028-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Yanayotengua Wudhuu - 3

FAIDA ZINAZOHUSIANA NA YALIYOTANGULIA

(a) Mwanamke akigusa utupu wake atatawadha

Ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake aliyenukuu toka kwa babu yake, amesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((من مس ذكره فليتوضأ، وأيما امرأة مست فرجها فلتتوضأ))
((Mwenye kuugusa uume wake atawadhe, na mwanamke yeyote aliyeugusa utupu wake, basi atawadhe)).([1])

Hadiyth hii inatiliwa nguvu na kauli ya mama wa waumini ‘Aaishah (Allaah Amridhie) isemayo:

“Mwanamke akiugusa utupu wake, atawadhe”.([2])

Na asili ni kwamba wanawake ni washiriki wa wanaume katika hukumu. Na haya ndiyo madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad kinyume na Abu Haniyfah na Maalik!!


(b) Kugusa utupu wa mwingine

Ikiwa mwanaume ataugusa utupu wa mkewe, au mkewe akaugusa uume wake, basi hakuna dalili ya kutenguka wudhuu wa yeyote kati yao isipokuwa tu kama madhii au manii yatamtoka. Hapo wudhuu utatenguka kwa kutokwa na maji hayo na si kwa sababu ya kugusa. Lakini Maalik na Ash-Shaafi’iy wamesema kuwa ni lazima kutawadha([3]) kwa kujengea juu ya madhehebu yao kuwa wudhuu unatenguka kwa kumgusa mwanamke. Baadaye tutakuja kuona kwamba kauli yenye nguvu ni kinyume cha hivyo.
Aidha, wudhuu hautenguki ikiwa mwanamke au mwanamume ataugusa utupu wa mtoto. Maalik amekubaliana na hili. Nayo pia ni kauli ya Az-Zuhriy na Al-Awzaa’iy.([4])


(c) Yote ni sawasawa kuugusa utupu kwa makosa au kwa kukusudia([5])

Ni madhehebu ya Al-Awzaa’iy, Ash-Shaafi’iy, Is-haaq na Ahmad.
Na kundi la Maulamaa linaona kuwa lenye kutengua wudhuu ni kukusudia kuugusa. Kati yao ni Mak-huul, Jaabir bin Zayd na Sa’iyd bin Jubayr. Pia ni madhehebu ya Ibn Hazm aliyetolea dalili kwa neno Lake Subhaanah:

((وليس عليكم جناح فيما أخطأتم ولكن ما تعمدت قلوبكم))
«Wala si lawama juu yenu kwa mlivyokosea, lakini zipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi »([6])

Yenye nguvu zaidi ni kauli ya kwanza. Ibn Al-Mundhir amesema: “Inampasa  aliyekufanya kuugusa utupu kwa maana ya hadathi yenye kuwajibisha kutawadha, akufanye kukusudia kwake au kutokusudia kuwa ni sawa kama ilivyo kwa hadathi nyinginezo”.

Ninasema: “Kukosea na kusahau kwa yanayohusiana na masharti na nguzo, kunasamehewa lakini hakuondoshi hukumu. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.


(d) Kugusa kwa juu ya nguo hakutengui

Kwa vile hili haliitwi kugusa kama inavyoonekana. Linatiliwa nguvu hili na Hadiyth ya Abu Hurayrah ambayo ni marfu’u:

((إذا أفضى أحدكم بيده إلى ذكره ليس بينهما شيئ فليتوضأ))
((Atakapoupeleka mmoja wenu mkono wake katika uume wake bila kuwepo kizuizi, basi atawadhe))([7])


(e) Kugusa tundu ya nyuma hakutengui([8])

Ni kwa vile tundu ya nyuma haiitwi utupu. Na si sahihi kuwekwa mizani moja na uume kwa kutokuwepo sababu jumuishi kati ya kugusa tundu ya nyuma na uume. Na kama mtu atasema kuwa sehemu zote mbili ni mapitio ya najisi, basi atajibiwa kuwa hiyo siyo sababu ya kutenguka wudhuu kutokana na kugusa. Halafu ikiwa kugusa najisi hakutengui wudhuu, basi vipi utatenguka kwa kugusa mapitio yake?!! Hii ni kauli ya Maalik, Ath-Thawriy na wenye rai kinyume na Ash-Shaafi’iy.                                                                                                                                                                                                     


 
([1]) Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na Ahmad (2/223) na Al-Bayhaqiy (1/132).
([2]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Ash-Shaafi’iy katika “Musnadi yake” (90) na Al-Bayhaqiy (1/133). Al-Haakim amesema ni sahihi (1/138).
([3]) “Mawaahib Al-Jaliyl” (1/296) na “Al-Ummu” (1/20).
([4])“Al-Kaafiy” cha Ibn ‘Abdi Al-Barri (1/149) na “Al-Awswat” (1/210).
([5]) “Al-Muhalla” (1/241) na “Al-Awswat” (1/205-207).
([6]) Surat Al-Ahzaab : 5
([7]) Hadiyth Hasan: Imetolewa na Ad-Daar Qutwniy (1/147) na Al-Bayhaqiy (1/133). Na tazama pia katika “Asw-Swahiyhah” (1235).
([8])“Al-Muhalla” (1/238) na “Al-Awswat” (1/212).

0 Comments