034-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupaka Juu Ya Vizuizi - Kupaka Juu Ya Khufu

KUPAKA JUU YA VIZUIZI
KWANZA
KUPAKA JUU YA KHUFU MBILI
Fasili yake: khufu ni viatu vya ngozi vinavyofunika visigino viwili.([1]) Na kupaka kilugha ni kisoukomo cha kitenzi cha “amepaka”, nako ni kuupitisha mkono juu ya kitu kwa kuukunjua.([2]) Na kupaka juu ya khufu mbili maana yake ni kuitia umajimaji  khufu maalumu katika wakati na mahala maalumu([3]) badala ya kuosha miguu miwili wakati wa kutawadha.

USHERIA WA KUPAKA JUU YA KHUFU MBILI
Wanachuoni wote wamekubaliana kwamba mwenye kutawadha kikamilifu, kisha akazivaa khufu zake mbili, halafu wudhuu ukamtenguka, basi anaruhusika kupukusa juu yake.([4]) Ibn Mubaarak amesema: “Hakuna khitilafu yoyote kuwa  kupukusa juu ya khufu mbili, kunajuzu. Na hii ni kwa vile kila Swahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye imepokelewa toka kwake, amekirihisha kupaka juu ya khufu mbili([5]). Na hakika usheria wake umethibiti kwa Sunnah Sahihi iliyo “Mutawaatir” toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na madhubuti zaidi linaloonyesha usheria huo ni Hadiyth ya Hammam aliyesema: “Jurayr alikojoa, kisha akatawadha, halafu akapakaa juu ya khufu zake. Akaulizwa: Unafanya hivi? Akasema: Ndio. Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekojoa, kisha akatawadha na akapukusa juu ya khufu zake mbili”. Al-A’amash anasema: “Ibrahim amesema: Walikuwa wakiipenda Hadiyth hii, kwani Jurayr alisilimu baada ya kuteremka Surat Al- Maaidah”.([6])

HUKUMU YA KUPUKUSA JUU YA KHUFU MBILI
Kupukusa juu ya khufu mbili kunajuzu, lakini kuosha miguu ni bora zaidi kwa mujibu wa jamhuri ya Wanazuoni. Mahanbali wanaona kwamba kupukusa juu ya khufu mbili ni bora zaidi kwa ajili ya kuifuata ruhusa.([7])
Na lililo sawa ni kuwa lililo bora kwa kila mtu ni kwa mujibu wa mguu wake (kuzivaa au kutozivaa). Aliyevaa khufu mbili, basi apukuse juu yake na wala asizivue kwa ajili ya kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake. Ama yule ambaye hakuvaa, basi aoshe miguu na wala asipanie kuzivaa ili apukuse.([8]) Pia asipanie kuzivua ndani ya muda wake ili aoshe miguu yake. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

