025-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Sunnah Za Wudhuu

 SUNNAH ZA WUDHUU  
1- Kupiga mswaki

Jambo hili limekwishadokezwa kuwa linapendeza katika mlango wa “Sunnah za hulka asili2- Kupiga bismillaah mwanzoni

Kiilivyo, kupiga bismillaahi ni jambo zuri la kisheria katika mambo yote. Kuna Hadiyth dhaifu zilizopokelewa kuhusu kupiga bismillaahi wakati wa kutawadha ingawa baadhi ya Maulamaa wamesema kuwa Hadiyth ni sahihi. Kati ya Hadiyth hizo ni ile isemayo:

 ((ولا وضوء لمن لم يذكر اسم الله عليه))
((Hakuna wudhuu kwa yule ambaye hakulitaja Jina la Allaah)).([1])

Na kuna Hadiyth nyingine dhaifu sana zisizofaa kabisa kutegemewa kwa hoja. Na kwa ajili hiyo, Imaam Ahmad amesema: “Siijui Hadiyth yoyote katika mlango huu yenye isnadi nzuri”.

Ninasema (Abuu Maalik): “Linalotilia nguvu kutokuwepo ulazima wa kupiga bismillaahi ni kuwa watu walioelezea sifa ya wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawakutaja kuhusu bismillaahi. Na haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Maalik na Ash-Shaafi’iy. Ni riwaya toka kwa Ahmad.([2])   3- Kuosha viganja viwili mwanzoni


Ni kwa yale yaliyomo katika Hadiyth ya ‘Uthmaan katika sifa ya wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). ‘Uthmaan anasema: “Akamiminia katika viganja vyake mara tatu, akaviosha…([3])


4- Kusukutua na kupaliza maji mara tatu kwa teko moja

Ni kwa yale yaliyomo katika Hadiyth ya Abdullaah bin Zayd alipokuwa akifundisha namna Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akitawadha: “Kwamba yeye (Mtume) alisukutua na akapaliza kwa teko moja. Akafanya hivyo mara tatu”.([4])


5- Kuyakomeza maji hadi mwisho wakati wa kusukutua na kupaliza kwa ambaye hakufunga

Ni kwa Hadiyth Marfuu ya Laqiyt bin Swabrah:

وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما)) ((
((Na komeza maji hadi mwisho isipokuwa kama umefunga)).([5])


6- Kutanguliza kulia kabla ya kushoto

Katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kuhusu sifa ya wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “…kisha alichukua teko la maji akaosha kwalo mkono wake wa kulia, kisha akachukua teko jingine akaosha kwalo mkono wake wa kushoto, kisha alipaka kichwa chake maji, kisha alichukua teko la maji, akanyunyizia kwalo mguu wake wa kulia mpaka akauosha, kisha alichukua teko jingine akaosha kwalo mguu wake, yaani wa kushoto….([6])
Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kuanza kwa upande wa kulia wakati wa kuvaa viatu, kutembea, kujitwaharisha na katika kila jambo lake alilolifanya.([7])


7- Kuviosha viungo mara tatu

Imepokelewa Hadiyth sahihi toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba alitawadha (akiviosha viungo) “mara moja moja”,([8]) na kwamba aliviosha “mara mbili mbili”.([9])
Na ukamilifu na utimilifu zaidi wa wudhuu ni kuviosha viungo mara tatu kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mujibu wa ilivyoelezewa katika Hadiyth za ‘Uthmaan na Abdullaah bin Zubayr. Hadiyth hizi zimekwisha zungumziwa.


8- Kuziasulia ndevu nyingi

Tumekwisha eleza kwamba kama ndevu ni nyingi zisizoonyesha ngozi, basi itatosha kuosha nje yake tu. Na hapa tunaongeza kusema kuwa imesuniwa kuziasulia kwa maji kutokana na Hadiyth ya Anas isemayo kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa kutawadha, alikuwa akichukua teko la maji, kisha huliingiza chini ya kaakaa na kuasulia kwalo pia. Kisha Mtume husema:

((هكذا أمرني ربي عز وجل))
((Hivi ndivyo Mola wangu Mtukufu Alivyoniamrisha)).([10])

Na jambo hili linageuziwa katika u-Sunnah kutokana na Hadiyth iliyotangulia hapo kabla ya Rifa’a bin Raafi’i inayozungumzia kisa cha mwenye kuswali vibaya.


