039-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (1)

KUOGA


Fasili yake:

Kilugha maana yake ni kuchuruzika maji juu ya kitu. Ama kisheria, ni kumiminisha maji yaliyo twahara katika mwili wote kwa njia maalumu.([1])


YENYE KUPASISHA KUOGA

1- Ni kutokwa na manii mtu akiwa macho au usingizini

Ni kwa neno Lake (Subhaanahu wa Ta’ala):

« وإن كنتم جنبا فاطهروا»

“Na mkiwa na janaba, basi ogeni” ([2])

Na  Lake (Subhaanahu wa Ta’ala):

« يا أ يها الذين لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلوا»

“Enyi mlioamini! Msikaribie Swalah hali mmelewa, mpaka muyajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge” ([3])

Na imepokelewa toka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy toka kwa Mtume  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

(( إنما الماء من الماء))

((Hakika maji ni kutokana na maji))([4])

Yaani kuoga (kwa maji) kunakuwa anapomwaga (maji) nayo ni manii.
Na Mtume ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alimwambia 'Aliy:

((إذا فضخت الماء فاغتسل))

((Ukiyabubujisha maji, basi oga))([5])

Na katika tamko jingine:
((إذا حذفت))

((Utakapokatia))

Na wala hayawi kwa sifa hii ila yanapotoka kwa matamanio kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

«خلق من ماء دافق»

Ameumbwa kutokana na maji yenye kuchupa([6])

Na imepokelewa toka kwa Ummu Salamah (Allaah Amridhie) akisema:
"Alikuja Ummu Sulaym, naye ni mke wa Abu Twalha, kwa Mtume wa Allaah ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akasema: Ewe Mtume wa Allaah! Hakika Allaah Haoni hayaa kwa haki. Je, inampasa mwanamke kuoga kama ameota? Mtume wa Allaah ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akasema:

((نعم، إذا رأت الماء))

((Naam, kama akiyaona maji))([7])

Kauli hii inafahamisha kuwa si lazima manii yatoke kwa matamanio na kuchupa wakati wa kuota ndipo ipase kuoga, bali itambidi kuoga anapoyaona manii katika nguo yake. Na kama hakuyaona, basi hapaswi kuoga hata kama atakumbuka kuwa aliota. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) aliyesema:
"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu anayekuta ubichi ubichi na wala hakumbuki kama aliota. Akasema:

((يغتسل))

((Ataoga))

Na kuhusu mtu anayeona kwamba yeye aliota lakini hakukuta ubichi bichi, akasema:

((لا غسل عليه))

((Hapaswi kuoga))([8])ZINDUSHI MBILI:

(a) Katika yote yaliyotangulia, mwanamke ni kama mwanamume, sawa kwa sawa.

(b) Yeyote mwenye kuchuruzikwa na manii bila ya matamanio kutokana na ugonjwa, au baridi au mfano wa hayo, basi hana lazima kuoga kwa mujibu wa kauli mbili zilizo sahihi zaidi za Maulamaa. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri kinyume na Ash-Shaafi'iy na Ibn Hazm.

Na Maulamaa([9]) kwa sauti moja wamesema kuwa ni lazima kuoga mtu anapotokwa na manii kwa matamanio wakati yu macho, na anapotokwa na manii akiota usingizini. Isipokuwa yale yaliyopokelewa toka kwa Ibraahiym An-Nakh'iy kwamba yeye alikuwa haoni kuwa inampasa mwanamke kuoga anapoota.


