031-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Wudhuu Unapasa Kwa Ajili Ya Swalah Basi Na Si Vinginevyo

Wudhuu Unapasa Kwa Ajili Ya Swalah Basi Na Si Vinginevyo

Wudhuu unapasa kwa yule anayetaka kuswali – kama hana wudhuu – sawasawa ikiwa Swalah ni ya faradhi, Sunnah au maiti. Hii ni kwa neno Lake Subhaanahu wa Ta’ala:
« يا أيها الذين آمنوا إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا»
‹ Enyi mlioamini! Mnaposimama kuswali, basi osheni…..› ([1])

Na kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 ((لايقبل الله صلاة بغير طهور))
((Allaah Haikubali Swalah bila ya wudhuu))([2])

Na haipasi kutawadha kwa jambo jinginelo lisilokuwa Swalah, na wala haikatazwi kwa asiyekuwa na wudhuu kufanya jambo jingine lolote isipokuwa Swalah. Lakini wudhuu umesuniwa katika mambo yafuatayo:


Kutufu Ka‘abah

“Hatujagundua au kuipata dalili yoyote sahihi na ya wazi yenye kuwajibisha kutawadha kwa wenye kutufu. Maelfu kwa maelfu ya Maswahaba ambao idadi yao hakuna aijuaye ila Allaah, walikuwa wakitufu katika enzi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na wala haikutujia habari yoyote inayoeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamrisha yeyote kati yao kutawadha kwa ajili ya kutufu pamoja na kuwepo uwezekano wa kutenguka wudhuu wa wengi kati yao wakati wa kutufu, na kuingia wengi wao katika ibada hiyo bila ya wudhuu na hususan katika siku hizo ambapo msongamano ulikuwa mkubwa kama katika Twawaaf ya “Quduum” na “Ifaadhwah”.

Na kwa vile hakuna dalili yoyote iliyopokewa juu ya kupasa kutawadha kwa ajili ya Twawaaf, na wala hakuna Ijma’a ya Maulamaa juu ya kupasa hilo pamoja na kuhitajika, basi inabainika kwamba si lazima.([3])

Maulamaa wameitolea dalili Hadiyth Marfu’u ya Ibn 'Abbaas juu ya ulazima wa kutufu isemayo:

((الطواف بالبيت صلاة ‘لا أن الله أباح فيه الكلام))
"Kutufu Nyumba ni Swalah, isipokuwa Allaah Ameruhusu kuzungumza ndani yake".([4])
Wamesema: "Ikiwa Twawaaf ni Swalah, basi inapasa kutawadha kama ilivyo katika Swalah". Lakini kauli yao hii inakataliwa kwa mambo mawili:

Kwanza:  Si sahihi kwamba Hadiyth hii ni Marfu’u. Lililo sawa ni kuwa ni Hadiyth Mawquuf kutokana na maneno ya Ibn 'Abbaas. Aidha, hili limetiliwa nguvu na At-Tirmidhiy, Al-Bayhaqiy, Ibn Taymiyah, Ibn Hajar na wengineo.

Pili: Na kama tukijaalia kama ni Hadiyth sahihi, basi haimaanishi kuwa Twawaaf ni kama Swalah katika kila kitu mpaka ishurutishiwe masharti yanayohusiana na Swalah.([5]) Si hivyo tu, bali Swalah ya kisheria ambayo sharti yake ni utwahara na mfano wake, ni ile inayofunguliwa kwa takbiri na kumalizwa kwa kutoa salaam.

Na kwa ajili hiyo, Shaykh wa Uislamu amesema: "Imenidhihirikia kwamba kujitwaharisha na hadathi, - bila shaka yoyote - hakushurutishwi katika Twawaaf na wala si wajibu. Lakini imesuniwa katika Twawaaf twahara ndogo (wudhuu), kwani dalili za kisheria zinaonyesha kuwa si wajibu, na hakuna katika sheria lenye kuthibitisha wajibu wa kutawadha katika Twawaaf."([6]) Abu Muhammad Ibn Hazm amekubaliana na hili.([7])

Ama kugusa Msahafu:
Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Jamhuri ya Maulamaa, wao wanaona kwamba haijuzu kwa mwenye hadathi kugusa Msahafu.([8]) Kigezo cha ushahidi wao ni:

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:
  ‹لا يمسه إلا المطهرون
‹ Hapana akigusaye ila waliotakaswa › ([9])

2- Hadiyth ya Amri bin Hazm kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaandikia watu wa Yemen barua. Kati ya yaliyoandikwa ni:

((لا يمس القرآن إلا طاهر))
((Asiiguse Qur-aan isipokuwa aliye twahara)).([10])


Ninasema: "Waliyoyatolea ushahidi yanajibiwa kama ifuatavyo:

1- Ama aya tukufu, haiwezekani kuitolea dalili isipokuwa kama kiwakilishi kilichopo katika (يمسه) kitarejeshwa kwa Qur-aan. Na kauli iliyodhahiri iliyoshikiliwa na wafasiri wengi ni kuwa kiwakilishi hicho kinarejea kwa Kitabu kilichohifadhiwa huko mbinguni; nacho ni "Al-Lawh Al-Mahfuudh". Na waliotwaharika ni Malaika. Na hili linaonyeshwa kutokana na muundo wa aya tukufu:

إنه لقرآن كريم۞ في كتاب مكنون۞ لايمسه إلا المطهرون› ›
‹Hakika hii bila ya shaka ni Qur-aan Tukufu ۞ Katika Kitabu kilichohifadhiwa ۞  Hapana akigusaye ila waliotakaswa ›."([11]).