9- Kusugua viungo

Ni kwa Hadiyth ya Abdullaah bin Zubayr aliyesema: “Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha, na kisha akaingilia kuisugua mikono yake miwili”.([11])


10- Kuasulia vidole vya mikono na miguu

Ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((أسبغ الوضوء، وخلل الأصابع، وبالغ في الاستنشاق إلا ان تكون صائما))
((Tawadha wudhuu kamili, asulia vidole, na ubalighishe katika kupaliza maji, isipokuwa kamaumefunga)).([12])

Na kama vidole na sehemu za kati yake haviosheki ila kwa kuasulia, basi wakati huo itakuwa ni lazima kufanya hivyo kama tulivyotangulia kusema.


11- Kuosha zaidi ya mahali pa faradhi

Imesuniwa kutawadha kikamilifu, kurefusha kuosha uso hadi katika ncha ya utosi, na kuosha zaidi ya vifundo viwili na visigino. Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((إن أمتي يأتون يوم القيامة غرا محجلين من آثار الوضوء))
((Hakika umati wangu utakuja siku ya Qiyaama hali ya kuwa nyuso zao, mikono yao na miguu yaoinang’ara kutokana na athari za wudhuu)).  
Abu Hurayrah anasema: Basi yeyote kati yenu atakayeweza kurefusha kuosha uso, basi na afanye)).([13])

Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba alitawadha, akaosha mikono yake hadi akaingia kuosha vipanya vyake, akaosha miguu yake miwili hadi akaingia kuosha miundi yake. Kisha alisema; “Hivi ndivyo nilivyomwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha.([14])

Na imepokelewa tena toka kwake akisema: Nimemsikia kipenzi changu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((تبلغ الحلية من المؤمن حيث يبلغ الوضوء))
((Nuru ya Muumini inafikia pale wudhuu unapofikia)).([15])


12- Kutumia maji kwa uangalifu

Ni kwa Hadiyth ya Anas aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea maji ya lita 2 hadi lita 2½, na akitawadha kwa maji ya ½ lita.([16])


13- Du’aa baada ya kutawadha 
Imepokelewa toka kwa ‘Umar amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ما منكم من أحد يتوضأ فيسبغ ثم يقول:( أشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له، وأشهد أن محمدا عبده ورسوله) إلا فتحت له أبواب الجنة الثمانية يدخل من أيها شاء))
((Hakuna yeyote kati yenu anayetawadha akautimiza vilivyo wudhuu wake, kisha akasema: “Nashuhudia ya kwamba hapana mola mwingine isipokuwa Allaah Aliye Peke Yake na Asiye na mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mja Wake na Mtume Wake, isipokuwa hufunguliwa milango minane ya pepo aingie wowote autakao)).([17])
Imepokelewa na Abu Sa‘iyd kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 ((من توضأ فقال: سبحانك اللهم وبحمدك، أشهد أن لا إله إلا أنت، أستغفرك وأتوب إليك، كتب فى رق ثم طبع بطابع فلا يكسر إلى يوم القيامة))
((Mwenye kutawadha akasema: “Umetakasika ewe Mola na kwa himdi Yako, ninashuhudia ya kwamba hapana mola mwingine ila Wewe, nakuomba maghfira na ninatubia Kwako”, huandikwa katika karatasi nyeupe, kisha hutiwa chapa, halafu haichanwi mpaka siku ya Qiyaama)).([18])


14- Kuswali rakaa mbili baada ya kutawadha

Ni kwa Hadiyth ya ‘Uthmaan aliyesema: “Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha kama hivi ninavyotawadha akasema”:

 ((من توضأ نحو وضوئي هذا، ثم صلى ركعتين لايحدث فيهما نفسه، غفر له ما تقدم من ذنبه))
((Mwenye kutawadha kama wudhuu wangu huu, kisha akasimama akaswali rakaa mbili haizungumzishi nafsi yake, basi husamehewa madhambi yake yaliyotangulia)).([19])

Na imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal wakati wa Swalah ya alfajiri:

 (( يا بلال! حدثني بأرجى عمل عملته فى الاسلام، إني سمعت دف نعليك بين يدي في الجنة)). قال : ماعملت عملا أرجى عندي من أني لم أتطهر طهورا في ساعة من ليل أو نهار إلا صليت بذلك الطهور ما كتب لي أن أصلى))                                                                                                          
  
((Ewe Bilaal! Nielezee amali yenye matarajio zaidi uliyoifanya katika Uislamu, kwani mimi nimesikia mtaharuki wa viatu vyako mbele yangu huko peponi)).
Bilal akasema: “Sikufanya amali yoyote yenye matarajio makubwa kwangu zaidi ya kuwa sikupata kujitwaharisha wakati wowote wa usiku au mchana, ila huswali kwa twahara hiyo kile nilichoandikiwa kukiswali”.([20])

