026-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Yanayotengua Wudhuu -1

YANAYOTENGUA WUDHUU

1-    Ni kutoka mkojo, au kinyesi, au upepo katika moja ya njia mbili (utupu wa mbele au wa nyuma)
Ama mkojo na kinyesi, ni kwa neno Lake Subhaana:
«أو جاء أحد منكم من الغائط»
«Au mmoja wenu ametoka chooni»([1])

“Al-Ghaaitw” ni kinaya cha kukidhi haja ndogo au haja kubwa. Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa wudhuu unatenguka kwa kutoka kinyesi au mkojo toka moja ya njia mbili (mbele na nyuma).([2])

Ama ikiwa vitatoka sehemu isiyo ya mbele au nyuma kama kutoka kwenye jeraha la kwenye kibofu au tumbo, hapa wanachuoni wamevutana. Wanachuoni wenye kukizingatia kile tu kinachotoka (kitu chenyewe) kama Abu Haniyfah, Ath-Thawriy, Ahmad na Ibn Hazm, hao wamesema: “Wudhuu unatenguka kwa kila najisi inayobubujika toka mwilini iliyotokea sehemu yoyote”. Ama wale wenye kuyazingatia matokeo mawili (nyuma na mbele) kama Ash-Shaafi’iy, hao wamesema: “Unatenguka kinapotoka kitu chochote toka sehemu hizo mbili hata kama si najisi kama kijiwe na mfanowe”.([3])

Ama upepo, ikiwa utatoka kwa nyuma, sawasawa kwa sauti au bila sauti, basi unatengua wudhuu. Hii ni kwa ijmaa ya Maulamaa na kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((((لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ
((Allaah Haikubali Swalah ya mmoja wenu anapopata hadathi mpaka atawadhe)).

Mtu mmoja toka Hadhramawt akauliza: “Ni nini hadathi ewe Abu Hurayrah? Akajibu: “Ni ushuzi wa kimya kimya na ushuzi wa sauti ”.([4])

Na ikiwa upepo utatokea mbele, jamhuri ya Maulamaa([5]) wamesema kuwa unatengua. Lakini Abu Haniyfah aliyeungwa mkono na Ibn Hazm amesema kuwa upepo huo hautengui wudhuu kwa vile ushuzi wa kimya na ushuzi wa sauti ni majina mawili ambayo hayaitwi upepo ila tu kama utatokea kwa nyuma.([6])
Ninasema: Ikiwa mtu atauhisi upepo unaojulikana (kwa harufu yake), basi utatengua wudhuu sawasawa ukiwa umetoka kwa mbele au kwa nyuma. Na ikiwa hauna harufu, basi ni ule tu unaotoka nyuma.


ZINDUZI

Mwanamke anaweza kuhisi kitu kinachofanana na upepo kikitoka kwenye utupu wake wa mbele. Hiki si kingine bali ni mjazo na mtaharuki wa ndani kwa ndani na wala si upepo unaotoka. Huo hautengui wudhuu wake, kwani ni kama kuteuka na mfano wake. Lakini ikiwa mwanamke huyo ni yule ambaye njia yake ya haja ndogo na kubwa zimeingiliana, basi atatawadha kiakiba tu kwa kuwepo uwezekano wa kuwa pengine upepo huo umetokea nyuma. Na Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

2-    Kutoka manii, wadii na madhii

Kutoka manii kunatengua wudhuu kwa ijmai ya Wanazuoni([7]) na kunawajibisha kuoga kamaitakavyokuja. Na kila lile lenye kupasisha kuoga, basi linabatilisha wudhuu kwa ijmai ya Wanazuoni.

Na madhii nayo inatengua kwa Hadiyth ya Aliy bin Abi Twaalib Allaah Amridhie aliyesema: “Nilikuwa ni mtu ninayetokwa sana madhii. Nikamwamuru mtu mmoja amuulize Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na heshima ya binti yake. Akamwuliza, naye akasema:

((((توضأ واغسل ذكرك
((Tawadha na uoshe utupu wako)).([8])

Madii pia ni hivyo hivyo. Ni wajibu mtu aoshe utupu wake na atawadhe (kwa kutokwa navyo).

