043-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (5) Kuosha Miguu, Kuzifikicha Ndevu Na Kusugua Viungo Vyote

FAIDA MBILI:

Faida Ya Kwanza

Hukumu Ya Kusukutua Na Kupaliza Maji Puani Wakati Wa Kuoga

Katika mlango wa wudhuu, ilikwishatangulia kwamba Maulamaa wamehitilafiana katika kauli nne kuhusu kusukutua na kupaliza maji puani wakati wa kutawadha. Nasi tulitilia nguvu huko kwamba ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani.

Ama kuoga, Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake pamoja na Ahmad, ‘Atwaa na Ibn Al-Mubaarak ambao madhehebu yao ni mashuhuri, msimamo wao ni kuwa kusukutua na kupaliza maji puani ni lazima wakati wa kuoga janaba.([1]) Na kati ya dalili zao ni:


1- Hadiyth iliyopokelewa Marfuu:

((المضمضة والإستنشاق ثلاثا للجنب فريضة))

((Kusukutua na kupaliza maji puani mara tatu, lakini kwa mwenye janaba ni fardhi)).([2])


2- Hadiyth iliyopokelewa Marfuu:

((من ترك موضع شعرة من جسده لم يغسلها فعل به كذا وكذا من النار))

((Mwenye kuacha sehemu ya unywele katika kiwiliwili chake hakuuosha, atafanywa hivi na hivi motoni)).([3])


3- Hadiyth iliyopokelewa Marfuu:

((أداء الأمانة غسل الجنابة، وتحت كل شعرة جنابة))

((Kutekeleza amana ni kuoga janaba, na chini ya kila unywele janaba)).([4])

Hadiyth zote hizi ni dhaifu na wala hazifai kutolea hoja.

4- Ni kitendo chake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kilichopokewa katika Hadiyth ya Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) [kwa kiashirio wazi], na katika Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) [iliyojumuisha wudhuu]. Basi haya yanabainisha Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)):

« وإن كنتم جنبا فاطهروا»

«Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni»([5])


5- Ni kwamba kuosha kiwiliwili chote ni wajibu, na uso ni sehemu ya kiwiliwili. Na kwa hivyo, imekuwa ni lazima kusukutua na kupaliza maji puani, kwani mawili haya ni sehemu ya uso kama tulivyosema katika mlango wa wudhuu.

Ama waliosema kuwa hilo ni Sunnah, nao ni Maalik, Al-Layth na Al-Awzaa’iy ambao ni Jamhuri, dalili zao ni:

1- Kutawadha wakati wa kuoga si wajibu [kama ilivyotangulia], na kusukutua na kupaliza maji puani ni katika mambo yanayoambatana na wudhuu. Na kama wudhuu haupo, basi yanayoambatana nayo pia hupomoka.([6])

2- Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuyafanya mawili hayo, hakuonyeshi kuwa ni wajibu kwa kuwa tu amefanya, bali ni kwa “nadb” na “istihbaab”. Na haionyeshi wajibu ila ikiwa ni ubainisho wa mjumuiko uliofungamana na wajibu. Na hapa mambo si hivyo.([7])

3- Ni kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Abuu Dharri wakati alipomwuuliza kuhusu janaba iliyompata na wala hakupata maji:

(( الصعيد الطيب وضوء المسلم، وإن لم يجد الماء عشر حجج، فإذا وجد الماء فليمسه بشرته))

((Mchanga twahara ni kitwaharisho kwa Mwislamu ijapokuwa hakupata maji kwa miaka kumi. Na akiyapata maji, basi yaiguse ngozi yake)).([8])
Wamesema: “Al-Basharah” ni ngozi ya nje, na kwa hivyo haihusiani na kusukutua na kupaliza maji.


4- Hadiyth ya Jubayr bin Mutw’am (Radhiya Allaahu ‘anhu). Amesema: “Tulitajiana kuoga janaba mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema:

((أما أنا، فآخذ ملء كفي ثلاثا فأصب على رأسي، ثم أفيض بعد ذلك على سائر جسدي))

 ((Ama mimi, huchukua ujazo wa kiganja changu mara tatu, kisha namimina juu ya kichwa changu, kisha nabubujisha baada ya hapo juu ya kiwiliwili changu chote))([9])

Na katika tamko:

((أما أنا فأحثي على رأسي ثلاث حثيات من ماء فإذا أنا قد طهرت))

((Ama mimi, basi humwagia mateko matatu ya maji juu ya kichwa, na hapo nakuwa nimetwaharika)).([10])
Na tamko hili halifai.


5- Ni neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha):

((إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات من ماء، ثم تفيضين عليك الماء، فإذا أنت قد طهرت))

((Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)).