2- Kukutana tupu mbili ijapokuwa bila ya kumwaga manii

Kinapozama kichwa cha dhakari ya mwanamume katika utupu wa mwanamke, basi inawalazimu wote wawili kuoga sawasawa ikiwa wamemwaga manii au hawakumwaga. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyoipokea toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( إذا جلس بين شعبها الأربع، ثم جهدها فقد وجب الغسل)) (وإن لم ينزل))

((Anapokaa kati ya tanzu zake nne, kisha akamtoa jasho, basi ni lazima kuoga)) ((hata kama hakumwaga)) ([10])

Na imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayemwingilia mkewe kisha akaishiliwa nguvu, je, ni lazima waoge? – nailhali Mama wa Waumini 'Aaishah yuko hapo amekaa - Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

(( إني لأفعل ذلك أنا وهذه ثم نغتسل ))

((Hakika mimi nafanya hilo na huyu, kisha tunaoga))([11])

Amesema An-Nawawiy: "Na hili halina mvutano hivi leo. Lilikuwa na mvutano kwa baadhi ya Maswahaba na waliokuja baada yao. Kisha ikafungika ijmaa’ juu ya tuliyoyataja."

Ninasema: Ama hitilafu ya Maswahaba katika suala hili, miongoni mwake ni Hadiyth ya Zayd bin Khaalid ambapo yeye alimuuliza 'Uthmaan bin 'Affaan akimwambia: "Unasemaje endapo mtu atamwingilia mkewe na wala hakumwaga manii"? 'Uthmaan akamwambia: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalah na ataosha dhakari yake". Akasema 'Uthmaan: "Nimelisikia hilo toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nikaliulizia hilo kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr bin Al-'Awwaam, Twalha bin 'Ubayd Allaah na Ubay bin Ka'ab, nao wakamwamuru hilo".([12])

Daawuud Adh-Dhwaahiriy ameelekea msimamo wa kutolazimu kuoga kama mtu hakumwaga kwa Hadiyth:

((Hakika maji ni kutokana na maji)) ([13])

Na Hadiyth ya Abu Sa'iyd kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu fulani:

(( إذا أعجلت ـ أو قطحت – فعليك الوضوء))

((Ukikaukiwa, basi yakupasa kutawadha))([14])

Ama Maswahaba hawa, bila shaka imethibiti kutoka kwao kuwa waliachana na kauli ya kutokupasa kuoga.([15])

Ama kauli ya Daawuud, bila shaka imekwenda kinyume na jamhuri ya Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mafuqahaa wa Taabi'iyn na waliokuja baada yao. Hawa wanaona kwamba Hadiyth ya ((Maji ni kutokana na maji)) na yaliyo katika maana yake, ilikuwa ni mwanzoni mwa Uislamu kisha ikanasikhiwa.

At-Tirmidhiy amesema (1/185):
"Na hivi ndivyo alivyopokea zaidi ya mtu mmoja katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwemo Ubay bin Ka'ab([16]) na Raafi'i bin Khudayj. Na hili ndilo linalofanywa na Maulamaa wengi zaidi kuwa mtu anapomwingilia mkewe katika tupu, inawabidi wote wawili kuoga hata kama hajamwaga manii.


FAIDA([17])

1- Dhakari ya mwanamume ikigusa uchi wa mwanamke bila kuiingiza, basi haiwapasi kuoga kwa makubaliano ya Maulamaa([18]).
Ibraahiym An-Nakh'iy aliulizwa kuhusu mtu anayemwingilia mkewe sehemu isiyokuwa tupu (farji) kisha akamwaga. Alijibu akisema:
"Atakoga yeye, lakini mkewe hakogi bali ataosha ile sehemu iliyoguswa"([19]).

2- Mtu akimwingilia mkewe, akaingiza sehemu ndogo tu ya kichwa cha dhakari, kisha manii yake yakaingia katika utupu wa mkewe, na mkewe hakumwaga, basi haimpasi mke kuoga.
Amesema An-Nawawiy: "Anapoingiziwa mwanamke manii (si kwa dhakari) katika utupu wake wa mbele au wa nyuma kisha manii hayo yakamtoka, basi hapaswi kuoga. Hili ndilo sahihi lililopitishwa na jamhuri."([20])

3- Mtu anapomwingilia mkewe kisha mkewe huyu akakoga, halafu baadaye yakamtoka maji ya mumewe toka kwenye utupu wake, basi hapaswi kuoga tena. Lakini je, itamlazimu kutawadha?
Kwa mujibu wa kauli ya jamhuri([21]), itamlazimu kutawadha kwa vile maji hayo yametoka kupitia moja ya njia mbili ingawa ni twahara. Ibn Hazm([22]) amesema:
"Wudhuu utampasa kutokana na hadathi yake yeye na wala si kutokana na hadathi ya mwingine. Na kutoka maji ya mumewe toka kwenye utupu wake hakuzingatiwi kuwa yeye ndiye anayemwaga wala ni hadathi kutokana na yeye. Kwa hivyo, hakogi wala hatawadhi."

