037-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupaka Kwenye Soksi Na Viatu

KUPAKA KWENYE SOKSI NA VIATU


1- KUPAKA KWENYE SOKSI

Soksi ni kile anachokivaa mtu miguuni sawasawa zikiwa zimetengenezwa kwa sufi au pamba au katani au mfano wa hivyo.

Maulamaa wana kauli tatu kuhusu hukmu ya kupukusa juu ya soksi:


Ya kwanza:

Haijuzu kupukusa juu yake ila tu kama zitafunikwa na viatu vya ngozi.
Na haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah (kisha baadaye aliachana na msimamo huu), Maalik na Ash-Shaafi'iy[1]. Wao wanasema kuwa sababu ni kuwa soksi haiitwi khufu, na kwa hivyo haichukui hukmu yake, na wala hakuna Hadiyth yoyote inayothibitisha kupukusa juu ya soksi!!


Ya pili:

Inajuzu kupukusa juu ya soksi lakini kwa sharti ziwe nzito na zenye kusitiri mahala pa lazima kuoshwa.
Haya ni madhehebu ya Al-Hasan, Ibn Al-Musayyib na Ahmad. Pia Mafuqahaa wa Hanafi, Shaafi'iy na Hanbali[2].


Ya tatu:

Inajuzu kupukusa kwa hali yoyote hata kama ni nyepesi.
Ni madhehebu ya Ibn Hazm na Ibn Taymiyah kama inavyojulikana. Kauli hii pia imekhitariwa na Ibn 'Uthaymiyn na Al-'Allaamah Ash-Shanqiytwiy[3], nayo ndiyo yenye nguvu.
Maulamaa wenye kauli mbili za mwisho wamejuzisha kupukusa juu ya soksi kwa kutoa dalili zifuatazo:

1- Ni Hadiyh ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah aliyesema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake.([4])

2- Imepokelewa toka kwa Al-Azraq bin Qays akisema: "Nilimwona Anas bin Maalik ametengukwa na wudhuu, akaosha uso wake, mikono yake miwili na akapukusa juu ya soksi zake za sufi. Nikamuuliza: Je, wapukusa juu yake? Akasema: Hakika hizi ni khufu mbili, lakini ni za sufi"([5]).
Anas Allaah Amridhie akaeleza hapa kuwa khufu si lazima iwe ni ya ngozi tu, bali ni zaidi ya hivyo, naye ni Swahaba anayeijua vyema lugha.

3- Ni kwamba waliosema kuhusu kupukusa juu ya soksi mbili ni Maswahaba 11. Kati yao ni 'Umar na mwanawe Abdullaah, 'Aliy, Ibn Mas'uud, Anas na wengineo. Na hakuna yeyote katika enzi yao aliyekwenda kinyume, na hilo likawa limekubaliwa na wote.

Kisha jamhuri ya Maulamaa ikaja kupiga marufuku kupukusa juu ya soksi nyepesi kwa vile hazisitiri mahala pa lazima kuoshwa. Tumekwisha eleza nyuma kuwa hili si sharti – kwa mujibu wa utafiti – kwa kuchukulia kipimo cha soksi iliyotoboka. Na kwa vile siku hizi zinazovaliwa zaidi ni soksi nyepesi kwa kiasi na kiuwiano, tutaona kwamba kushurutisha mfano wa masharti kama haya, kunakwenda kinyume na makusudio ya Mwekaji sheria ya ukunjufu kwa kuwabana watu na kuwatia uzito. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


FAIDA

Inaingia katika maana ya soksi bendeji, plasta na matambara anayofungwa mtu mguuni kwa udhuru, kwani hizo ni vigumu kuzifungua. Yeye atapaka tu juu yake kama alivyolikhitari hilo Shaykh wa Uislamu.
Na hukumu za kupukusa juu ya soksi mbili ni hukumu zile zile za kupukusa juu ya khufu mbili.


ANAPOVAA SOKSI JUU YA NYINGINE

Hili lina hali mbalimbali:

1- Akitawadha kisha akavaa soksi juu ya nyingine (mbili mbili), basi atapukusa soksi ya juu endapo kama atatengukwa na wudhuu.
Na haya ni madhehebu ya Hanafiy. Na ni kauli yenye nguvu kwa Maalik na Hanbali. Aidha ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy aliyetofautiana nao katika kauli mpya.([6])

2- Akitawadha akavaa soksi juu ya nyingine, kisha akapukusa juu yake, halafu akaivua ya juu baada ya kupukusa, basi inajuzu kwake kuukamilisha muda kwa kuzipukusa soksi za ndani, kwa vile inasadikika kuwa ameingiza miguu yake ikiwa twahara.

