033-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Mambo Yaliyopendezewa Mtu Kuwa Na Wudhuu (Anapoyafanya)

MAMBO YALIYOPENDEZEWA MTU KUWA NA WUDHUU (ANAPOYAFANYA)

1- Wakati wa kumtaja Allaah Mtukufu

Hapa unaingia uradi wowote, kusoma Qur-aan, kutufu Ka’abah na mengineyo.
Wudhuu umesuniwa kwa hayo kutokana na Hadiyth ya Al-Muhaajir bin Qunfudh kwamba yeye alimsalimia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anatawadha, naye hakumjibu mpaka alipomaliza.  Kisha akamwambia:

((إنه لم يمنعني أن أرد عليك إلا أني كرهت أن أذكر الله إلا على طهارة))
((Hakika hakuna kilichonizuilia kukujibu isipokuwa tu niliona uzito kumtaja Allaah isipokuwa niwe katika twahara)).([6])
Na ingawa Hadiyth hii haiambatani na Hadiyth ya 'Aaishah iliyosajiliwa na Muslim (4/68) isemayo: 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimtaja Allaah katika nyakati zake zote.


2- Wakati wa kulala

Imepokelewa toka kwa Al-Barraa bin 'Aazib Allaah Amridhie, amesema: " Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا أتيت مضجعك فتوضأ وضوئك للصلاة، ثم اضطجع على شقك الأيمن، ثم قل: اللهم أسلمت نفسي إليك...))
((Unapotaka kulala, basi tawadha wudhuu wako wa Swalah, kisha lala kwa ubavu wako wa kulia, kisha sema: Ee Mola! Nimeisalimisha nafsi yangu kwako.))([7])


3- Kwa mwenye janaba kama akitaka kula, au kunywa, au kulala, au kumwingilia tena mkewe

Imepokelewa toka kwa 'Aaishah Allaah Amridhie, amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapokuwa na janaba na akataka kula au kulala, alikuwa akitawadha wudhuu wa Swalah".([8])

Na imepokelewa na Abi Sa'iyd Allaah Amridhie toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((إذا أتى أحدكم أهله ثم أراد أن يعود فليتوضأ))
((Anapomwingilia mmoja wenu mkewe kisha akataka kurejea tena, basi atawadhe)).([9])


4- Kabla ya kuoga

Imepokelewa na 'Aaishah Allaah Amridhie, amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akioga janaba, huanza kwa kuosha mikono yake, kisha humimina maji katika mkono wake wa kushoto kwa kutumia mkono wa kulia na kuosha utupu wake, kisha hutawadha wudhuu wake wa Swalah".([10])


5- Baada ya kula kilichopikwa kwa moto

Ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((توضأوا مما مست النار))
((Tawadheni kwa kile kilichopikwa kwa moto)).([11])

Amri hapa ni ya kupendezeshea kutokana na Hadiyth ya 'Amri bin Umayyah Adh-Dhamriy aliyesema: "Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akilikata bega la kondoo, akala sehemu, kisha akaitwa kwenda kuswali, akasimama, akakitupa kisu, akaswali na wala hakutawadha".([12])


6- Kujadidisha wudhuu kwa kila Swalah

Ni kwa Hadiyth ya Buraydah Allaah Amridhie, amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitawadha wakati wa kila Swalah. Na ilipokuwa siku ya ufunguzi, alitawadha, akapukusa juu ya khofu zake, akaswali Swalah nyingi kwa wudhuu mmoja.." Hadiyth.([13])


7- Kila mara wudhuu unapotenguka

Ni kutokana na Hadiyth ya Bilaal iliyotajwa hapo kabla ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisikia mlio wa viatu vyake mbele yake peponi. Akamwambia:

((بم سبقتني إليها))
((Ni kwa jambo gani umenitangulia))?

Akasema: 'Ewe Mtume wa Allaah! Kamwe sikuadhini ila niliswali rakaa mbili, na wala kamwe sikupata hadathi ila nilitawadha".
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

((لهذا)) 
((Ni kwa hili)).([14])


8- Kwa kutapika

Ni kwa Hadiyth ya Mu'daan bin Abi Twalha toka kwa Abu Ad-Dardaai kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua, kisha akatawadha. Kisha alikutana na Thawbaan katika Msikiti wa Damascus akalitaja hilo kwake na Thawbaan akamwambia: "Umesema kweli, na mimi ndiye niliyemmiminia maji yake ya kutawadhia".([15])
 
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (17), An-Nasaaiy (1/16), Ibn Maajah (350), Ad-Daaramiy (2/287) na Ahmad (5/80). Ni Hadiyth Sahihi kama ilivyo katika "As-Silsilat As-Swahiyhah"(834).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (247), Muslim (2710) na wengineo.
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (288), Muslim (305) na tamko ni lake, Abuu Daawuud (222), At-Tirmidhiy (118), An-Nasaaiy (1/138) na wengineo.
([9]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (3/217), Abu Daawuud (217), At-Tirmidhiy (141) na An-Nasaaiy (1/42).
([10]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (248), Muslim (316) na wengineo.
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (351), Abuu Daawuud (192), At-Tirmidhiy (79), An-Nasaaiy (1/105) na Ibn Maajah (485).
([12]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1/50), Muslim (4/45 Nawawiy) na Ibn Maajah (490).
([13]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (277), Abuu Daawuud (171), At-Tirmidhiy (61), An-Nasaaiy (1/89) na Ibn Maajah (510).
([14]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na At-Tirmidhiy alipotaja wudhuu wakati wa hadathi (3689), Abuu Daawuud (3055), Ahmad (21962) na tamko ni lake. Asili yake ni katika Sahihi mbili bila ya sehemu ya ushahidi.
([15]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na At-Tirmidhiy (87) na Abuu Daawuud (2381) kwa sanadi sahihi.

0 Comments