MUDA WA KUPUKUSA JUU YA KHUFU MBILI
Sheria imeweka muda wa siku tatu na masiku yake kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi. Haya ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Maulamaa wa Hanafi, Hanbali, Dhaahir na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya na Adh-Dhwaahiriyyah.([9])
Dalili ya hayo ni haya yafuatayo:
1- Ni Hadiyth ya Aliy (Allaah Amridhie) aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameweka muda wa siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.([10])
2- Ni Hadiyth ya ‘Ouf bin Maalik Al-Ashja’iy aliyesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kupukusa juu ya khufu mbili katika Vita vya Tabuk siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.([11])
3- Hadiyth ya Swafwan bin ‘Assal, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini, tusizivue khufu zetu siku tatu na masiku yake ila kwa janaba, lakini si kwa kwenda haja kubwa, au ndogo, au kulala”.([12])
Maalik amekwenda kinyume na haya – nayo ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi’iy - . Yeye anaona kwamba hakuna kuwekwa muda, bali mtu anaweza kupukusa juu ya khufu zake madhali hakuzivua au kupatwa na janaba!! Na ndivyo hivi hivi alivyosema Al-Layth.([13]) Wao wametoa hoja kwa Hadiyth dhaifu. Kati ya Hadiyth hizo ni:
1- Ile iliyopokelewa toka kwa Ubayya bin ‘Ammarah, amesema: “Nilisema: Ewe Mtume wa Allaah! Je, nipukuse juu ya khufu mbili? Akasema: Ndiyo. Nikasema: Siku moja? Akasema: Siku moja. Nikasema: Na siku mbili je? Akasema; Na siku mbili. Nikasema: Na siku tatu je? Akasema: Na siku uzitakazo”.
2- Yale yaliyopokelewa toka kwa Khuzaymah bin Thaabit, amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuwekea siku tatu, na lau kama tungelimtaka atuongezee, basi angetuongezea”.([14]) Yaani kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri. Na hili lau kama lingekuwa ni sahihi, basi haliwezi kuwa ni hoja, kwani ni dhana tu ya Swahaba, na sisi hatukulichukulia kama ni ibada.
3- Yale yaliyopokelewa toka kwa Anas bin Maalik kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((إذا توضأ أحدكم ولبس خفيه فليصل فيهما، وليمسح عليهما، ثم لا يخلعهما إن شاء إلا من جنابة))
((Anapotawadha mmoja wenu akazivaa khufu zake, basi aswali nazo na apukuse juu yake, kisha asizivue muda autakao, isipokuwa kwa janaba)).([15])
Hadiyth zote hizi ni dhaifu na hazifai kutolewa ushahidi.
4- Kauli pokezi iliyopokelewa toka kwa ‘Aamir akisema: “Nilitoka Sham kuelekea Madina. Niliondoka siku ya ijumaa na nikaingia Madina siku ya ijumaa. Kisha niliingia kwa ‘Umar bin Al-Khattab akaniuliza: Ni lini uliziingiza khufu zako kwenye miguu yako? Nikajibu: Siku ya ijumaa. Akauliza: Je, ulizivua? Nikajibu: Hapana. Akasema: Umefanya sawa”.([16])
Hii pia ni dhaifu. Al-Bayhaqiy amesema: “Hakika tumepokea toka kwa ‘Umar kuhusu wakati. Basi inawezekana kuwa ima alirejea katika kauli hiyo wakati ilipomfikia toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au iwe kauli yake iliyowafikiana na Sunnah sahihi na iliyo mashuhuri ni bora zaidi. Na kwa ajili hiyo, Ibn Hazm amesema katika kitabu cha Al-Muhalla (2/93): “Na haisihi kutofautika wakati kwa Swahaba yeyote yule isipokuwa Ibn ‘Umar peke yake”.

KUANZA MUDA WA KUPUKUSA
Imejulikana kwamba muda wa kupukusa kwa mkazi ni siku moja na usiku wake, na kwa msafiri ni siku tatu na masiku yake. Basi ni wakati gani muda huo unaanza kuhesabiwa? Katika hili, Wanachuoni wamesema kauli tofauti:
Ya kwanza
Unaanza pale anapopata hadathi ya kwanza baada ya kuzivaa. Hii ni kauli ya Sufyaan Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy, Abu Hanifa na wenzake. Na hili li wazi katika madhehebu ya Hanbali.([17]) Wao wamesema kuwa kwa vile kipindi cha baada ya  hadathi, ni wakati unaoruhusiwa kupukusa.
Ya pili
Unaanza kuanzia wakati wa kuzivaa. Ni kauli ya Al-Hasan Al-Basriy.([18])
Ya tatu
Atapukusa Swalah tano, yaani Swalah 15 kwa msafiri (3X5), na wala asipukuse zaidi ya hivyo. Ni madhehebu ya Ash-Sha’abiy, Ishaaq, Abu Thawr na wengineo.([19])  
Ya nne
Unaanza pale inapojuzu kwake kupukusa baada ya hadathi, sawasawa alipukusa au hajapukusa na wala hakutawadha kwa namna ambayo lau kama atapukusa baada ya kupita sehemu ya muda, itambidi apukuse ule muda uliosalia basi. Haya ni madhehebu ya Ibn Hazm. Yeye ameyajadili madhehebu mengi, basi yarejewe.([20])
Ya tano
Unaanza tokea pukuso la kwanza baada ya hadathi.([21]) Ni kauli ya Ahmad bin Hanbali na Al-Awzaa’iy. Pia ni kauli iliyoungwa mkono na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn ‘Uthaymiyn. Na hii ndio kauli yenye nguvu zaidi kutokana na maana bayana ya neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 
((يمسح المسافر))  و ((يمسح المقيم))
((Msafiri hupukusa)) na ((Mkazi hupukusa)).
Na haiwezekani kuthibitishwa kwamba mtu anapukusa, ila kwa kitendo cha kupukusa. Na haijuzu kuipiga pande maana hii bayana bila dalili au ushahidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Na kwa haya, ikiwa mtu ametawadha wakati wa Swalah ya adhuhuri na akavaa khufu zake saa sita kwa mfano, kisha akabakia na utwahara wake hadi saa tisa alasiri, kisha wudhuu ukamtenguka na wala hakutawadha mpaka saa kumi (baada ya Swalah ya alasiri) na akapukusa, basi yeye atapukusa mpaka saa kumi alasiri ya kesho yake ikiwa ni mkazi, na siku ya nne ikiwa ni msafiri.

