030-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Yasiyotengua Wudhuu

Mambo Yasiyotengua Wudhuu


Mambo haya Maulamaa wamehitilafiana juu ya kutengua kwake wudhuu. Na kwa kuyatafiti kwa kina, itabainika kwamba hayatengui. Kati ya mambo hayo ni:


1- Mwanaume kumgusa mwanamke bila ya kizuizi

Suala hili lina kauli tatu za Maulamaa:

Kauli ya kwanza:

Mwanamume kumgusa mwanamke kunatengua wudhuu kwa hali yoyote. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy. Ibn Hazm amemuunga mkono. Ibn Mas’uud na Ibn ‘Umar wamesema hivyo hivyo.([1])


Kauli ya pili:

Hakutengui kwa hali yoyote. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Muhammad bin Al-Hasan Ash-Shaybaaniy. Pia ni kauli ya ‘Abbaas, Twaawuus, Al-Hasan na ‘Atwaa. Kauli hii pia imeungwa mkono na Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyah,([2]) nayo ndio kauli yenye nguvu.


Kauli ya tatu:

Kugusa kunatengua kama ni kwa matamanio. Haya ni madhehebu ya Maalik na Ahmad kama ilivyo mashuhuri kwake.([3])


Ninasema (Abu Maalik): Kigezo cha kimsingi walichokitolea dalili waliosema kwamba wudhuu unatenguka kwa kumgusa mwanamke ni kauli Yake Allaah Mtukufu:

« أو لا مستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا»
«..au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni..»([4])

Imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn Mas’uud na Ibn ‘Umar wakisema kwamba “kugusa ni chini ya daraja ya kuingilia”.([5])
Lakini Mwanachuoni Mkubwa wa Ummah Ibn ‘Abbaas amehitilafiana nao akasema: “Kugusa na “mubaasharah”, kunamaanisha kuingilia, lakini Allaah Hukifanyia kinaya Akitakacho kwa Akitakacho”.([6])

« يا أيها الذين آمنوا إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا»
«Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalah, basi osheni…»([7])

« وإن كنتم جنبا فاطهروا »
«..na mkiwa na janaba, basi ogeni...»

« وإن كنتم مرضى أو على سفر أو جاء أحد منكم من الغائط أو لامستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا»
« Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake na hamkupata maji, basi tayamamuni…»

Na neno Lake:
  « فتيمموا»
« Basi tayamamuni ».

Hii inaonyesha twahara mbili. Kwa hiyo neno Lake:
  « أو جاء أحد منكم من الغائط »
«..au mmoja wenu ametoka chooni… »

Ni ubainisho wa sababu ndogo. Na neno Lake:
 «  أو لامستم النساء »
«Au mmewagusa wanawake...»

Ni ubainisho wa sababu kubwa.([8])

Ijulikane kwamba taawili ya Ash-Shaafi’iy mwenyewe ya maana ya aya tukufu, haikuwa kwa njia ya kukata moja kwa moja, bali inavyoonekana kutokana na maelezo yake ni kuwa yeye amelielezea hilo kwa aina fulani ya tahadhari.([9])

Ninasema (Abuu Maalik): Na kati ya yanayotilia nguvu kwamba kumgusa mwanamke hakutengui wudhuu ni haya yafuatayo:

(a) Ni Hadiyth ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: “Nilimkosa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) usiku kitandani. Nikapapasa kumtafuta na mkono wangu ukagusa tumbo la nyayo zake mbili zikiwa zimesimamishwa na yeye yuko katika sijdah. Alikuwa akisema:
((اللهم إني أعوذ برضاك من سخطك))
((Ewe Mola! Hakika mimi najilinda kwa radhi Zako kutokana na hasira Zako)).([10])

(b) Na imepokelewa vile vile kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema: “Nilikuwa nikilala mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hali ya kuwa miguu yangu iko sehemu yake ya Qiblah. Anaposujudu, alikuwa akinibonyeza na mimi huikunja miguu, na anaposimama nainyoosha”. Anaongeza akisema: “Na nyumba nyakati hizo zilikuwa hazina taa”.([11])
Na katika tamko jingine: “Hata anapotaka kuswali witri, alikuwa akinigusa kwa mguu wake”.([12])

