042-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (4) Niyyah, Nguzo Na Yaliyosuniwa

NIYAH NI SHARTI YA KUSIHI KUKOGA

Hii ni kwa vile kukoga ni ibada isiyojulikana ila kupitia Shar’iah, na kwa ajili hiyo, niyah imekuwa ni sharti humo. Na niyah ni moyo kuazimia tendo la kukoga ikiwa ni kufuata na kuitii Amri ya Allaahu (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaahu (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

» « وما أمروا إلا ليعبدوا الله مخلصين له الدين
»Na hawakuamrishwa ila kwa ajili ya kumwabudu Allaah wakimtakasia Yeye Dini«([1])

Maana ya ikhlaasi ni kuwa na niyah ya kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumkusudia Yeye tu kwa kutekeleza mambo ambayo Ameyafaradhisha kwa Waja Wake Waumini.

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((إنما الأعمال بالنيات))
((Hakika ‘amali ni kwa niyah)).([2])
Na hili ni ‘amali.([3])


NGUZO YA KUOGA

Ni kukieneza kiwiliwili chote kwa maji. Na uhakika wa kukoga ni kububujisha maji kwenye kiwiliwili chote na kufika maji hayo katika kila unywele na ugozi. Na hili limethibiti katika Hadiyth zote zinazoelezea kuhusu picha ya namna alivyokuwa akikoga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – Hadiyth hizi nitazielezea hivi karibuni –. Na kati ya Hadiyth hizo ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie):

((..kisha anamimina maji juu ya kiwiliwili chake chote)).([4])

Al-Haafidh amesema katika “Al-Fat-h” (1/361):
“Usisitizo huu unaonyesha kwamba yeye alieneza kiwiliwili chake chote kwa josho.”

Na katika Hadiyth ya Jubayr bin Mutw-am (Allaah Amridhie) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))
((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote)).([5])

Hadiyth hii inaonyesha kuwa kueneza kiwiliwili kwa maji ni faradhi ya kukoga na wala si vinginevyo.

Na Hadiyth ya Mama wa Waumini Ummu Salamah (Allaah Amridhie) aliyesema:
“Nilisema: Ewe Mtume wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayesuka sana nywele, je, nizifumue wakati wa kukoga janaba?” Akasema:

(( لا، إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات، ثم تفيضين عليك الماء فتطهرين))
((Hapana, bali yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu, kisha utajimiminia maji utwaharike)).([6])

Ama kusugua viungo, kusukutua na kupaliza maji wakati wa kukoga, kauli yenye nguvu inasema kuwa hayo yote ni Sunnah kama itakavyokuja. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri.


YALIYOSUNIWA WAKATI WA KUOGA

Mhimili katika mlango huu ni Hadiyth mbili:
1- Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikoga janaba:
“Alianza, akaiosha mikono yake miwili, kisha anatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya kuswali, kisha huingiza vidole vyake katika maji, kisha hufikicha kwavyo mizizi ya nywele zake, halafu humimina [Na katika riwaya nyingine: mpaka anapodhani kwamba amekwishatotesha ngozi yake, humimina] juu ya kichwa chake mateko matatu kwa mikono yake, kisha humimina maji juu ya ngozi yake yote”.([7]) 

2- Hadiyth ya Mama wa Waumini Maymuunah (Allaah Amridhie) Alisema:
“Nilimtengea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maji ya kukoga, akaosha mikono yake mara mbili au tatu, kisha akajimiminia maji upande wake wa kushoto kwa kutumia mkono wake wa kulia, kisha akaosha utupu wake [Na katika riwaya nyingine: utupu wake pamoja na uchafu ulioipata], kisha alisugua mkono wake kwenye udongo au ukutani [kisha akauosha], kisha alisukutua na kupaliza, akauosha uso wake, mikono yake miwili na kichwa chake, kisha alijimiminia maji juu ya kiwiliwili chake, kisha alisimama kando, akaosha makanyagio yake mawili, nikampa kitambaa, kisha akaambatisha mkono wake hivi na wala hakukitaka”.([8])


Ninasema:
Kutokana na Hadiyth hizi mbili na nyinginezo, tunahitimisha tukisema kuwa, linalopendeza ni kuwa kuoga janaba kunatakikana kuwe katika picha ifuatayo:

