilizobakia zina uwezekano wa hili au lile. Ninaloliona mimi kuwa ni sawa, ni ulazima wa kuandamisha kutokana na Hadiyth hii. Pia, ni kwa vile wudhuu ni ibada moja, isitenganishwe. Ama kaulipokezi ya Ibn ‘Umar, inavyoonekana ni kuwa hiyo ni katika hali ya udhuru na kulazimika, na kwa hivyo, haipimiwi na hali ya kawaida. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

Lakini ikiwa patatokea mtengano kidogo katika kuosha viungo, basi hakuna ubaya. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 
([1])“Al-Ummu” (1/30), “Al-Majmuu’i” (1/451), “Kash-Shaaf Al-Qina’i” (1/93), “Al-Mudawwanah”(1/15), “Al-Istidhkaar” (1/267) na “Majmuu’i Al-Fatawa” (21/135).
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (232), Ibn Maajah (666) na Ahmad (1/21). Hadiyth hii imetiwa baadhi ya dosari, lakini ina vithibitisho vyake vinavyoifanya kuwa sahihi bila ya shaka yoyote. Angalia katika “At-Talkhiysw” (1/95) na “Al-Irwaa” (86).
([3]) Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi. Imetolewa na Abuu Daawuud (175) na Ahmad (3/424) kupitia kwa Buqayyah bin Al-Waliyd.
([4]) “Al-Mabsuut” (1/56), “Al-Ummu” (1/30), “Al-Majmuu’i” (1/451) na “Al-Muhalla” (2/70).
([5]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Maalik (48) na kutoka kwake akapokea Ash-Shaafi’iy (16) na Al-Bayhaqiy katika “Al-Ma’arifah” (99).

0 Comments