(c) Waislamu walikuwa siku zote wakiwagusa wake zao. Na hakuna yeyote aliyenukulu toka kwake (Mtume) kuwa alikuwa akiwaamuru Waislamu kutawadha kwa kufanya hilo. Na wala haikunukuliwa toka kwa Maswahaba wakieleza kwamba alitawadha kutokana na hilo katika maisha yake. Na wala haikunukuliwa kutoka kwake kwamba alitawadha kwa sababu ya hilo, bali lililonukuliwa kutoka kwake katika “As-Sunan” ni kuwa yeye alikuwa akiwapiga busu baadhi ya wakeze na wala hatawadhi.([13]) Usahihi wa Hadiyth hii una hitilafu. Lakini hata hivyo, hakuna hitilafu kuhusu kwamba haikunukuliwa kuwa yeye alitawadha kwa sababu ya kumgusa (mwanamke).([14])

Ama kauli ya kutenguka wudhuu kwa kugusa kwa matamanio au kutotenguka kwa kugusa bila matamanio, kauli hii haina hoja. Lakini hata hivyo inaweza kusemwa: “Ikiwa atatawadha kwa sababu amemgusa mwanamke kwa matamanio lakini bila ya kumwingilia, basi itakuwa ni vizuri kwa ajili ya kuzima matamanio kama ilivyokuwa imesuniwa kutawadha kwa sababu ya hasira ili kuzituliza. Ama kulazimu kutawadha, hilo haliko. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


2- Kutoka damu sehemu isiyo ya kawaida sawasawa ikiwa ni kwa jeraha au kuumikwa, au ikiwa ni nyingi au kidogo

Hili halitengui kwa mujibu wa kauli mbili sahihi za Maulamaa. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy na Maalik. Lakini Abuu Haniyfah anasema kwamba hili linatengua. Na wafuasi wa Hanbali wanasema kuwa wudhuu hutenguka kama damu ni nyingi.([15]) Kauli ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi kutokana na mambo yafuatayo:

(a) Hadiyth zinazowajibisha kutawadha kutokana na kutokwa damu hazina usahihi wowote.

(b) Ni kwamba asili (ya mambo) ni uhalali. Kwa hiyo anayetawadha wudhuu sahihi, wudhuu huu hautenguki ila kwa matini au Ijmaa’.

(c) Ni Hadiyth ya Jaabir bin Abdillaah katika kisa cha vita vya Dhaat Ar-Riqaa’i. Anasema: “Swahaba Muhaajir alilala na mwenzake Muanswari alisimama kuswali. (Akiendelea kuswali) mtu mmoja alimlenga mshale. Akauchomoa akauweka mpaka ikafikia mishale mitatu. Kisha alirukuu na kusujudu na mwenzake (aliyelala) akagutuka. Na alipojua (mlenga mshale) kuwa wao wataweza kumkamata, alikimbia. Na mara Swahaba Muhaajir alipoziona damu zikimchuruzika Muanswari alisema: “ Subhaana Allaah. Kwa nini usingenigutusha mara tu alipokulenga? Akasema: “Nilikuwa nikiisoma Surah na wala sikupenda kuikatisha”.([16])

Inavyojulikana ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilijua hilo na wala hakumkatalia kuendelea kwake na Swalah baada ya kutokwa na damu. Na lau kama damu ingelikuwa inatengua wudhuu, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelimbainishia hilo na wengineo wote waliokuwepo katika vita hivyo. Na kuchelewa kutoa maelezo wakati yanapohitajika haijuzu.([17])

(d) Imethibiti kuwa ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipochomwa kisu, aliswali na hali jeraha lake linafuka damu. 