Inajuzu kukausha viungo baada ya kutawadha kwa kutopokelewa lolote la kuzuia hilo. Na asili ni kufaa hilo. Na kama itasemwa kuwa imethibiti kwamba Maymuunah (Allah Amridhie) alimletea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitambaa cha kujifutia baada ya kuoga, na yeye hakujifutia nacho, na akaondoka na ilhali anakung’uta mikono yake miwili.([21])

Tunasema: Tukio hili lina uwezekano wa kuwa na mambo mengi. Inawezekana kuwa alikirejesha kitambaa hicho kutokana na sababu inayohusiana nacho kama vile kutokuwa kisafi, au kuhofia kwake kukilowesha na maji au sababu nyingine. Kisha Bi Maymuunah kumletea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kitambaa hicho, inaonyesha kuwa ilikuwa ni mazoea yake.([22]) Kujuzu huku kunatiliwa nguvu na yale yaliyopokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akaligeuza juba la sufi alilokuwa nalo, kisha akajifuta nalo.([23])
At-Tirmidhiy anasema: “Baadhi ya Maswahaba wasomi wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wa baada yao, wameruhusu kujifuta kwa kitambaa baada ya kutawadha. Na mwenye kulifanya hilo ni makruhu, basi amefanya hivyo kwa yale yaliyosemwa kuwa “wudhuu hupimwa”.


WUDHUU HAUFAI KWA ALIYEPAKA KUCHA RANGI([24])

Kwa vile hilo huzuia maji kupenya na kufika sehemu ya faradhi. Ama rangi nyingine ya kawaidakama vile hina na mfanowe, hiyo haiathiri. Lakini hata hivyo ni vizuri kuiondosha kabla ya kutawadha na kuswali kwa kauli ya Ibn ‘Abbaas: “Wake zetu hujipaka hina bora kabisa. Hujipaka baada ya Swalah ya ‘Ishaa na huiondosha kabla ya Alfajiri”.([25])
Na imepokelewa kuwa Ibraahiym An-Nakh’iy aliulizwa kuhusu mwanamke anayepaka mikono yake hina bila ya kuwa na wudhuu kisha wakati wa Swalah ukafika. Alijibu akisema: “Ataondosha vilivyomo mkononi mwake kama atataka kuswali”.
 
([1]) Hadiyth dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (101), At-Tirmidhiy (25), Ahmad (2/418) na wengineo. Lenye nguvu ni kuwa Hadiyth hii ni dhaifu. Shaykh Al-Albaaniy Allaah Amrehemu katika kitabu cha “Al-Irwaai” (1/122), amesema kuwa ni Hadiyth nzuri. 
([2]) Vitabu vya “Fat-h Al-Qadiyr” (1/22), “Mawaahib Al-Jaliyl” (1/266), “Majmuu’i” (1/385) na “Al-Insaaf” (1/128).
([3]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (159) na Muslim (226).
([4]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim (235), At-Tirmidhiy (28) na Ibn Maajah (405).
([5]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (142), An-Nasaaiy (1/66), Ibn Maajah (407) na Ahmad (4/33).
([6]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (140).
([7]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (168) na Muslim (268).
([8]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (156) toka kwa Ibn ‘Abbaas.
([9]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (157) toka kwa Abdullaah bin Zayd.
([10]) Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na Abu Daawuud (145), Albayhaqiy (1/54), na Al-Haakim (1/149). Angalia kitabu cha “Al-Irwaai” (92).
([11]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Ibn Hibaan (1082) na Albayhaqiy (1/196).
([12]) Hadiyth sahihi: Imetangulia hapo nyuma.
([13]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (36) na Muslim (246).
([14]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim (246).
([15]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim (250).
([16]) Imetolewa na Al-Bukhaariy (198) na Muslim (325).
([17]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim.
([18])  Imetolewa na An-Nasaaiy katika “Al-Kubraa” (9909) na Al-Haakim (1/564). Ina vishuhudilio.
([19]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6433) na Muslim (226).
([20]) Imetolewa na Al-Bukhaariy (1149) na Muslim (2458).
([21]) Imetolewa na Al-Bukhaariy (270).
([22]) Ameielezea katika “Ash-Sharh Al-Mumti’I” (1/181). Pia tizama “Zaad Al-Ma’ad” (1/197).
([23]) Isnadi yake iko karibu na Hadiyth hasan: Imetolewa na Ibn Maajah (468,3564).
([24]) Imenukuliwa toka kitabu changu “Fiqh Ssunnat Linnisaai”.
([25]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Ibn Abi Shaybah (1/120).

0 Comments