038-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kupaka Juu Ya Kinachofunika Kichwa

TATU

KUPAKA JUU YA KINACHOFUNIKA KICHWA


1- KUPAKA JUU YA KILEMBA KATIKA WUDHUU

Inajuzu kupukusa juu ya kilemba – badala ya kupukusa kichwa – wakati wa kutawadha kwa hali yoyote. Na haya ni madhehebu ya Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Awzaa'iy, Ibn Hazm na Ibn Taymiyah. Nayo ni kauli ya Abu Bakr, 'Umar, Anas na Maswahaba wengineo (Radhiya Allaahu ‘anhum)([1]). Na bila shaka, hilo limethibiti toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Imepokelewa toka kwa 'Amri bin Umayyah Adh-Dhumariy akisema: "Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu mbili na kilemba"([2]).

Kauli kama hiyo hiyo imepokelewa toka kwa Al-Mughiyrah bin Shu'ubah([3]).
Na imepokelewa toka kwa Bilaal akisema: "Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akipukusa juu ya khufu mbili na khimaar"([4]). Khimaar hapa ni kinachofunika kichwa, na makusudio ni kilemba.

Haya ni katika wakati ambapo Abuu Haniyfah na wenziwe, Maalik na Ash-Shaafi'iy([5])wameelekea kwingine wakisema kuwa mwenye kutawadha hapukusi juu ya kilemba basi, bali hupukusa juu yake pamoja na utosi, na utosi unakuwa ni fardhi na kilemba ni Sunnah (ziada) kwa kujengea juu ya kujuzisha kwao kupaka sehemu tu ya kichwa!!

Lakini pamoja na hivyo, Ash-Shaafi'iy anasema: Ikiwa Hadiyth ya kupukusa juu ya kilemba ni Swahiyh, basi hiyo ndiyo kauli yangu. Na bila shaka yoyote Hadiyth hiyo ni Swahiyh, kwa hiyo ndiyo kauli yake.

Wenye kupinga kupukusa juu ya kilemba wametoa hoja kwa Hadiyth ya Jaabir bin Abdillaah aliyesema: "Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikivuta nyuma kilemba chake na akapukusa juu ya utosi wake"([6]). Sijaipata sanadi yoyote ya Hadiyth hii!!

Na kwa Hadiyth ya Al-Mughiyrah akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipukusa juu ya kilemba chake, na juu ya utosi na khufu zake mbili"([7]).

Ninasema: "Kauli yenye nguvu ni kuwa inajuzu kwa hali yoyote kupukusa juu ya kilemba kwa kuthibiti kuelezewa hilo toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa kufanywa hilo na Makhalifa wawili waliokuja baada yake, na kutokuwa na uzito hoja iliyotolewa na wenye kulipinga hilo([8]). Hii ni pamoja na kuwa ni bora kupukusa sehemu ya utosi pamoja na kilemba ili kuepuka mahitilafiano. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.2- KUPUKUSA MWANAMKE JUU YA USHUNGI/MTANDIO

Shaykh wa Uislam anasema: "Ikiwa mwanamke atahofia baridi au mfano wa baridi, atapukusa juu ya ushungi wake, kwani Ummu Salamah alikuwa akipukusa juu ya ushungi wake. Na inatakikana apukuse pamoja na hivi baadhi ya nywele zake. Na ikiwa hakuhitajia hilo, basi hapa kuna mvutano baina ya Maulamaa."([9])

Ninasema: "Katika riwaya([10]),  Hanafiy, Maalik, Ash-Shaafi'iy na Hanbali, wameelekea mwelekeo wa kusema kuwa haijuzu kutokana na yale yaliyopokelewa toka kwa 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba yeye aliingiza mkono wake chini ya ushungi wake na akapukusa kichwa chake, akasema: "Kwa hivi, ndivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoniamuru".([11])

Wamesema: "Na kwa vile hicho ni kivazi cha kichwani kwa mwanamke na hakuna uzito katika kukiondosha, haikujuzu kupukusa juu yake."

Al-Hasan Al-Baswriy amechukua msimamo wa kuwa inajuzu kupukusa juu ya ushungi. Hayo hayo wameyasema Mahanbal, - lakini wameshurutisha kuwa ni lazima mitandio au shungi ziwe zimezungushiwa chini ya koo!! – kwa kuchukulia kipimo cha kilemba, kwani khimaar kikawaida huvaliwa kichwani.

