029-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Yanayotengua Wudhuu - 4

6- Kati ya yanayotengua wudhuu ni kula nyama ya ngamia

Aliyekula nyama ya ngamia sawasawa ikiwa mbichi, iliyopikwa au ya kuchoma, ni lazima atawadhe. Hii ni kwa Hadiyth ya Jaabir bin Samrah anayesema kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Je, tutawadhe kwa kula nyama ya kondoo au mbuzi?” Akamjibu:
 ((إن شئت توضأ، وإن شئت فلا تتوضأ))

((Ukitaka tawadha, ukitaka usitawadhe)).

Akamuuliza: “Je, tutawadhe kwa kula nyama ya ngamia?” Akasema:

 ((نعم، توضأ من لحوم الابل))

((Ndiyo, tawadha ukila nyama ya ngamia)). ([1])

Na imepokelewa toka kwa Al-Barra bin ‘Aazib kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((((توضأوا من لحوم الابل، ولا توضأوا من لحوم الغنم

((Tawadheni kwa kula nyama ya ngamia, na wala msitawadhe kwa kula nyama ya kondoo na mbuzi)).([2])
                                                                                 
Na haya ni madhehebu ya Ahmad, Is-haaq, Abu Khaythamah, Ibn Al-Mundhir na Ibn Hazm. Pia ni moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy na ni chaguo la Shaykh wa Uislamu. Aidha, ni kauli iliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Umar na Jaabir bin Samrah.

Lakini Jamhuri ya Maulamaa kama Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ath-Thawriy na kundi la watangu wema, hawa wanaona kwamba si lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia bali ni Sunnah([3]) kutokana na Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Amri mbili za mwisho toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kutotawadha kwa kile kilichoguswa na moto (kilichopikwa)”.([4]) Wakiizungumzia kauli hii wamesema: “Neno lake “kile kilichoguswa na moto” linakusanya nyama ya ngamia vilevile, nayo imethibiti kunasikhiwa”.

Hili linajibiwa kwa mambo mawili:([5])

La kwanza:
Ni kwamba Hadiyth ya Jaabir ni jumuishi, na yale yaliyopokelewa katika kutenguka wudhuu kwa kula nyama ya ngamia ni hali maalumu. Na jambo jumuishi hubebeshwa juu ya jambo maalumu, na hapo hutoka lile ambalo limethibitishwa na dalili kulifanya ni maalumu. Na hapa naskhi haizungumziwi kwa vile inawezekana kukusanya.

La pili:
Amri iliyokuja kuamuru kutawadha kwa kula nyama ya ngamia, bila shaka ni hukumu inayohusiana na kilichopikwa au kibichi. Kwa hiyo kuguswa na moto hakuwajibishi kutawadha, na kwa hivyo hukumu yake inakuwa nje ya habari zilizokuja kuhusu kutawadha kwa kula kilichopikwa na kwa ku-naskh wudhuu.

Baadhi yao wanasema kwamba makusudio ya wudhuu katika Hadiyth ni kuosha mkono!!([6]) Hili ni batili kwani hakuna wudhuu mwingine uliokuja kupitia maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zaidi ya wudhuu wa Swalah. Kisha, katika Hadiyth ya Jaabir bin Samrah iliyopokelewa na Muslim, amri ya kutawadha kwa sababu ya kula nyama ya ngamia, imefungamanishwa na kuswali katika sehemu ya malalio yao kwa kutofautisha kati ya hilo na kuswali katika mapumzikio ya mbuzi. Hivi ndivyo unavyojulikana wudhuu wa Swalah bila mjadala.


LENYE NGUVU

Ni kuwa ni lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia kwa hali yoyote ile. Na kwa ajili hiyo, An-Nawawiy katika kitabu cha “Sharh Al-Muslim” (1/328) anasema: Madhehebu haya yana nguvu zaidi ingawa Jamhuri ya Maulamaa wako kinyume nayo.


TANBIHI

Ya kwanza:
 Katika “Sharh Al-Muslim” (1/328), An-Nawawiy ameinasibisha kauli ya kutolazimu kutawadha kwa kula nyama ya ngamia kwa Makhalifa Wanne Waongofu!! Madai haya hayana dalili yoyote wala haijulikani sanadi yoyote kwao inayohusiana na hilo. Ibn Taymiyah (Allaah Amrehemu) ametanabahisha kuhusu madai haya akisema: “Ama yule aliyenukulu toka kwa Makhalifa Waongofu au Jamhuri ya Maswahaba kwamba wao walikuwa hawatawadhi kwa kula nyama ya ngamia, basi bila shaka amewakosea. Hilo anakuwa amelidhania tu kutokana na yale yaliyonukuliwa kuhusu wao ya kuwa walikuwa hawatawadhi kwa kula kilichoguswa na moto…”([7])

Ya pili:

 KISA MASHUHURI CHA UZUSHI([8])

Kimetangaa baina ya watu wa kawaida kisa wanachokihadithia mara kwa mara. Kisa hiki wamekisikia toka kwa wanafunzi wanaoeleza kwamba ni lazima kutawadha kwa kula nyama na ngamia. Kisa hiki kinaeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika kundi la Maswahaba wake, akasikia harufu (ya upepo) kwa mmoja wao. Swahaba huyo akaona hayaa kunyanyuka kati ya watu (kwenda kutawadha) naye alikuwa amekula nyama ya ngamia. Hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 ((من أكل لحم جزور فليتوضأ))

((Aliyekula nyama ya ngamia akatawadhe)).

Hapo wote waliokuwa wamekula ngamia wakanyanyuka wakatawadha!!
Kisa hiki ni dhaifu kwa upande wa sanadi na munkari kwa upande wa matini.
                                                                                                                 


([1]) Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim (360) na Ibn Maajah (495).
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (184), At-Tirmidhiy (81) na Ibn Maajah (494).
([3])“Al-Mabsuut” (1/80), “Mawaahib Al-Jaliyl” (1/320), “Al-Majmuu” (1/57), “Al-Mughniy” (1/138),“Al-Muhalla” (1/241) na “Al-Awsat” (1/138).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (192), At-Tirmidhiy (8) na An-Nasaaiy (1/108).
([5])“Al-Muhalla” (1/244) na “Al-Mumti’i” (1/249).
([6]) “Majmuu’ Al-Fataawa” (21/260 na baada yake).
([7])“Al-Qawaaid An-Nuuraaniyyah” (uk.9) ikinukulu toka kwa “Tamaam Al-Minnah” (uk.105).
([8]) Tazama “Adh-Dhwaiyfah” ya Al-Albaaniy (1132) na “Qaswasun Laa Tathbut” cha Mash-huur Hasan (uk.59).

0 Comments