027-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Yanayotengua Wudhuu - 2

YANAYOTENGUA WUDHUU - 2

4- Kuondokewa na akili kwa kulewa au kupoteza fahamu au wendawazimu
 Hili linatengua wudhuu kwa makubaliano ya Maulamaa wote.([1]) Na kupatwa na mfadhaiko au mshtuko kuna uzito zaidi kuliko kulala.


5- Kugusa utupu bila kizuizi sawasawa ikiwa ni kwa matamanio au bila ya matamanio

Maulamaa wana kauli nne kuhusu kugusa utupu baada ya kutawadha. Kauli mbili kwa kutilia nguvu na kauli mbili kwa kukusanya.


Kauli ya kwanza: Kugusa utupu hakutengui kabisa wudhuu

Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na riwaya moja toka kwa Maalik. Pia kauli hii imepokelewa toka kwa kikundi cha Maswahaba.([2]) Hoja zao ni haya yafuatayo: 
(a) Ni Hadiyth ya Twaaliq bin ‘Aliy kwamba mtu mmoja alimwuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayeugusa utupu wake baada ya kutawadha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

((((هل هو إلا بضعة منك
((Hakika hiyo ni sehemu tu ya mwili wako)).([3])

Na katika kauli nyingine, mtu mwenye kuuliza alisema: “Wakati nikiwa katika Swalah, niliingilia kulikuna paja langu na mkono wangu ukagusa utupu wangu”. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

((((إنما هو منك
((Hakika utupu ni sehemu ya mwili wako)).([4])

(b) Wamesema: Ikiwa uume utaligusa paja, basi hakuwajibishi kutawadha, na hakuna tofauti kati ya mkono na paja. Hakuna mahitilafiano yoyote kati ya Maulamaa katika suala hili. Na wameizungumzia Hadiyth ifuatayo ya Bisarrah([5]) inayogusia amri ya kutawadha kwa kuugusa uume.


Kauli ya pili: Kugusa utupu kunatengua wudhuu kwa hali yoyote

Ni madhehebu ya Maalik – kama anavyojulikana - , Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm. Kauli hii imepokelewa toka kwa Maswahaba wengi.([6]) Hoja yao ni:

(a) Hadiyth ya Bisarrah binti Swafwaan kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((من مس ذكره فليتوضأ))
((Mwenye kuugusa uume wake, basi atawadhe)).([7])

(b) Hadiyth ya Ummu Habiybah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((من مس فرجه فليتوضأ))
((Mwenye kuugusa utupu wake, basi atawadhe)).([8])

Mfano wa Hadiyth hizi mbili umepokelewa katika Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyohadithiwa na Binti Unays, ‘Aaishah, Jaabir, Zayd bin Khaalid na Abdullaahi bin ‘Amri.

Wamesema: Hadiyth ya Bisarrah inatiliwa nguvu kuliko Hadiyth ya Twaaliq. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

(a) Kwamba Hadiyth ya Twaaliq ina kasoro. Imekosolewa na Abu Zar’ah, na Abu Haatim. Na An-Nawawiy katika “Majmu’i” (2/42), amezungumza sana akieleza kuwa wahafidhi wamekubaliana kuifanya Hadiyth hii dhaifu!!

(b) Ingelikuwa ni sahihi, basi Hadiyth ya Abu Hurayrah yenye maana sawa na Hadiyth ya Bisarrah, ingelitangulizwa, kwa vile Twaaliq alikuja Madiynah wakati wanaujenga Msikiti nailhali Abu Hurayrah alisilimu mwaka wa Khaybar baada ya hilo kwa miaka sita. Na kwa ajili hiyo, Hadiyth yake itaondosha hukumu ya Hadiyth ya Twaaliq.([9])

(c) Kwamba Hadiyth ya Twaaliq ni yenye kuubakisha uasili, na Hadiyth ya Bisarrah ni yenye kunukuu. Nayo hutangulizwa kwa vile hukumu za kisheria ni zenye kunukuu yale waliyokuwa wakiyafanya.

(d) Kwamba wapokezi wa kutenguka wudhuu kwa kugusa ni wengi na Hadiyth zake ni mashuhuri zaidi.

(e) Ni kauli ya Maswahaba wengi.

(f) Kwamba Hadiyth ya Twaaliq imechukuliwa kuwa yeye alijikuna paja akaugusa uume wake juu ya nguo kama inavyoonyesha riwaya kuwa yeye alikuwa katika Swalah.


Kauli ya tatu: Wudhuu unatenguka ikiwa kugusa utupu ni kwa matamanio na kama si kwa matamanio hautenguki

Hii ni riwaya toka kwa Maalik, na ni kauli iliyochaguliwa na Al-‘Allaamah Al-Albaaniy.([10]) Wenye kusema hivi, wameichukulia Hadiyth ya Bisarrah juu ya kama itakuwa ni kwa matamanio, na Hadiyth ya Twaaliq juu ya kama si kwa matamanio. Wamesema kuwa kiashirio cha hilo ni neno lake:

((Hakika hiyo ni sehemu ya mwili wako)).

Kwa hiyo kama ataugusa utupu wake bila ya matamanio, basi anakuwa ni kama aliyegusa kiungo chake kingine chochote.