1- Ni kuosha mikono miwili mara tatu kabla ya kuiingiza katika chombo au kuanza kukoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah (Allaah Amridhie):
((Alianza, akaiosha mikono yake miwili….)).
Na katika tamko la Muslim (317) kwa Hadiyth ya Maymuuna (Allaah Amridhie):
((Akaosha viganja vyake viwili mara mbili au mara tatu, kisha akaingiza mkono wake katika chombo…)).
Al-Haafidh amesema katika “Al-Fat-h” (1/429):
“Inawezekana kuwa aliviosha kwa ajili ya kuvisafisha uchafu. Pia yawezekana kuwa huo ni mwosho wa kisheria wakati wa kuamka usingizini.”

2- Kuosha utupu na uchafu ulioipata kwa mkono wa kushoto kutokana na maelezo ya Hadiyth ya Maymuunah. Ama kuukamata utupu kwa mkono wa kulia, hilo ni makruhu kutokana na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((إذا بال أحدكم فلا يأخذن ذكره بيمينه، ولا يستنجى بيمينه، ولا يتنفس في الإناء))
((Anapokojoa mmoja wenu, basi asiikamate kabisa dhakari yake kwa mkono wake wa kulia, wala asistanji kwa mkono wake wa kulia, na wala asipumulie ndani ya chombo)).([9])

3- Kuuosha mkono - baada ya kuosha utupu – na kuutakasa kwa sabuni au mfano wake kama mchanga. Maymuuna (Allaah Amridhie) katika Hadiyth yake anasema:
((Kisha akaambatisha mkono wake ardhini akaupangusa kwa udongo, kisha akuosha….)).
Na katika tamko jingine:
((Kisha akapiga ardhi kwa mkono wake wa kushoto, akausugua msuguo wa nguvu)).([10])

An-Nawawiy katika “Sharh Muslim” (3/231) anasema:
“Ni kwamba inapendeza kwa anayestanji kwa maji anapomaliza, aoshe mkono wake kwa udongo (mchanga) au “ashnaan” (mada mfano wa sabuni)   au ausugulie na mchanga au ukuta ili usafike kutokana na uchafu”.

4- Kutawadha wudhuu kamili kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalah. Na hili limethibiti katika Hadiyth za ‘Aaishah na Maymuuna (Allaah Awaridhie).

Al-Haafidh katika “Al-Fat-h” (1/429) anasema:
“Inawezekana kuwa kuanza kutawadha kabla ya kukoga, ni Sunnah ya kando, pale ambapo ni lazima kuviosha viungo vya wudhuu pamoja na kiwiliwili chote wakati wa kukoga. Na inawezekana kuwa badala ya kuviosha tena wakati wa kukoga, itatosheleza kuoshwa kwake wakati wa kutawadha. Na bila shaka ametanguliza kuosha viungo vya wudhuu kwa ajili ya kuvipa hadhi yake, na ili mwenye kukoga apate picha ya twahara zote mbili; kubwa na ndogo”.

Ninasema:
Kutawadha kabla ya kukoga ni Sunnah kwa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Thawr, Daawuud na Adh-Dhwaahiriy.([11])


 
([1]) Surat Al-Bayyinah.
([2]) Hadiyth Sahihi: Imekwishatajwa.
([3]) Angalia mlango wa ((Niyah ni sharti ya kuswihi wudhuu uk.40)).
([4]) Hadiyth Sahihi: Matini na takhriyj yake zitakuja karibu.
([5]) Hadiyth Sahihi: Ahmad ameitoa kwa tamko hili (4/81), na katika Al-Bukhaariy (254) na Muslim (327) kwa ufupisho.
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (330), Abuu Daawuud (251), An-Nasaaiy (1/131), At-Tirmidhiy (105) na Ibn Maajah (603).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (248) na Muslim (316).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (266) na Muslim (317).
([9]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (154) na Muslmi (267).
([10]) Hii ni kauli ya Muslim (317).
([11]) “Fat-h Al-Baariy” (1/426), “Al-Majmuu” (1/186) na “Al-Istidhkaar” (3/59).

0 Comments