(e) Habari zimetangaa kutoka zama hadi zama kwamba Maswahaba waliokuwa wakipigana Jihadi, walikuwa wakipata maumivu ya majeraha. Hakuna anayeweza kupinga kwamba majeraha haya hayakuwa yakitoka damu na nguo zao kutapakaa damu. Pamoja na haya, walikuwa wakiswali hivyo hivyo. Na hakuna yeyote aliyenukulu toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliwaamuru watoke kwenye Swalah au wasiswali. Na kwa ajili hiyo, Al-Hasan Al- Baswriy anasema: “Waislamu wangali wanaswali na majeraha yao”.([18])


3- Kutapika na mfano wake

Madhehebu ya Maulamaa katika suala hili, yako vilevile kama yalivyo katika suala la kutokwa damu. Na lililo sahihi ni kuwa kutapika hakutengui wudhuu kwa vile hoja zinazowajibisha kutawadha, hazina usahihi wowote na kwamba asili ya mambo ni uhalali.

Ama Hadiyth ya Mi’idaan bin Twalha aliyenukuu toka kwa Abu Ddardaai kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua kisha akatawadha. Hakuna shaka kwamba Hadiyth hii haimaanishi kuwa ni lazima kutawadha kama mtu ametapika, kwani hicho ni kitendo tu. Na lengo la kitendo hicho ni kuonyesha kuwa ni vizuri (mustahabbu) kufanya hivyo. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. ([19])


4- Kucheka ndani ya Swalah au nje yake

Maulamaa kwa sauti moja wamekubaliana kwamba kucheka nje ya Swalah hakutengui twahara wala hakuwajibishi kutawadha, na wamekubaliana kwamba kucheka ndani ya Swalah huibatilisha. Na Maulamaa hao wamehitalifiana katika kutenguka wudhuu kwa kucheka ndani ya Swalah. Madhehebu ya Abu Haniyfah, wenye rai, Ath-Thawriy, Al-Hasan na An-Nakh’iy ni kwamba hilo hutengua wudhuu. Wao wameitolea hoja Hadiyth Munqati’iisiyozingatiwa. Ni Hadiyth ya Abu Al-‘Aaaliyah isemayo: “Mtu mmoja kipofu alikuja hali ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaswalisha watu. Mtu yule aliporomoka katika shimo ndani ya msikitini na kundi la watu wakacheka. Hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaamuru waliocheka watawadhe na waswali tena”.([20])

Hadiyth iliyothibiti ni ya Jaabir, nayo ni Hadiyth Mawquuf isemayo: “Ni kwamba aliulizwa (Mtume) kuhusu mtu anayecheka ndani ya Swalah”. Naye akajibu:
((يعيد الصلاة ولا يعيد الوضوء))
((Ataswali tena, lakini hatotawadha upya)).([21])

Na Hadiyth hii ndio sahihi. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy, Maalik, Ahmad, Is-haaq na Abu Thawr.([22])


5- Kuosha maiti
Mwenye kumwosha maiti au kumbeba, basi wudhuu wake hautenguki kwa mujibu wa kauli yenye nguvu. Lakini baadhi ya Maulamaa wanaona ni vizuri kuoga kwa yule aliyemwosha maiti na kutawadha kwa aliyembeba. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah anayesema kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((من غسل ميتا فليغتسل، ومن حمله فليتوضأ))
((Mwenye kumwosha maiti aoge, na mwenye kumbeba atawadhe)).([23])
Hii ikiwa Hadiyth hii ni sahihi.


6- Kufanya shaka aliyetawadha kutenguka wudhuu wake

Mwenye kutawadha wudhuu sahihi, kisha akafanya shaka kama wudhuu umemtenguka au la, basi atabakia juu ya uasili wa kile alichokiyakinisha katika utwahara mpaka atakapoyakinisha kutenguka wudhuu wake. Na ikiwa atafanya shaka na ilhali yuko ndani ya Swalah, basi hatoivunja mpaka ayakinishe kutenguka wudhuu. Hii ni kwa Hadiyth ya Abdullaah bin Zayd aliyesema: “Mtume alishtakiwa kuhusu mtu anayekuwa na wasiwasi katika Swalah”. Mtume akasema:
((لا ينصرف حتى يسمع صوتا أو يجد ريحا))
((Haivunji mpaka asikie sauti au anuse harufu)).([24])

Al-Baghawiy katika “Sharhu as-Sunnah” (1/353) amesema: Mpaka apate uhakika wa hadathi, kwa vile kusikia sauti au kuwepo harufu ni sharti.


