041-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (3)


6- SWALAH YA IJUMAA

Kukoga siku ya Ijumaa ni jambo la lazima, na mwenye kuacha, basi anapata dhambi kwa mujibu wa kauli mbili sahihi zaidi za Maulamaa. Haya yamesemwa na Abuu Hurayrah, 'Ammaar bin Yaasir, Abuu Sa'iyd Al-Khudriy na Al-Hasan. Haya yamekuja pia katika riwaya iliyopokelewa toka kwa Maalik na Ahmad. Aidha, ni madhehebu ya Ibn Hazm.([1])
Dalili za hili ni:

1- Hadiyth ya Abuu Sa'iyd Al-Khudriy kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((غسل يوم الجمعة واجب على كل محتلم))
((Kukoga siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila mwenye kuota (aliyebaleghe))).([2])

2- Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((من جاء منكم إلى الجمعة فليغتسل))
((Anayekuja Ijumaa miongoni mwenu, basi aoge)).([3])

3- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((حق على كل مسلم أن يغتسل في كل سبعة أيام يوما، يغسل رأسه وجسده))
((Haki iliyo juu ya kila Mwislamu, ni kuoga siku moja katika kila siku saba. Aoshe kichwa chake na mwili wake)).([4])

4- Hadiyth ya Thawbaan kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((حق على كل مسلم السواك، وغسل يوم الجمعة، وأن يمس من طيب أهله إن كان))
((Haki iliyo juu ya kila Mwislamu ni mswaki, kuoga siku ya Ijumaa na aguse mafuta uzuri ya ahli wake kama yapo)).([5])

5- Hadiyth ya Hafswa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((على كل محتلم رواح الجمعة، وعلى من راح الجمعة أن يغتسل))
((Ni juu ya kila mwenye kuota (aliyebaleghe) kwenda Ijumaa, na ni juu ya anayekwenda Ijumaa, akoge)).([6])

6- Imepokelewa toka kwa Ibn 'Umar, amesema:
"Tuliamrishwa kukoga siku ya Ijumaa, na tusitawadhe kutokana na kujamii".([7])Wamesema:
Na kuyafanya kuwa si wajibu wala si haki kwa mfano wa dalili hizi zilizotajwa hapo juu hayoaliyoyaelezea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba ni haki ya Allaahu (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kila Mwislamu na kwamba ni wajibu kwa kila aliyeota (aliyebaleghe),basi hili ni jambo ambalo ngozi husisimka kwalo!!([8])
Nayo Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Ibn Mas'uud na Ibn 'Abbaas ambao ni katika Maswahaba, msimamo wao ni kuwa kukoga siku ya Ijumaa ni jambo mustahabbu na wala si lazima. Na kati ya dalili muhimu walizozitoa ni:

1- Hadiyth Marfuu ya Samurah bin Jundub:
((من توضأ يوم الجمعة فبها ونعمت، ومن اعتسل فالغسل أفضل))
((Mwenye kutawadha siku ya Ijumaa, basi hilo ni jambo zuri, na mwenye kukoga, basi kukoga ni jambo bora))([9]).
Haya ni maneno yaliyo wazi zaidi katika dalili yao ijapokuwa Hadiyth ni dhaifu kwa kauli yenye nguvu.

2- Hadiyth Marfuu ya Abuu Hurayrah:
((من توضأ فأحسن الوضوء ثم أتى الجمعة فاستمع وأنصت، غفر له ما بينه وبين الخمعة وزيادة ثلاثة أيام ...))
((Mwenye kutawadha, akatawadha ipasavyo, kisha akaja Ijumaa, akasikiliza na akanyamaza, hughufiriwa yaliyo baina yake na kati ya Ijumaa pamoja na nyongeza ya siku tatu...)).([10])

Wamesema:
Lau kama kuoga kwa ajili ya Ijumaa kungelikuwa ni lazima, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingelitaja wudhuu peke yake.

Al-Haafidh ameijibu kauli hii katika "Al-Fat-h" (2/422) kwa kusema:
"Hakuna ndani yake kukanusha kukoga, kwani Hadiyth imekuja kwa njia nyingine katika Asw-Swahiyh kwa tamko "Mwenye kukoga". Kwa hiyo inawezekana kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametaja wudhuu kwa yule ambaye alikwishaoga kabla ya kwenda, na akahitajia kutawadha tena".