3- Akitawadha akavaa soksi, kisha akaivaa nyingine juu yake kabla ya kutengukwa na wudhuu, basi atapukusa juu ya soksi zozote azitakazo (za ndani au za nje).([7])

4- Akitawadha akaivaa soksi moja, akapukusa juu yake kisha akaivaa nyingine hali ya kuwa ana twahara, itajuzu kwake kupukusa ya juu, kwa vile inasadikika kuwa ameiingiza miguu yake ikiwa ni twahara([8]). Na kama alitengukwa na wudhuu kisha akaivaa nyingine, haitojuzu kwake kupukusa ya juu, bali itajuzu ya chini.


2- KUPAKA KWENYE VIATU

Imetangulia katika Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu'ubah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha, akapukusa juu ya soksi zake na viatu vyake([9]). Hadiyth hii tukisema kuwa ni Sahihi, inaweza kubeba mambo mawili:

1- Ni kuwa alivaa viatu juu ya soksi na akapukusa juu yake na hivyo hukmu yake kuwa ni moja kama ilivyotangulia katika kuvaa soksi juu ya soksi au khufu juu ya khufu.

2- Ni kuwa Al-Mughiyrah alimwona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa mara juu ya soksi na mara nyingine juu ya viatu. Na hii inakuwa ni dalili kuwa inajuzu kupukusa juu ya viatu ijapokuwa bila ya soksi. Na hili ingawa liko mbali kidogo, lakini linaweza kutolewa dalili juu ya kujuzu hilo kutokana na yaliyotangulia katika Hadiyth ya Abuu Dhwabyaan kwamba "Aliy bin Abi Twaalib alitawadha, akapukusa juu ya viatu vyake, kisha akaingia msikitini, akavua viatu vyake, kisha akaswali…" Na hapa hakutaja soksi.([10])
Na pengine kujuzu kupukusa juu ya viatu kunatilika nguvu vile vile kwa kutoshurutishwa kuwa chenye kupukuswa kiwe ni chenye kusitiri mahala pa lazima kuoshwa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
[1] Al-Mabsuutw" (1/102), "Al-Mudawwanah" (1/40), "Al-Ummu" (1/33) na "Al-Awsatw" (1/465).

[2] "Masaail Ahmad" ya Ibn Haani’i (1/21), "Al-Awsatw" (1/464), "Al-Majmu'u" (1/540) na "Fat-h Al-Qadiyr"(1/157).

[3] Al-Muhalla" (2/86), "Al-Masaail Al-Maardiyniyyah" (uk.58), "Majmuu Al-Fataawa" (21/184), "Al-Mumt'i"(1/190) na "Adhwaau Al-Bayaan" (2/18,19) ambayo ina utafiti murua kabisa.

[4] Al-Albaaniy amesema ni Swahiyh. Imetolewa na Abuu Daawuud (159), At-Tirmidhiy (99) na Ahmad (4/252), naye ndiye mzungumzaji. Angalia katika "Al-Irwaa "(101).

[5] Ahmad Shaakir amesema kuwa ni Swahiyh. Imetolewa na Ad-Duwlaabiy katika "Al-Kunaa" (1/181).

[6] "Haashiyat Ibn 'Aabidiyn" (1/179), "Jawaahir Al-Ikliyl" (1/24) na "Rawdhat At-Twaalibiyn" (1/127).
Mengi wameyazungumzia hapa kuhusu khufu, lakini hukumu ni moja.

[7] Mahanbali wamelielezea hili katika "Kash-Shaaf Al-Qina'a" (1/117-118).

[8] Imeelezwa katika "Kash-Shaaf Al-Qina'a (1/117-118) kwamba hapukusi. Amesema: "Kwa vile khufu iliyopukuswa ni badala ya kuosha ile iliyo chini yake. Na badali haijuzu kuwa na badali nyingine, bali atapukusa ya chini kwa vile ruhusa imefungamana nayo!!
Ninasema: "Katika hili, pana maangalizi, kwa vile suala lina kidhibiti kimoja, nacho ni kuingiza miguu yake ikiwa twahara. Na hili linapatikana ijapokuwa kwa kupukusa ya chini kabla ya kuvaa ya juu na kuruhusika kuswali kwa kufanya hivyo.

[9]  Imeelezewa nyuma kidogo.

[10] Imeelezewa nyuma kidogo.

0 Comments