035-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Masharti Ya Kupukusa Juu Ya Khufu Mbili

MASHARTI YA KUPUKUSA JUU YA KHUFU MBILI

Kwa ajili ya kujuzu kupukusa juu ya khufu mbili, ni sharti mtu azivae akiwa twahara. Imepokelewa toka kwa Al-Mughyrah bin Shu’ubah amesema: “Nilikuwa na Mtume  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari usiku mmoja. Nilimmiminia maji toka katika chombo, naye  akaosha uso wake na mikono yake, na akapaka kichwa chake. Kisha niliinama mzima mzima ili nizivue khufu zake naye akanambia:
((دعهما، فإني أدخلتهما طاهرتين))
((Ziwache, kwani mimi nimeziingiza (nimezivaa) nailhali miguu ni twahara)).
Kisha akapukusa juu yake.([1])
Na Hadiyth hii imeufanya utwahara kuwa ni sharti ya kujuzu kupukusa kabla ya kuzivaa khufu mbili. Na jambo lenye kufungamanishwa na sharti, halijuzu ila kwa kuwepo sharti hilo. Na wudhuu ndio utwahara wa kisheria uliochukuliwa na jamhuri ya Maulamaa.([2])


FAIDA
Mwenye kutawadha, kisha akaosha mguu wake mmoja halafu akauvisha khufu, kisha akauosha mguu wake mwingine halafu akauvika khufu, basi wudhuu wake unapotenguka, haitojuzu kwake kupukusa kwa sababu alivaa khufu moja kabla ya kukamilisha wudhuu wake. Lakini kama aliivua ya kwanza kisha akaivaa, basi itajuzu kupukusa. Haya yamesemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad.([3])
Ama Abu Haniyfah na Ahmad – katika moja ya riwaya mbili - , Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Shaykh wa Uislamu,([4]) wao wanaona kwamba inajuzu kwake kupukusa juu ya khufu hizo kwa mazingatio ya ukweli kuwa alizivaa katika miguu yake yote miwili hali ya kuwa ni twahara.
Ninasema: Kusema kuwa inajuzu, hakuna tatizo lolote mpaka itakapoonyesha dalili kwamba utwahara haugawanyiki, na hivyo kupelekea kwenye kuzuia. Na kiakiba tu na tahadhari, ni vizuri kuingiza miguu miwili katika khufu baada ya kumaliza kutawadha. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


JE, HUPUKUSWA JUU YA KHUFU ILIYOTOBOKA?
Mafuqahaa wengi wameshurutisha kwamba kwa ajili ya kujuzu kupukusa juu ya khufu mbili, ni lazima ziwe  ni zenye kusitiri mahala palipolazimu kuoshwa katika wudhuu. Kwa ajili hiyo, wamezuia kupukusa juu ya khufu iliyotoboka, kwani huonekana kupitia khufu hiyo, mahala pa viungo vinavyolazimu kuoshwa. Na kuosha na kupukusa haviendi pamoja, na kwa hivyo hukumu ya  kuosha inapewa uzito zaidi.
Haya ndiyo madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad.([5])
Na Maalik na Abuu Haniyfah wamesema kuwa inajuzu kupukusa juu ya khufu iliyotoboka madhali inaweza kutembelewa na jina lake bado lipo. Na hili ndilo neno la Ath-Thawriy, Is-Haaq, Abu Thawr, Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah.([6])
Haya ndiyo sahihi, kwani ruhusa ya kupukusa juu ya khufu mbili ni ya kiujumla na kinaingia kila kile  kinachoitwa khufu kwa mujibu wa ubayana wa khabari. Na khufu haitofautishwi na khufu nyingine ila kwa dalili. Na lau kama kutoboka kunazuia kupukusa, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha hilo na hususan pale walipokuwa Maswahaba wengi ni masikini katika enzi yake. Wengi wao ilikuwa haikosekani khufu zao kuwa na matundu.


MAHALA PA KUPUKUSA NA SIFA YAKE
Linalo ruhusika kisheria, ni kuzipukusa khufu mara moja tu nje (juu)  na sio ndani (chini ya unyayo). Hii ni kwa Hadiyth ya Aliy bin Abi Twaalib aliyesema: “ Lau kama dini ingelikuwa ni kwa rai, basi kupukusa chini ya khufu ingelikuwa ni bora kuliko juu yake. Na hakika nilimwona Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu zake mbili”.([7])
Na haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Abuu Haniyfay na wenzake ([8]). Na haya ndio sahihi.

Maalik na Ash-Shaafi’iy([9])  wamesema: “Hupukusa juu yake na chini yake. Na kama atapukusa juu tu, basi itamtosheleza. Hili limetolewa dalili kwa Hadiyth ya Al-Mughyrah bin Shu’bah aliyesema kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)     alitawadha, kisha akapukusa chini na juu ya khufu zake.
Hii ni kauli dhaifu, lakini lililo na uthibitisho toka kwa Al-Mughyrah ni kauli yake isemayo: “Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu zake mbili”.
Kwa hiyo, kupukusa hakuwi isipokuwa juu ya khufu mbili tu. Na kama atapukusa chini tu akaacha juu, basi kupukusa huko hakutatosheleza. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi
([1]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (206) na Muslim (232).
([2]) “Fath Al-Baariy” (1/370).
([3]) “Al-Muwatwa’a” (1/46), “Al-Ummu” (1/33) na “Al-Mughniy” (1/282).
([4]) “Al-Mabswuut” (1/99), “Al-Awswat” (1/442), “Majmuu’u Al-Fataawaa” (21/209) na “Al-Muhalla” (1/100).
([5]) “Al-Ummu” (1/28), “Masaail Ahmad” cha Ibn Haani (1/18) na “Al- Mughniy” 1/287).
([6]) “Al-Mudawwanah” (1/44), “Al-Mabswuut” (1/100), “Al-Awswat” (1/449), “Al-Muhalla” (2/100) na “Majmuu Al-Fataawaa” (21/173).
([7]) Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (162), Ad-Dar Al-Qutniy (73) na Al-Bayhaqiy (2/111). Tazama “Al-Irwaa” (103).
([8]) “Ikhtilaaf Al-‘Ulamaa” (uk.30), “Masaail Ahmad” cha Ibn Haani (1/21), “Al-Awswat” (1/453) na “Al-Muhalla” (2/111)..
([9]) “Nihaayat Al-Muhtaaj” (1/191), “Al-Mudawwanah” (1/39) na “Al-Khurshiy” (1/177).

0 Comments