040-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (2)

3, 4 - HEDHI NA NIFASI

Mambo haya mawili ni sababu mbili zenye kuwajibisha kukoga. Na kwa vile kukoga kunatokana na sababu ambapo hakufanyiki ila baada ya kukatika kwake na kumalizana nayo, inabidi kukoga baada ya kukatika hedhi na nifasi.
Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alimwambia Faatwimah binti Abi Hubaysh:

((Ukiingia hedhini, basi acha kuswali, na ukiipa mgongo (ikikatika), basi oga na uswali)).([1])

Na nifasi ni kama hedhi kwa ijma’a. Kisha imethibiti toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiielezea nifasi kama hedhi na hedhi kama nifasi.
Hukumu za hedhi na nifasi zitakuja kwa uchambuzi inshaAllaah.


5- KAFIRI ANAPOSILIMU

Maulamaa wana kauli tatu kwa upande wa hukumu ya kuoga wakati kafiri anaposilimu:


KWANZA:

Ni lazima aoge kwa hali yoyote. Haya ni madhehebu ya Maalik, Ahmad, Abu Thawr na Ibn Hazm. Pia Ibn Al-Mundhir na Al-Khattaabiy([2]) wamelikhitari. Dalili zao ni:

1-      Hadiyth ya Qays bin ‘Aaswim aliyesema kwamba aliposilimu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alimwamuru akoge kwa maji na mkunazi. Na asili ya amri hii ni ulazima.

2-      Ni yale yaliyomo katika Hadiyth ya Abu Hurayrah katika kusilimu Thumaamah bin Uthaal kutokana na kauli ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):


((Nendeni naye hadi katika ukuta (bustani) wa Bani Fulani, kisha mwamrisheni kukoga)).([3])
3-      Kisa cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Kisa hiki kinaeleza kwamba Asyad aliwauliza Mus’ab bin ‘Umayr na As’ad bin Zuraarah: “Mnafanya vipi mkitaka kuingia katika dini hii?” Wakajibu: “Unaoga unatwaharika, halafu unazitwaharisha nguo zako mbili, kisha unashuhudia shahada ya haki, halafu unaswali…” Hadiyth.([4])


PILI:

Inapendeza (imesuniwa) kuoga, isipokuwa tu kama alikuwa na janaba kabla ya kusilimu, hapo italazimu akoge. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Abu Haniyfah.([5])


TATU:

Si lazima kukoga kwa hali yoyote. Ni madhehbu ya Abu Haniyfah.([6])
Hawa wametoa dalili zao katika haya yafuatayo:

1.     Neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

«Waambie waliokufuru, ikiwa wataacha (ukafiri), watasamehewa yaliyopita»([7])

2.     Hadiyth ya ‘Amru bin Al-‘Aasw ikiwa marfuu:

((Uislamu unapomosha yaliyopita))([8]).

Katika kutolea ushahidi wa Aayah na Hadiyth, kuna mlahadha. Ni kuwa yanayokusudiwa katika Aayah na Hadiyth ni kughufiriwa madhambi. Maulamaa wamekubaliana wote kuwa anayesilimu lau kama alikuwa na deni au kisasi, basi hayo hayapomoki kwa kusilimu kwake, na hasa kwa vile kuwa kulazimika kuoga si uchukulifu au ukalifisho kwa yaliyomlazimu katika ukafiri, bali ni ulazimisho wa sharti katika masharti ya Swalah katika Uislamu, kwani yeye ana janaba. Na Swalah haisihi mtu akiwa na janaba. Naye havuliki na janaba hiyo kwa kuwa ameingia katika Uislamu([9]).

3.     Wamesema:
Watu wengi walisilimu wakiwa na wake na watoto lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamrisha kuoga kwa njia ya lazima. Na lau ingelikuwa ni wajibu, basi angeliwaamrisha hilo.

Na hapa kuna mlahadha:
Lililo dhahiri ni wajibu kuoga, kwani kuamrishwa baadhi, kuna maana kuwa wao washafikishiwa amri. Ama kudai kuwa wengineo hawakuamrishwa, hilo halifai kwa kushikilia tu, kwani ukomo wake ni wao tu kutokuwa na habari nalo, nako si kutojua kwa sababu ya kutojulikana.([10])

Kwa hivyo, lenye nguvu zaidi ni kuwa inamlazimu kafiri – sawasawa akiwa kafiri wa asili au aliyeritadi – aoge kwa hali yoyote anaposilimu. Na linalotuhisisha kwamba kuoga wakati wa kuingia katika Uislamu lilikuwa ni jambo linalojulikana vizuri na Maswahaba, ni yale yaliyomo ndani ya kisa cha kusilimu mama wa Abu Hurayrah. Kisa kinaeleza kuwa mama huyo alioga na akavaa deraya yake.[11] Pia kisa kilichotangulia cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.([1]) Hadiyth Sahihi: Takhriyj yake itakuja katika mlango wa hedhi.
([2]) “Mawaahib Al-Jaliyl” (1/311), “Al-Mughniy” (1/152), “Al-Majmuu’i”, (2/175) na “Al-Muhalla” (2/4).
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (355), At-Tirmidhiy (605) na An-Nasaaiy (1/109). Na tazama “Al-Mishkaat” (543).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ahmad (2/304) na Ibn Khuzaymah (252). Na asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili, lakini hakuna amri ya kuoga. Angalia vilevile “Al-Irwaa” (128).
([5]) “Al-Majmuu” (1/174), “Al-Ummu” (1/38) na “Ibn ‘Aabidiyn” (1/167).
([6]) “Al-Mabsuutw” na “Sharh Fat-h Al-Qadiyr” (1/59).
([7]) Surat Al-Anfaal: 38
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (121) toka katika Hadiyth ya ‘Amru bin Al-‘Aasw.
([9]) “Al-Majmuu” (2/174).
([10]) “Nayl Al-Awtwaar” (1/281).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (2491) na Ahmad (7911).

0 Comments