Ibn ‘Abbaas anasema: “Manii, wadii na madhii; ama manii, ni yale ambayo inapasa kuoga kwa kutoka. Ama wadii na madhii, akasema: Osha utupu wako, au nyuchi zako, na utawadhe wudhuu wako wa Swalah”.([9])


FAIDA

Aliyepata bahati mbaya ya kusumbuliwa na kichocho cha mkojo au cha madhii, au akawa mara kwa mara anatokwa na kimoja ya viwili hivyo vilivyotangulia kutokana na kasoro ya kimwili mpaka ikawa ni uzito kwake, basi huyo ataosha nguo yake na mwili wake, na atatawadha kwa kila Swalah kama mwanamke mwenye damu ya istihaadha (maelezo yatakuja). Kisha kile kitakachomtoka akiwa ndani ya Swalah au kati ya wudhuu wake na Swalah yake, hakitakuwa na neno.    


3- Usingizi mzito wa kutojifahamu 

Kaulipokezi zilizokuja kuhusu kutawadha baada ya kulala zimetofautiana, na maana zake kamazinavyoonekana zimegongana. Kuna Hadiyth ambazo maana zake kama zinavyoonekana, huonyesha kuwa kimsingi hakuna kutawadha kwa sababu ya kulala (usingizi), wakati ambapo kuna nyingine maana yake ya nje inalazimisha kuwa kulala ni hadathi (kunatengua). Kwa hivyo basi, Maulamaa katika suala hili, wameelekea mielekeo miwili:

(a) Madhehebu ya kukusanya

(b) Madhehebu ya kutilia nguvu (uzito).

Maulamaa wa madhehebu ya kutilia nguvu, hawa ima wameliondosha kabisa suala la kutawadha baada ya kulala wakisema kuwa (kulala) si hadathi, au ima wameliwajibisha hilo moja kwa moja wakisema kuwa kulala ni hadathi.

Ama Maulamaa wa madhehebu ya kukusanya, hawa wamesema kuwa kulala si hadathi bali ni kwa kuzoeleka kuwa hupelekea katika hadathi. Maimamu hawa wamehitalifiana kuhusu namna ya ulalaji unaowajibisha kutawadha.

Na kutokana na mielekeo hii mitatu ya Maulamaa hawa, pamechipuka kauli nane.([10]) Nazo ni:

 Kwanza - Kulala hakutengui wudhuu kabisa

Haya yameelezewa yakinukuliwa toka kwa kundi la Maswahaba akiwemo Ibn ‘Umar na Abu Musa Al-Ash‘ariy. Nayo ni kauli ya Sa‘iyd bin Jubayr, Mak-huul, ‘Ubaydah As-Salmaaniy, Al-Awzaa‘iy na wengineo. Hoja yao ni:

(a) Hadiyth ya Anas bin Maalik (Allah Amridhie) aliyesema: “Swalah ilikimiwa nailhali Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anazungumza chemba na mtu fulani. Basi aliendelea kuzungumza naye mpaka Maswahaba zake wakalala. Halafu alikuja, akawaswalisha”.([11]) 

(b) Imenukuliwa toka kwa Qataadah akisema: “Nilimsikia Anas akisema: “Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakilala, kisha wanaswali wala hawatawadhi”. Akasema: Nikasema: Je, umesikia toka kwa Anas? Akasema: Ndiyo, naapa kwa Allaah”.([12])

Na tamko jingine lasema: “Wakingojea Swalah, wakasinzia mpaka vichwa vyao vikajigonga (vikainamia chini), kisha husimama wakaswali”.

(c) Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Nililala kwa mama yangu mdogo Maymuunah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama, nami nikasimama upande wake wa kushoto. Akauvuta mkono wangu akanisimamisha upande wake wa kulia. Nikawa kila ninaposinzia, hunivuta ndwele ya sikio. Aliswali rakaa 11”.([13])        

(d) Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas wakati alipolala kwa Maymuunah. Anasema: “…kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilala mpaka nikasikia mkoromo wake, kisha alitoka akaenda kuswali”.([14]) Na katika tamko jingine: “Kisha alisimama, akaswali na wala hakutawadha”.