Ninasema: Ama kaida ya kutawadha kwa kila chenye kutoka katika moja ya njia mbili, kaida hii haikubaliki kama ilivyotangulia, kwani mapitio ya manii kwa mwanamke, siyo mapitio ya mkojo. Hivyo basi madhehebu ya Ibn Hazm yanakuwa na nguvu zaidi. Lakini pamoja na hivyo, pachukuliwe tahadhari kuwa manii haya yanaweza kuchanganyika na madhii ya mwanamke. Hivyo la akiba zaidi atawadhe, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

4- Mume anapomwingilia mkewe mdogo (hajaingia hedhini bado), au kijana mdogo ambaye hajabaleghe akamwingilia mwanamke, basi inamlazimu mwanamke kuoga vile vile kama alivyosema Imam Ahmad:
"Hebu nielezeni! Je, 'Aaishah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimwingilia, alikuwa hakogi?!([23])

5- Mume anapomwita mkewe kufanya mapenzi, basi haitakikani kumkatalia hilo kwa kisingizio cha kutokuwepo maji ya kukogea.
Shaykh wa Uislamu katika "Al-Fataawaa" 21/454" anasema:
"Haitakikani kwa mwanamke kumkatalia mumewe tendo la ndoa. Amwachie amwingilie. Na ikiwa ataweza kuoga, basi akoge, na kama hakuweza, atatayammamu na kuswali".

 
([1]) "Majmu'u Al Fataawaa" (1/185).
([2])  Surat Al-Maaidah :6
([3]) Surat An-Nisaai : 43
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (343) na Abuu Daawuud (214).
([5]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (206), An-Nasaaiy (193) na Ahmad (1/247). Na asili yake ni katika "Swahiyh Mbili".
([6])Surat At-Twaariq :6
([7])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (282) na Muslim (313).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na At-Tirmidhiy (113) na Abuu Daawuud (233).
([9]) "Al-Majmuu" (1/139), "Bidaayat Al-Mujtahid" (1/58) na "As-Sayl Al-Jarraar"(1/104).
([10])Hadiyth Sahihi: Imepokelewa na Al-Bukhaariy (291) na Muslim (348) na ziada ni yake yeye.
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (350).
([12])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (292) na Muslim (347).
([13])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (343). Imekwishatangulia.
([14]) Imetolewa na Al-Bukhaariy (180) na Muslim (345).
([15]) Angalia kauli pokezi kutoka kwao katika kitabu cha "Jaami Ahkaam An-Nisaa"cha Shaykh wetu Allaah Amhifadhi (1/89,90).
([16])Hadiyth ya Ubayya ni Sahihi kwa njia zake kama alivyoibainisha Shaykh wetu Abu 'Umayr Al-Athariy- Allah Amstareheshe katika maisha yake- katika "Shifaau Al'ayyi bitahqiyq musnad Ash-Shaafi'iy" (100).
([17])Zimetolewa toka kwenye kitabu changu cha "Fiqhi Assunnah Linnisaa" (uk 46).
([18]) "Al-Mughniy" cha Ibn Qudaamah (1/204).
([19]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na 'Abd Rrazzaaq (971). Angalia kauli pokezi mfano wake kutoka baadhi ya watangu wema katika  "Jaami Ahkaam An-Nisaa"(1/95).
([20]) "Al-Majmuu" (2/151). Tazama "Al-Muhalla" (2/7).
([21]) "Al-Majmuu" (2/151).
([22]) "Al-Muhalla" (2/6).
([23]) "Al-Mughniy" (1/206).

0 Comments