032-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Faida: Kusoma Qur-aan Kwa Mwenye Hadathi

FAIDA: KUSOMA QUR-AAN - BILA KUIGUSA - KWA MWENYE HADATHI


Hakuna ubaya kusoma Qur-aan kwa mwenye hadathi ndogo au hadathi kubwa bila kugusa msahafu kwa mujibu wa kauli za Maulamaa zenye nguvu. Suala la kusoma Qur-aan ni jepesi zaidi hapa kuliko suala la kugusa msahafu kwa mambo yafuatayo:

1- Hakuna Hadiyth yoyote ya Mtume ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyo marfuuinayokataza kusoma. Kila Hadiyth iliyopokelewa ni dhaifu na haina hoja yoyote. Ni kama Hadiythmarfuu ya Abdullaah bin 'Amr:

((لا يقرأ الجنب ولا الحائض شيئا من القرآن))
((Mwenye janaba au hedhi asisome chochote katika Qur-aan)).

Na Hadiyth ya Ibn Rawaaha:

((نهى رسول الله (ص) أن يقرأ أحد منا القرآن وهو جنب))
((Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza yeyote kati yetu kusoma Qur-aan hali ya kuwa ana janaba)).

Na Hadiyth ya Abdullaah bin Maalik:

((إذا توضأت وأنا جنب أكلت وشربت، ولا أصلي ولا أقرأ حتى أغتسل))
"Ninapotawadha nailhali nina janaba, ninakula na kunywa, lakini siswali wala sisomi mpaka nioge".
Hadiyth zote hizi si sahihi.([1])

2- Imethibiti kutoka kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimtaja Allaah Mtukufu katika nyakati zake zote.([2])

3- Ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamuru wanawake wenye hedhi kutoka siku ya ‘Iyd waketi nyuma ya watu na wafuatilize takbiri zao na du’aa zao.([3])
Kwa hiyo, hii inaonyesha kuwa mwenye hedhi hupiga takbira na humtaja Allaah Mtukufu.

4- Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Aaishah wakati alipokuwa na hedhi:

((إفعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت))
((Fanya yote ayafanyayo mwenye kuhiji isipokuwa tu usizunguke Ka’abah)).([4])
Inajulikana kwamba mwenye kuhiji humtaja Allaah na husoma Qur-aan.

Na kwa vielelezo hivi, inafahamika kuwa mwenye hadathi hazuiliwi kusoma Qur-aan. Shaykh wa Uislamu anasema: "Haya ndiyo madhehebu ya Abu Haniyfah na ndio madhehebu mashuhuri ya Ash-Shaafi'iy na Ahmad".([5])
([1]) Zitazame katika "Al-Irwaa" (192, 485) cha Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy na maelezo ya Shaykh Mash-huur katika "Al-Khilaafiyyaat" cha Al-Bayhaqiy (2/11). Basi ni vizuri yapitiwe.
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (373), na imetolewa maelezo na Al-Bukhaariy kabla ya Hadiyth ya (608).
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (971) na Muslim (890).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1650).
([5])"Majmuu Al-Fataawa" (21/459) na "Al-Awswat" (2/97).

0 Comments