Ninasema:
"Wao wana dalili nyinginezo nilizozitafiti kwa kina na kuzijadili moja baada ya nyingine katika Kitabu changu cha "اللمعة في آداب وأحكام الجمعة".

Na hitimisho la suala ni kuwa wenye kusema kwamba kukoga ni wajibu, dalili zao zina nguvu zaidi, sanadi zake ni sahihi zaidi na kuzitumia ni salama zaidi.


7- KUFA

Ni moja kati ya sababu zenye kuwajibisha kukoga, lakini si kwa maiti mwenyewe, bali ni kwa aliyemfikia kati ya Waislamu. Uchambuzi wake utakuja katika mlango wake wa "Kitaab Al-Janaaiz".
MAJOSHO YALIYO MUSTAHABBU (YA SUNNAH)

1- Kwa Ajili Ya ‘Iyd Mbili
Imepokelewa toka kwa Al-Faakih bin Sa'ad kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikoga wakati wa ‘Iyd Al-Fitwr na ‘Iyd Al-Adhw-ha.([11]) Lakini Hadiyth hii ni dhaifu.
Lakini inaweza kutolewa dalili juu ya kusuniwa hilo, kwani imethibiti toka kwa 'Aliy bin Abi Twaalib na Ibn 'Umar kuwa imepokelewa kwa Zaadhaan kuwa mtu mmoja alimuuliza ‘Aliy Allaah Amridhie kuhusu kuoga. Akamjibu akimwambia:
"Oga kila siku ukipenda". Akasema: "Hapana. Kuoga ambako ni kuoga". Akamwambia: "Siku ya Ijumaa, siku ya ‘Arafah, siku ya kuchinja na siku ya Fitwr".([12])
Na imepokelewa toka kwa Naafi'i kwamba ‘Abdullaah bin 'Umar alikuwa akikoga siku ya Fitwr kabla ya kwenda sehemu ya kuswalia([13]).


2- Kuzindukana Baada Ya Kupoteza Fahamu
Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioga kutokana na kupoteza fahamu.([14]) Na hii ilikuwa katika maradhi yake aliyofia.
Na ijmaa’ imenukuliwa juu ya kusuniwa hilo, na Maulamaa wamekufanya kuzindukana na wendawazimu kuwa sawa na kupoteza fahamu.


3- Kuhirimia Hijjah Na ‘Umrah
Ni kwa Hadiyth ya Zayd bin Thaabit kwamba yeye alimwona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebadili nguo kwa ajili ya kuhirimia na kisha akakoga.([15])
Na mwanamke hata kama atakuwa na hedhi au nifasi ataoga, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamrisha Asmaa bint 'Umays akoge wakati alipojifungua katika Hijjah.([16]) Haya yataelezwa zaidi katika mlango ha Hijjah.


4- Kuingia Makkah
Ni kwa Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba yeye alikuwa haingii Makkah ila hulala Dhiy Tuwaa mpaka asubuhi, halafu hukoga, kisha huingia Makkah mchana. Inaelezewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilifanya hilo.([17])


5- Baada Ya Kila Jimai Kama Atarudiarudia
Ni kwa Hadiyth ya Abu Raafi'i kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazungukia wakeze usiku mmoja huku akikoga kwa huyu na kwa yule. Nikasema: "Ewe Mtume wa Allaah! Kwa nini usikoge mara moja tu?”
Akasema:
(( هذا أزكى وأطيب وأطهر ))
((Hili ni utakaso zaidi, jema zaidi na twahara zaidi)).([18])


6- Baada Ya Kumwosha Maiti (Kama Hadiyth Itakuwa Sahihi)
Imepokelewa Hadiyth Marfu’u toka kwa Ab Hurayrah:
(( من غسل ميتا فليغتسل ))
((Mwenye kumwosha maiti, basi akoge)).([19])