Pili - Kulala kwa hali yoyote kunatengua wudhuu

Hakuna tofauti kati ya kulala kidogo au kulala sana. Haya ni madhehebu ya Abu Hurayrah, Abu Raafi’i, ‘Urwa bin Zubayr, ‘Atwaa, Al-Hasan Al-Baswriy, Ibn Al-Musayyib, Az-Zuhriy, Al-Mazniy, Ibn Al-Mundhir na Ibn Hazm. Ni chaguo la Al-Albaaniy. Ni kwa hoja zifuatazo:

(a) Ni kwa Hadiyth ya Swafwaan bin ‘Assaal. Amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamuru tunapokuwa safarini, tupukuse (tupanguse kwa maji) juu ya khofu zetu na wala hatuzivui kwa muda wa siku tatu hata kama tutakwenda haja kubwa au ndogo au kulala, ila kwa janaba”.([15])

Wamesema: “Hapa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amechukulia kiujumla usingizi wote wala hakuhusisha usingizi hafifu au mzito, wala hali hii kwa ile, na akaufanya sawa na haja kubwa na ndogo”.

(b) Ni kwa yale yaliyohadithiwa toka kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Allah Amridhie) aliyepokea toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((العينان وكاء السه، فمن نام فليتوضأ))
((Macho mawili ni kizibo cha tundu la nyuma([16]) . Basi mwenye kulala, atawadhe)).([17])

(c) Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 ((إذا نعس أحدكم وهو يصلي فليرقد حتى يذهب عنه النوم، فإن أحدكم إذا صلى وهو ناعس لا يدري لعله يستغفر فيسب نفسه))
((Anaposinzia mmoja wenu wakati anaswali, basi alale mpaka usingizi umwishe, kwani mmoja wenu anaposwali hali ya kuwa anasinzia, hajui pengine yeye anaomba maghfirah huku kumbe anajitukana mwenyewe)).([18])

Katika “Sahihi yake”, Al-Bukhaariy ameitolea dalili Hadiyth hii juu ya ulazima wa kutawadha baada ya kulala. Lakini ninaloliona mimi ni kuwa kuna kijinukta cha kukizungumzia katika utoaji dalili kwa kutumia Hadiyth hii. Ikiwa ataifanya sababu ya kuikatiza Swalah kutokana na usingizi ni kuchelea kujiombea mwenyewe vibaya, au kusoma asichokijua, au kutouhudhurisha moyo wake kukawa hakuna khushui, basi haya hayana uhusiano na kutawadha baada ya kulala. Bali huenda wenye kusema kuwa wudhuu hautenguki kwa usingizi wameitumia dalili hii kuthibitishia hoja yao. Basi atazame.

(d) Wamesema: Maulamaa wote wamekubaliana kwamba ni lazima kutawadha kwa mtu aliyeondokewa na akili kwa wendawazimu au kupotewa na fahamu kwa hali yoyote iwayo. Pia aliyelala.


Tatu - Usingizi mzito unatengua kwa hali yoyote, na mwepesi hautengui

Na hii ni kauli ya Maalik, riwaya ya Ahmad, Az-Zuhriy Rabi‘ah na Al-Awzaa‘iy!! Wameichukulia Hadiyth ya Anas ya kulala Maswahaba kuwa ni usingizi hafifu. Na pia wametolea dalili kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah:

((((من استحق النوم فقد وجب عليه الوضوء
((Mwenye kustahiki kulala, basi imemwajibikia kutawadha)).([19])
Na lililo sahihi ni kuwa Hadiyth hii ni mawquuf.


Nne - Kulala hakutengui ila kama atalala kwa ubavu au kwa kuegemea

Mwenye kulala kwa umbo lolote kati ya maumbo ya Swalah kama kwa staili ya mwenye kurukuu, au mwenye kusujudu, au mwenye kusimama, au mwenye kukaa, basi wudhuu wake hautenguki, sawasawa akiwa katika Swalah au nje ya Swalah. Hii ni kauli ya Hammaad, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake, Daawuud na Ash-Shaafi’iy. Na hoja yao ni:

(a) Ni yale yaliyohadithiwa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake aliyepokea toka kwa babu yake ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((((ليس على من نام جالسا وضوء حتى يضع جنبه
((Hakuna kutawadha kwa aliyelala kwa kukaa mpaka aweke ubavu wake)).([20])
Ni Hadiyth dhaifu, haifai.
  