Kauli ya nne: Kutawadha kwa sababu ya kugusa uume kumesuniwa kwa hali yoyote na wala si wajibu

Ni madhehebu ya Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili na Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyah. Ni kauli ambayo Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn - Allaah Amrehemu – anaonekana kuwa ameipondokea zaidi, isipokuwa amelijaalia hilo kuwa ni Sunnah endapo kama ataugusa utupu bila matamanio, na akatilia nguvu kuwa ni wajibu kama ni kwa matamanio kwa njia ya tahadhari.([11])Kwa hivyo wameichukulia Hadiyth ya Bisarrah kuwa ni Sunnah na Hadiyth ya Twaaliq kuwa maswali yaliyoulizwa yalikuwa ni kwa upande wa wajibu.
  

Kauli mbili za mwisho zinazosimamia juu ya mkondo wa kukusanya zinatolewa dalili kwa haya yafuatayo:

(a) Ni kwamba dai la kuwepo “naskh” kwa vile Twaaliq alitangulia kusilimu kabla ya Bisarrah, ni lazima liangaliwe. Kwa vile dai hilo si dalili ya kuwepo “naskh” kwa upande wa wahakiki waliobobea katika fani ya taaluma ya “Uswuul”, kwa sababu aliyetangulia kusilimu anaweza kuwa alihadithia akiwa amenukulu toka kwa mwingine.

(b) Katika maelezo ya Twaaliq, kuna sababu ambayo haiwezi kuondoka, nayo ni kuwa uume ni sehemu ya mwili wake. Na kama hukumu itafungamanika na sababu isiyoweza kuondoka, basi hukumu haiondoki. Kwa hiyo “naskh” haiwezekani kuwepo.

(c) Kisha ni kuwa suala halipelekwi katika “naskh” ila baada ya kushindikana kukusanya na hasahasa tukizingatia kuwa haifai kufanya “naskh” kama ilivyotangulia.

Ninasema (Abu Maalik): Kauli ya mwisho ndiyo yenye nguvu kwa mujibu wa hali. Lakini endapo kama Hadiyth ya Twaaliq bin Aliy itakuwa ni sahihi - na hili liko mbali bali kauli ya kuifanya dhaifu ndiyo yenye mwelekeo zaidi - , basi kauli itakayokuwa na uzito ni ile isemayo kuwa kuugusa uume kunatengua wudhuu kwa hali yoyote, ni sawasawa ikiwa ni kwa matamanio au bila ya matamanio, kwa vile matamanio hayana mpaka na wala hakuna dalili ya kipimo chake. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

                                     

([1]) “Al-Awswat” cha Ibn Al-Mundhir” (1/155).
([2]) “Al-Badaai’i” (1/30), “Sharhu Fat-h Al-Qadiyr” (1/37), “Al-Mudawwanah” (1/8-9) na “Al-Istidhkaar” (1/308 na baada yake).
([3]) Isnadi yake ni tepetepe: Imetolewa na Abu Daawuud (182), At-Tirmidhiy (85) na An-Nasaaiy (1/101). Maulamaa wamehitalifiana juu ya usahihi wake. Kauli yenye nguvu ni kuwa hii ni Hadiyth dhaifu kwa ajili ya Qays bin Twaaliq. Lakini Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi. Kwa hiyo kila mmoja na mwono wake. Na sisi hatuubani wasaa. Na Allaah Ndiye Mwelewa zaidi.
([4]) Isnadi yake ni dhaifu: Imetolewa na Abu Daawuud (183), Ahmad (4/23), Al-Bayhaqiy (1/135) na wengineo.
([5])“Al-Awswat” (1/203). Na tazama pia “Sharhu Ma’aniy Al-Aathar” (1/71-79).
([6]) “Al-Istidhkaar” (1/308), “Al-Mudawwanah” (1/8-9), “Al-Ummu” (1/19), “Al-Majmu’u” (1/24), “Al-Mughniy” (1/178), “Al-Insaaf” (1/202), “Al-Muhalla” (1/235).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abu Daawuud (181), An-Nasaaiy (1/100) na Ibn Hibaan (1112).
([8]) Sahihi kwa vishuhudilio vyake: Imetolewa na Ibn Maajah (481), Abu Ya’aliy (7144) na Al-Bayhaqiy (1/130). Angalia “Al-Irwaa” (117).
([9]) Na kati ya waliosema kuwa hukumu yake imeondoshwa (naskh) ni: At-Twabaraaniy katika  “Al-Kabiyr” (8/402), Ibn Hibaan (3/405), Ibn Hazm katika “Al-Muhalla” (1/239), Al-Haazimiy katika “Al-I’itibaar” (77), Ibn Al-‘Arabiy katika “Al-‘Aaridhwa” (1/117) na Al-Bayhaqiy katika “Al-Khilaafiyyaat”(2/289).
([10]) Angalia vitabu rejea vilivyotangulia vya madhehebu ya Malik na kitabu cha “Tamaam Al-Minna” (uk 103). Hapo ameinasibisha kauli hii kwamba ni chaguo la Ibn Taymiyah. Amesema: “Ninavyokumbuka”. Ninasema: Bali ni madhehebu ya nne ya Ibn Taymiya kama utakavyokuja kuona. Basi Ametukuka Yule Asiyesahau.
([11])“Majmu’u Al-Fataawa” (21/241) na “Ash-Sharhu Al-Mumti’i” (1/233).

0 Comments