7- Kwa Mwenye Damu Ya Istihaadha Kwa Kila Swalah
Amri ya kukoga kwa mwanamke mwenye damu ya istihaadha wakati wa kila Swalah imekuja katika mjumuiko wa Hadiyth dhaifu.([20])
Lakini imethibiti kuwa Ummu Habiybah alipatwa na damu ya istihaadha kwa muda wa miaka saba. Akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wasallam) kuhusu hilo. Mtume ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) akamwamrisha akoge akimwambia:
(Huu ni mshipa)

Na kwa hivyo, akawa anakoga wakati wa kila Swalah([21])

Ash-Shaafi'iy Allaah Amrehemu anasema: "Bila shaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamrisha akoge na aswali([22]), na hakuna ndani yake kuwa alimwamrisha kukoga kila Swalah. Nami sina shaka yoyote – InshaAllaah – kuwa kuoga kwake kulikuwa ni kwa kupenda yeye mwenyewe kinyume na alivyoamrishwa, na hilo halina mipaka kwa bibi huyo"([23]).


Ninasema:
"Na hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa Salaf na Khalaf kuwa mwenye damu ya istihaadha si lazima kwake kukoga kila Swalah".
([1])  "Al-Muhalla" (2/12) na "Al-Awsatw" (4/43).
([2])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (879) na Muslim (846).
([3])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (2/6) na Muslim (844).
([4])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (2/318) na Muslim (849).
([5])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ahmad (4/34). Tazama "Asw-Swahiyhah" (1796).
([6])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (338), An-Nasaaiy (3/89) na Ahmad (3/65).
([7])  Isnadi yake ni hasan: Imetolewa na Abuu Bakr Al-Muruuziy katika "Ijumaa na fadhila zake".
([8])  Mfano wake katika "Al-Muhalla".
([9])  Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (354), An-Nasaaiy (3/94), At-Tirmidhiy (497) na wengineo. Hadiyth hii ina njia ambazo nimezitafiti kwa kina na kuzizungumzia katika "Allam'at Fiy Aadaab Wa Ahkaam Al-Jum'ah". Al-'Allaamah Al-Albaaniy amesema ni Hasan.
([10]) Isnadi yake ni Sahihi: Imetolewa na Muslim (857), At-Tirmidhiy (498) na wengineo.
([11])  Hadiyth Dhaifu sana: Imetolewa na Ibn Maajah (1316).
([12])  Isnadi yake ni Sahihi: Imetolewa na Ash-Shaafi'iy katika "Musnadi yake" (114) na kwa njia yake Al-Bayhaqiy 3/278).
([13])  Isnadi yake ni Sahihi: Imetolewa na Maalik (426), na kutoka kwake imepokelewa na Ash-Shaafi'iy katika"Al-Ummu" (1/231).
([14])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (687) na Muslim (418) katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa toka kwa 'Aaishah Allaah Amridhie.
([15])  Hadiyth Hasan: Imetolewa na At-Tirmidhiy (831). Na tazama "Al-Irwaa" (149).
([16])  Hadiyth Sahihi: Itakuja katika mlango wa Hijjah.
([17])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1573) na Muslim (1259).
([18])  Hadiyth Hasan: Imetolewa na Abuu Daawuud (216) na Ibn Maajah (560).
([19]) Imetolewa na Abuu Daawuud (3162), At-Tirmidhiy (993) na Ibn Maajah (1461). At-Tirmidhiy, Ibn Hajar na Al-Albaaniy wamesema ni Hasan. Tazama "Al-Irwaa" (1/174). Lakini inavyoelekea ni kuwa inahitaji aina fulani ya ufuatilio, kwani Hadiyth imetiwa kasoro.
([20]) Irejee katika "Jaami'i Ahkaam An-Nisaa" (1/230-237).
([21])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (327) na Muslim (334).
([22]) Amri hii ya kukoga ni mutwlaq, na kwa hivyo haionyeshi kukariri. Na huenda yeye alifahamu kutakiwa kufanya hivyo kwa kielelezo (alama) fulani. Na kwa ajili hii, alikuwa akikoga kila Swalah (Fat-h Al-Baariy (1/509).
([23]) "Sunan Al-Bayhaqiy" (1/349).

0 Comments