(b) Ni Hadiyth ya Anas toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

 ((إذا نام العبد في سجوده باهى الله تعالى به الملائكة يقول: أنظروا إلى عبدي روحه عندي وجسده في طاعتي))
((Anapolala mja katika sijida yake, Allaah Hujifaharisha kwake kwa Malaika Akiwaambia: “Mwangalieni Mja Wangu; roho yake iko Kwangu na mwili wake uko katika kunitii Mimi)).([21])

Na wamevipimia vipambo vingine vya mwenye kuswali kwa sijida.

Ninasema: “Hadiyth hii sanadi yake ni dhaifu. Al-Bayhaqiy amesema: “Kisha hakuna linaloashiria kuwa hatoki kwenye Swalah yake. Na makusudio ya yaliyoelezwa - kama yatakuwa ni sawa - ni kumsifia mja anayedumu katika Swalah mpaka usingizi unamlemea…”.


Tano - Hakutengui ila usingizi wa aliyerukuu au aliyesujudu

An-Nawawiy ameinasibisha kauli hii kwa Ahmad. Na huenda mwono wake ni kuwa mwinamo wa kurukuu na kusujudu ulivyozoeleka, hupelekea kutenguka wudhuu.


Sita - Hakutengui ila usingizi wa aliyesujudu 
Kauli hii imepokelewa vilevile toka kwa Ahmad. 


Saba - Usingizi ndani ya Swalah hautengui kabisa, lakini nje ya Swalah hutengua

Kauli hii imepokelewa na Abu Haniyfah kwa mujibu wa Hadiyth iliyotangulia katika kauli ya nne.


Nane - Wudhuu hautenguki kama atalala kwa kuambatisha barabara makalio yake chini, sawasawa ikiwa ni ndani ya Swalah au nje yake, usingizi ukiwa mzito au mwepesi.

Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, kwa vile kwa mujibu wa anavyoona yeye ni kuwa usingizi wenyewe si hadathi, bali ilivyozoeleka ni kuwa hupelekea kwenye hadathi. Anasema Ash-Shaafi’iy: “Kwa vile mwenye kulala, hujiambatisha barabara na ardhi na hakiwezi kutoka chochote isipokuwa hukishtukia”. Ash-Shawkaaniy ameichagua kauli hii.

Ninasema: “Wenye kuisema kauli hii, wameichukulia Hadiyth ya Anas ya kulala Maswahaba juu ya kuwa walikuwa wamekaa. Al-Haafidh katika kitabu chake cha “Al-Fat-h” (1/251) amelijibu hilo kwa kusema: “Lakini katika musnadi ya Al-Bazzaar kwa sanadi sahihi katika Hadiyth hii (panaelezwa): “Wakaweka ubavu wao, wengine wakilala, kisha hunyanyuka wakaswali”.([22])


LENYE NGUVU

Usingizi mzito wa kutojifahamu kiasi ambacho mtu hawezi kusikia sauti, au kuhisi kudondoka kitu toka mkononi mwake, au kutokwa na udenda na mfano wa hayo, bila shaka usingizi huo unatengua wudhuu, kwani ilivyozoeleka hupelekea hadathi. Ni sawasawa ikiwa mtu amesimama, au amekaa, au amelala ubavu, au amerukuu au amesujudu, hakuna tofauti kati ya milalo hiyo.

Na ikiwa wenye kauli ya kwanza wanamaanisha usingizi wa aina hii, basi sisi tuko nao. Na kama si hivyo, basi usingizi mwepesi wa kusinzia ambao mtu huhisi yanayopita, hautengui wudhuu kwa hali yoyote iwavyo. Ni kwa Hadiyth ya kulala kwa Maswahaba mpaka vichwa vyao vikajigonga (vikainama). Pia kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliposwali na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Na kwa haya, zinakusanyika dalili zote zilizokuja katika mlango huu.
Ni Zake Allaah himdi na ihsaan.