Ninasema: Ingelikuwa Hadiyth ya 'Aaishah ni Swahiyh, basi ingelimaliza mjadala katika kuzuia kupukusa juu ya ushungi Na kama si hivyo, basi kipimo kitachukuliwa juu ya kilemba. Na ili kuondosha wasiwasi, ni vyema mwanamke apukuse juu ya ushungi wake pamoja ncha ya utosi wake.3- KUPUKUSA JUU YA KOFIA KATIKA WUDHUU

Jamhuri ya Maulamaa imeshikilia mwelekeo wa kuwa haijuzu katika wudhuu kupukusa juu ya kofia badala ya kichwa, kwani fardhi ni kupukusa kichwa. Lakini hilo limeachiliwa katika kilemba kutokana na uzito wa kukivua kwa Jamhuri ya Maulamaa, au kwa matini ya Ahmad.

Ibn Hazm, Ibn Taymiyah([12]) na watafiti kati ya wadau wa taaluma hii, wameshikilia mwelekeo wa kujuzu kupukusa juu ya kofia. Hii ni kwa vile, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipopukusa juu ya kilemba, sisi tumejua kwa hilo kuwa si fardhi kugusanisha maji na kichwa, bali inajuzu kupukusa juu ya kitu chochote kilichovaliwa kichwani hata kama hakisitiri mahala pa lazima kuoshwa na wala haikuwa ni uzito kukivua. Na hili ndilo sawa, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.FAIDA

Si sharti kuwa na twahara wakati wa kuvaa chenye kufunika kichwa ili ijuzu kupukusa juu yake.

Hili halipimiwi na kupukusa juu ya khufu mbili, kwa vile hakuna sababu ya kuvikutanisha viwili hivyo, bali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameelezea ulazima wa twahara wakati wa kuvaa khufu mbili na wala hakulielezea hilo kwa upande wa kilemba na ushungi. Na lau kama ingelikuwa ni lazima, basi angelibainisha.([13])
Ninasema: Hii ni kwa vile, khufu mbili ni badala ya kilicho fardhi kukiosha. Ama kichwa, fardhi yake ni kupukusa, na kilicho juu ya kichwa, huchukua hukmu yake. Kwa hiyo vimekuwa ni vitu viwili tofauti. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


Hakuna wakati wala muda maalumu wa kupukusa juu ya chenye kufunika kichwa

Ni kwa kutofaa kipimo cha kupukusa juu ya khufu mbili. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipukusa juu ya kilemba na khimaar na wala hakulipangia hilo wakati. Na hili limepokelewa toka kwa 'Umar bin Al-Khattwaab Allah Amridhie([14]).NNE

KUPAKA JUU YA "AL JABIYRAH"

"Al Jabiyrah" ni majiti mawili ambayo huungiwa kwayo mifupa iliyovunjika ili ishikamane. Na katika maisha yetu ya leo, plasta ya jasi (piopi) hutumiwa badala yake.

Na mtu ambaye katika kiungo chake kimoja cha wudhuu kutakuwa na "jabiyrah" (piopi) kama mikono miwili au miguu miwili, basi inajuzu kwake kupukusa kwa mujibu wa rai ya Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo.([15]) Wao wametolea dalili yafuatayo:

1- Hadiyth ya Jaabir kwa yule aliyepatwa na mpasuko usoni, na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika inamtosheleza tu kufunga jeraha lake kwa kitambaa, kisha akapukusa juu yake)). Na hii ni Hadiyth Dhaifu.([16])

2- Ni kauli ya Ibn 'Umar: "Mwenye jeraha lililofungwa, atatawadha na atapukusa juu ya bendeji, na ataosha pembezoni mwa bendeji".([17])
Na hajulikani Swahaba yeyote aliyekwenda kinyume na Ibn 'Umar.

3- Ni kuchukulia kipimo cha kupukusa juu ya khufu mbili, kwani kupukusa juu ya khufu mbili kunajuzu bila ya dharura, basi vipi kwa upande wa "jabiyrah" (piopi) ambayo ni dharura. Hivyo inachukua uzito zaidi.