 
([1])“Al-Ummu” (1/15), “Al-Majmu’u” (2/23 na baada yake) na “Al-Muhalla” (1/244).
([2])“Al-Mabsuutw” (1/68), “Al-Badai’i” (1/30), “Al-Awsatw” (1/126) na “Majmuu’ Al-Fataawa”(21/410).
([3])“Al-Mudawwanah” (1/13), “Haashiyat Ad-Dusuuqiy” (1/119), “Al-Mughniy” (1/192) na “Kash-Shaaf Al-Qinaa’i” (1/145).
([4]) Surat Al-Maaidah: 6
([5]) Kauli sahihi: “Tafsiri At-Twabariy” (1/502) kwa sanadi tofauti sahihi.
([6]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na At-Twabariy (9581) na Ibn Abu Shaybah (1/166).
([7]) Surat Al-Maaidah : 6
([8])“Ash-Sharh Al-Mumti’i” (1/239) na mfanowe katika ”Al-Awswat” (1/128).
([9]) Ameyaelezea haya Shaykh Al-Mash-huur Allaah Amhifadhi katika uhakiki wake wa “Masuala yenye mivutano” (2/217).
([10]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (222), Abuu Daawuud (865) na At-Tirmidhiy (3819).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (382), Muslim (272) na wengineo.
([12]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na An-Nasaaiy (1/101).
([13]) Maimamu wameitia doa: Imetolewa na Abuu Daawuud (178) na An-Nasaaiy (1/104). Na waliotangulia wameitia ila. Tazama “Sunan Ad-Daar Qutwniy” (1/135-142).
([14])“Majmuu’ Al-Fataawa” (21/410, 20/222) na sehemu nyinginezo.
([15])“Al-Ummu” (1/180), “Al-Majmuu’” (2/55), “Al-Istidhkaar” (2/269), “Al-Mabswuutw” (1/74) na “Al-Mughniy” (1/184).
([16]) Isnadi yake ni dhaifu: Imetolewa na Al-Bukhaariy kama ni Hadiyth Mu’allaq (1/280), Ahmad ameitoa kama ni Hadiyth Mawswuul (195), Ahmad (3/343), Ibn Hibaan (1096), Al-Haakim (1/156) na Ad-Daar Qutwniy (1/223) na sanadi yake ni dhaifu kwa sababu ya ‘Uqayl bin Jaabir. Katika “Swahiyh Abi Daawuud” (193), Al-Albaaniy ameiona kuwa ni sahihi!!
([17])“As-Sayl Al-Jarraar” (1/99).
([18]) Imetolewa na Al-Bukhaariy kama ni Hadiyth Mu’allaq (1/280). Na Ibn Abi Shaybah ameifanya kuwa Hadiyth Mawswuul kwa sanadi sahihi kama ilivyo katika “Al-Fat-h” (1/281).
([19]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na At-Tirmidhiy (87) na Abu Daawuud (2381). Tazama “Al-Irwaa” (111).
([20]) Isnadi yake ni dhaifu sana: Imetolewa na Ad-Daar Qutwniy (1/162) na Ibn ‘Uday (2/716).
([21]) Hadiyth Sahihi Mawquuf: Imetolewa na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq (1/280), Al-Bayhaqiy kama Hadiyth Mawswuul (1/144) na Ad-Daar Qutwniy (1/172).
([22])“Al-Majmuu’i” (2/61), “Al-Kaafiy” (1/151), “Al-Mughniy” (1/117) na “Al-Awswatw” (1/227).
([23]) Imetolewa na Abuu Daawuud (3162), At-Tirmidhiy (993), Ibn Maajah (1463) na Ahmad (2/433). At-Tirmidhiy, Ibn Hajar na Al-Albaaniy wameifanya Hadiyth Hasan katika “Al-Irwaa” (1/174). Lakini linaloonekana ni kuwa inahitaji kuchunguzwa zaidi!! Kwani imetiwa kasoro.
([24]) Hadiyth Sahihi: Imetangulia kuelezwa hivi karibuni.

0 Comments