FAIDA

Ilivyokuwa usingizi umezoeleka kuwa hupelekea kwenye hadathi yenye kuwajibisha kutawadha, basi kutenguka kwake kutategemezewa kwa mwenye wudhuu kwa mujibu wa mwenyewe alivyolala na kwa jinsi dhana yake itakavyopondokea. Na ikiwa atafanya shaka kama alivyolala kunatengua au la, basi lililo na nguvu ni kuwa asihukumie kutenguka wudhuu wake, kwa vile twahara ni yenye kuthibiti kwa yakini na haiondoki kwa shaka. Na hili ndilo alilolichagua Shaykh wa Uislamu katika kitabu cha “Al-Fataawaa” (21/230).


 
([1])  Surat Al-Maaidah : 6
([2])“Al-Ijmaa’i” (uk. 17) na “Al-Awsat” cha Ibn Al-Mundhir (1/147).
([3])“Al-Muhalla” (1/232), “Bidaayat Al-Mujtahid” (1/40) na “Al-Awsat” (1/137).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (135) na Muslim (135), lakini kwake bila kauli ya Abu Hurayrah.
([5])“Bidaayat Al-Mujtahid” (1/40) na “Al-Ummu” (1/17).
([6])“Al-Muhalla” (1/232) na “Al-Mabswuut” (1/83).
([7])“Al-Ifswaah” (1/78) na “Al-Ijmaa’i” (uk.31).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (269) na Muslim (303).
([9]) Isnadi yake ni sahihi: Al-Bayhaqiy (1/115).
([10]) Ziangalie katika vitabu vya “Al-Muhalla” (1/222-231), “Al-Istidhkaar” (1/191), “Al-Awswat” (1/142), “Fath Al-baariy” (1/376), “Sharhu Muslim” cha An-Nawawiy (370) na “Nayl Al-Awtwaar”(1/241).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6192) na Muslim (376) na tamko ni lake.
([12]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (376) na At-Tirmidhiy (78).
([13]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (117) na Muslim (763) na tamko ni lake.
([14]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (117), Muslim (184) na Ahmad (1/341).
([15]) Hadiyth Hasan: Imetolewa na An-Nasaaiy (1/32), At-Tirmidhiy (3535) na Ibn Maajah (478). Angalia pia kitabu cha “Al-Irwaai” (104).
([16])  "السه" ni tundu la nyuma la haja kubwa, na  "الوكاء"ni uzi unaofungiwa mdomo wa kiriba. Kwa hiyo kuwa macho kwa jicho, kumefanywa ni kama kizibo cha kiriba. Na jicho linapolala, kifuniko hicho huchopoka na hadathi huwa.    
([17]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abu Daawuud (203), Ibn Maajah (477) na wengineo. Ni dhaifu kwa kauli yenye nguvu. Al-Albaaniy ameifanya kuwa ni Hadiyth Hasan.
([18]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (212) na Muslim (222).
([19]) Hadiyth Sahihi Mawquuf: Imetolewa na Ibn Abi Shaybah (1/158) na Abdur-Raaziq (481) ikiwa mawquuf kwa sanadi sahihi. Na imepokelewa ikiwa marfuu. Na si sahihi, kama alivyosema Ad-DaaraQutniy katika “Al’Ilal” (8/954). Angalia “Adh-Dhwa’iyfah” (954).
([20]) Hadiyth Munkar: Imetolewa na ibn ‘Uday katika “Al-Kaamil” (6/2459), Ad-DaaraQutniy (1/160) na At-Twabaraaniy katika “Al-Awsat”.
([21]) Hadiyth Dhaifu: Angalia katika kitabu cha “As-Silsilat Adh-Dhwa’iyfah” (953).
([22]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Al-Bazzaaz. Na kama hiyo hiyo, imetolewa na Abu Daawuud katika kitabu cha “Masaail Ahmad” (uk.318). Na isnadi yake ni sahihi kwa sharti ya ma-Shaykh wawili. Tazama pia katika “Tamaam Al-Minnah” (uk.100).

0 Comments