Na Ibn Hazm ameshikilia msimamo wa kuwa mwenye kufungwa "jabiyrah" (piopi), basi halazimiki kupukusa juu yake na kwamba hukumu ya mahali hapo inaondoka.([18])

Ninasema: "Hii ni kwa vile Ibn Hazm amezichukulia Hadiyth za kupukusa juu ya bendeji, plasta n.k kuwa ni Dhaifu na wala haoni Qiyaas kuwa ni hujjah!! Na Hadiyth hizi hazifai kama alivyosema. Ama Qiyaas, bila shaka itakuwa ni hujjah endapo kama nguzo na sharti zake zitakuwepo. Lakini inaweza kusemwa kuwa Qiyaas hapa hakifai kutokana na kutofautiana tanzu na asili. Ni Qiyaas waajib (kupukusa juu ya piopii kwa Jamhuri ya Maulamaa) juu ya mubaah (kupukusa juu ya khufu mbili). Na hapa basi, madhehebu ya Ibn Hazm yanang'aa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.FAIDA

1- Kupukusa juu ya "jabiyrah" (piopi) kunatosheleza, sawasawa katika wudhuu au katika kuoga, kwa vile "jabiyrah" (piopi) ni jambo lisilo na budi, na kwa hivyo hakuna tofauti ndani yake kati ya hadathi ndogo na hadathi kubwa. Ni kinyume na kupukusa juu ya khufu mbili, kwani hili limeruhusiwa (kwa atakaye).

2- Si lazima kufungwa "jabiyrah" wakati mtu ana twahara wala hakuna muda maalumu wa kupukusa juu yake.
Hii ni kwa vile, hilo linakwenda kinyume na makusudio ya sharia katika kuruhusu kupukusa kati ya kuondosha uzito na tabu. Aidha, kufungwa (piopi) ni hali ya kulazimika ambayo huja ghafla bila kutegemewa kinyume na khufu mbili. Mbali ya hivyo, hakuna matini au ijma’a.
Hivyo basi, hakuna muda maalumu wa kupukusa juu ya "al-Jabiyrah". Lakini wakati wowote atakapoliondosha au kiungo kikapona, basi haitojuzu kupukusa.

3- Bendeji na plasta za kitiba (hospitali) zilizofungwa katika kiungo cha wudhuu, zina hukumu ya "al-Jabiyrah" (piopi) kama lilivyohakikiwa hilo na Shaykh wa Uislamu.
 
([1]) "Masaail Abuu Daawuud" (8), "Al-Mughniy" (1/300), "Al-Majuu'u" (1/406), "Al-Awswat" (1/468), "Al-Muhalla" (2/58) na "Majmuu'u Al-Fataawiy" (21/184).
([2]) Hadiyth Swahiyh: Imetolewa na Al-Bukhaariy (205).
([3]) Hadiyth Swahiyh: Imetolewa na Muslim (275).
([4])  Hadiyth Swahiyh: Imetolewa na Muslim (285).
([5])  "Haashiyat Ibn 'Aabidiyn" (1/181), "Haashiyat Ad-Dusuuqiy" (1/164) na "Al-Majmu'u" (1/407).
([6]( Sikuipata na wala haipo katika kitabu chochote kati ya vitabu vya Hadiyth nilivyonavyo. Na Ibn Al-Mundhir ameitaja bila ya isnaad (1/469).
([7])  Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika mlango wa wudhuu.
([8]) Angalia hoja zao na zilivyojibiwa katika "Al-Muhalla" (2/61).
([9])"Majmuu'u Al-Fataawaa" (21/218).
([10])"Al-Mudawwanah" (1/42), "Al-Ummu" (1/26), "Al-Badaai'i" (1/5) na "Al-Mughniy" (1/305).
([11]) Sijapata kuiona bali ameitaja Al-Kaasaaniy katika "Al-Badaai'i" (1/5) na wala sijaiona katika kitabu chochote cha Hadiyth.
([12]) "Al-Muhalla" (2/58) na "Majmuu'u Al-Fataawaa" (21/ 184-187, 214).
([13]) "Al-Muhalla" (2/64).
([14])"Al-Muhalla" (2/65).
([15]) "Sharh Fat-h Al-Qadiyr" (1/140), "Al-Mudawwanah" (1/23), "Al-Mughniy"(1/203) na "Al-Majmuu'u" (2/327).
([16]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (236) na wengineo. Angalia "Al-Irwaa" (105).
([17]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Ibn Abi Shaybah (1/126) na Al-Bayhaqiy (1/228).
([18]) "Al-Muhalla" (2/74).

0 Comments