Na hili linatiliwa nguvu na neno Lake Subhaanah:

في صحف مكرمة۞ مرفوعة مطهرة۞ بأيدي سفرة۞ كرام بررة› 
‹Yamo katika kurasa zilizoheshimiwa ۞ Zilizoinuliwa, zilizotakaswa ۞ Zimo mikononi mwa Malaika waandishi ۞ Watukufu wema ›.([12])

2- Ama Hadiyth, basi ni dhaifu na haifai kutolewa dalili, kwa vile imetokana na nyaraka zisizosikikambali na kuwepo mvutano mkali kuhusu wapokezi wake.

Ama kama tukijaalia kuwa Hadiyth hii ni sahihi na kwamba kiwakilishi kinarejea kwa Qur-aan, basi tunasema:

"Kilicho twahara" ni katika visawe matamshi. Inaweza kuwa kwa maana ya Muumini, au kwa maana ya mtu aliyejitwaharisha na hadathi kubwa, au kwa maana ya mtu aliyejitwaharisha na hadathi ndogo, au kwa maana ya mtu ambaye hana najisi katika mwili wake. Hivyo suala inabidi lirejeshwe katika taaluma ya fani ya "Uswuul" isemayo:

"Mwenye kujuzisha kukichukulia kisawe matamshi kwa maana zake zote, basi maana hizo atazichukulia hapa. Lakini kwa vile haijuzu kutumia jina la najisi kwa Muumini asiye na wudhuu au mwenye janaba sawasawa ikiwa ni kweli anayo najisi hiyo, au kimajazi, au kilugha kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((المؤمن لا ينجس))
((Muumini hanajisiki))([13])

mbali na kuthibiti kuwa Muumini daima ni twahara, basi haiwezekani Aayah au Hadiyth kuitumia maana hiyo. Hivyo basi, inalazimu kulichukulia tamshi kwa asiye mushriki kama Alivyosema Allaah Mtukufu:

  ‹ إنما المشركون نجس ›
‹Hakika washirikina ni najsi›([14])
Na kwa Hadiyth iliyokataza kusafiri na Qur-aan kwenda nayo katika nchi ya adui.

Na mwenye kusema kuwa kisawe matamshi kimekusanya maana zote, kwa hivyo hakiwezi kutumiwa mpaka ibainishwe. Atajibiwa kuwa hakuna hoja katika Aayah wala Hadiyth na hata kama jina la "aliyetwaharika" litakuwa na maana ya mtu asiye na hadathi ndogo au kubwa.([15])

Kwa hivyo, inajulikana kuwa hakuna dalili yoyote inayoashiria kuwa ni lazima kutawadha kwa ajili ya kugusa msahafu. Na haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Daawuud na Ibn Hazm. Na ndivyo hivyo hivyo alivyosema Ibn 'Abbaas na kikundi cha watangu wema. Pia Ibn Al-Mundhir yupo katika mkondo huo huo.([16])

 
([1]) Surat Al-Maaidah :6
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (224) na wengineo.
([3]) "Jaami'i Ahkaam An-Nisaai" cha Shaykh wetu Allaah Amlinde (2/515).
([4]) Hadiyth Mawquuf: Imetolewa na At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Al-Haakim na wengineo. Na haifai kuwa ni Hadiyth Marfu’u, bali lililo sawa ni kuwa ni Hadiyth Mawquuf kama alivyobainisha Shaykh wetu Allaah Amnyanyulie cheo chake katika kitabu cha "Jaami'i Ahkaam An-Nisaai" (2/515-521) kinyume na Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy Allaah Amrehemu aliyesema kuwa ni sahihi katika kitabu cha "Al-Irwaa'i" (1/156).
([5]) Tazama katika "Majmu'u Al-Fataawaa" (26/198) na "Jaami'i Ahkaam An-Nisaai" (2/522). Ndani yake kuna tofauti 11 kati ya Swalah na Twawaaf.
([6])"Majmu'u Al-Fataawaa" (26/298).
([7])"Al-Muhalla" (7/179).
([8])"Al-Majmuu'u" (1/17), "Al-Istidhkaar" (8/10), "Al-Mughniy" (1/147) na "Al-Awswat" (2/102).
([9]) Surat Al-Waaqi'ah : 79.
([10]) Hadiyth dhaifu: Ina sanadi dhaifu na baadhi yake ni karatasi tu zisizo na sanadi yoyote. Maulamaa wametofautiana katika kuipandisha ili ifikie ngazi ya Hadiyth Hasan. Na Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi katika kitabu cha "Al-Irwaa" (1/158). Lililo wazi zaidi ni kuwa Hadiyth hii haipandi. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
([11]) Surat Al-Waaqi'ah : 77-79.
([12]) Surat 'Abasa : 13-16.
([13]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (279) na Muslim (371).
([14]) Surat At-Tawbah : 28.
([15]) Limezungumziwa katika "Nayl Al-Awtwaar" (1/260).
([16]) "Al-Badaa'i (1/33), "Haashiyat Ibn "Aaabidiyn" (1/173), "Al-Muhalla" (1/81) na "Al-Awsatw" (2/103).

0 Comments