IKIWA MKAZI AMEPUKUSA KISHA AKASAFIRI
Aliyepukusa khufu zake naye ni mkazi kwa muda wa chini ya siku na usiku wake kisha akasafiri, basi Maulamaa wana kauli mbili:
Ya kwanza:
Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa kujumlisha na ule muda aliopukusa kabla ya kusafiri. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake, na riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Ibn Hazm pia amesema hivyo.([22])
Ya pili:
Ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku moja na usiku wake, kisha itampasa aoshe miguu yake anapotawadha. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ishaaq.([23])
Yenye nguvu ni kuwa ni haki yake kupukusa mpaka akamilishe siku tatu na masiku yake kwa vile mtu huyu inapomalizika siku na usiku wake na yeye ni msafiri, basi ana haki ya kuutimiza muda kutokana na uwazi wa maana ya Hadiyth: 
 ((يمسح المسافر ثلاثة أيام ولياليهن))
((Msafiri hupukusa siku tatu na masiku yake)).


IKIWA MSAFIRI AMEPUKUSA KISHA AKAWASILI MJINI KWAKE
Ikiwa msafiri atapukusa juu ya khufu zake siku moja na usiku wake au zaidi kisha akawasili kwake, ni lazima azivue khufu zake, aoshe miguu yake anapotawadha, kisha atakuwa na hali ile ile ya mkazi.
Na ikiwa msafiri amepukusa kwa muda wa chini ya siku na usiku wake, basi inajuzu kwake anapowasili mjini akamilishe muda uliosalia wa siku moja na usiku wake, kisha ni lazima azivue. 
Ibn Al-Mundhir amenukulu ijmaa ya kila Mwanachuoni anayezungumzia kwa kuainisha kuhusu muda wa kupukusa.([24])

([1]) “Nayl Al-Awtwaar” (1/241).
([2])  Kamusi ya “Al-Muhiytw” na “Maqaayiys Al-Lugha”.
([3]) “Ad-Durru Al-Mukhtaar” (1/174).
([4]) “Al-‘Ijmaa” cha Ibn Mundhir (20) na “Al-Awswat” (1/434).
([5]) “Al-Awswat” (1/434), “Sunan Al-Bayhaqiy” (1/272) na “Al-Fath” (1/305).
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (387) na Muslim (1568) na tamko ni lake.
([7]) “Fath Al-Qadiyr” (1/126), “Ash-Sharh Asw-Swaghyr” (1/227), “Al-Majmuu’u” (1/502) na “Muntahaa Al-Iraadaat” (1/23).
([8]) Hili ni chaguo la Shaykh wa Uislamu kama ilivyo katika “Al-Ikhtiyaaraat” (uk.13).
([9]) “Al-Mabswuut” (1/98), “Al-Ummu” (1/34), “Al-Mughniy” (1/209) na “Al-Muhalla” (2/80).
([10]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (276) na An-Nasaaiy (1/84).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ahmad (6/27) kwa sanadi sahihi, nayo ina ushahidi toka Hadiyth ya Abu Bakrah iliyoko kwa Ibn Maajah (556) na wengineo.
([12]) Hadiyth Hasan: Imetajwa hivi karibu.
([13]) “Al-Mudawwanah” (1/41) na “Bidaayat Al-Mujtahid” (1/24).
([14]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (157), At-Tirmidhiy na Ibn Maajah (553).
([15]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Al-Bayhaqiy (1/280).
([16]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Al-Bayhaqiy (1/280), Atw-Twahaawiy (1/48) na Ad-Daar Qutniy (72). 
([17]) “Al-Mabswuut” (1/99), “Al-Majmu’i”(1/470), “Al-Mughniy” (1/291) na “Al-Awswat” (1/443).
([18]) “Al-Ikliyl Sharh Manaar As-Sabiyl” cha Shaykh Wahiyd Abdu Ssalaam (1/136).
([19]) “Al-Mughniy” (1/291), “Al-Majmuu” (1/466) na “Al-Awswat” (1/444).
([20]) “Al-Muhalla” cha Ibn Hazm (2/95 na kurasa zinazofuatia).
([21]) “Masaail Ahmad” cha Abu Daawuud (10) na “Al-Muhalla” (2/95).
([22]) “Ikhtilaaf Al’ulamaa” cha Al- Maruuziy (uk.31), “Al-Mughniy” (1/299) na “Al-Muhalla” (2/109).
([23]) “Al-Ummu” (1/35), “Ikhtilaaf Al’ulamaa” (uk.31) na “Al-Awswat” (1/446).
([24]) “Al-Awswat” (1/446).

0 Comments