Ninasema:
“Lau si Hadiyth ya mwisho ya Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha), basi wajibu wa kusukutua na kupaliza maji puani ungelikuwa na sauti ya nguvu. Lakini Hadiyth ya Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha), inaonyesha kwa kielelezo cha nguvu kwamba kiasi kitoshelezacho katika kuoga ni kile kilichotajwa, na hakukutajwa humo kusukutua wala kupaliza maji. Na wala haisemwi: “Mawili hayo yanaingia katika neno lake (kisha unajimiminia maji), kwani maana ya kumimina, haiyagusi mawili haya kama inavyoonekana wazi.
Hivyo basi, madhehebu ya Jamhuri inayosema kuwa kusukutua na kupaliza ni jambo mustahabb na wala si wajibu wakati wa kuoga, ndiyo yenye nguvu kwangu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.”Faida Ya Pili

Ni Wakati Gani Wa Kuosha Miguu Miwili?

Lililo wazi kutokana na Hadiyth ya Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichelewesha kuosha makanyagio yake mawili mpaka pale alipomaliza kuoga.
Al-Bukhaariy katika tamko lake anasema:
“Alipomaliza kuoga, aliosha miguu yake”.
Ama Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), hakuna kingine humo zaidi ya kuwa tu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitawadha kabla ya kuoga([11]). Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wamekuwa na mielekeo minne kutokana na Hadiyth hizi mbili:([12])

1- Ni mustahabbu (jambo linalopendeza) kuchelewesha kuosha miguu miwili wakati wa kuoga kutokana na Hadiyth ya Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha). Haya ni madhehebu ya Jamhuri.

2- Ni kutawadha wudhuu kamili kabla ya kuoga kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Sababu ni kuwa Hadiyth hii inaelezea alivyokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya aghalabu kinyume na Hadiyth ya Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye ameelezea josho moja tu. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Maalik na Ahmad.

3- Mtu anahiarishwa, ima kuanza kuosha miguu miwili pamoja na wudhuu au kuiosha mwishoni. Hii ni riwaya ya Ahmad.

4- Kama mtu anaoga sehemu isiyo safi, basi ataiosha miguu yake mwishoni. Na kama si hivyo, basi ataiosha mwanzoni wakati akitawadha. Haya ni madhehebu ya Maalik.


Ninasema:
Mwelekeo huu wa mwisho ndio wenye nguvu zaidi. Lakini pamoja na yote hayo, jambo hili lina wasaa na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
                                            ____________________

5- Kumimina maji juu ya kichwa mara tatu mpaka yafike katika mashina ya nywele.

6- Kuanza upande wa kulia wa kichwa kisha upande wa kushoto.  

7- Kufikicha (kusugua) nywele
Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) inasema:
((Kisha hufikicha nywele zake kwa mkono wake mpaka anapohakikisha kuwa ameilowesha ngozi yake, hapo humiminia juu yake maji mara tatu...)).

Imepokelewa vile vile toka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikoga janaba, hutaka aletewe kitu kama “alhilaab”,([13]) huikamata kwa kiganja chake, kisha huanza kwa upande wake wa kulia wa kichwa, kisha upande wake wa kushoto….)).([14])

Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) vile vile akisema: ((Mmoja wetu alipokuwa akipatwa na janaba, huchukua kwa mkono wake mateko matatu juu ya kichwa chake, kisha huchukua maji kwa mkono wake juu ya upande wake wa kulia na kwa mkono wake mwingine juu ya upande wake wa kushoto.([15])


FAIDA

Je, Ndevu Huasuliwa Wakati Wa Kuoga Janaba?

Jamhuri ya Maulamaa ambao ni Maalik, Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ibn Hazm ([16])wamesema: “Haimlazimu kuziasulia (kuzifikicha), bali ni jambo mustahabbu.


Ninasema:
Hili mahala pake ni pale yanapokuwa maji yanafika hadi kwenye ngozi, na kama si hivyo, basi ni lazima kuziasulia ili kuyafikisha maji ndani yake. Na la akiba zaidi kwa vyovyote, ni kuziasulia ndevu zake kutokana na ujumuishi wa neno la ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): ((basi huasulia kwayo mashina ya nywele zake)).

8, 9- Kumimina na kuyaeneza maji katika kiwiliwili chote kwa kuanzia upande wa kulia kisha wa kushoto.
Kumimina na kueneza maji katika kiwiliwili kizima ni jambo lililothibiti katika Hadiyth zote zinazotoa picha ya josho lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ama kuanzia kulia, ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
((Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa kunampendeza kuanza kwa kulia akivaa viatu, akitembea, akijitwaharisha na katika mambo yake yote)).([17])


FAIDA MBILI

Faida Ya Kwanza

Kujimiminia Maji Kiwiliwili Chote Kunakuwa Ni Mara Moja Tu.

Na hili liko wazi katika muktadha wa Hadiyth mbili za ‘Aaishah na Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha). Ndani ya Hadiyth hizi, pametajwa kuoshwa mara tatu mikono miwili na kichwa. Ama kiwiliwili kizima, ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anasema:
((Kisha anamiminia juu ya kiwiliwili chake chote)).

Na Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) anasema:
((Kisha alimiminia juu ya kiwiliwili chake)).

Na Ibn Batwaal amesema:([18])
“Na kwa vile suala halikufungiwa kwa idadi, basi lichukuliwe chini ya ilivyotajwa, nayo ni mara moja, kwani asli ni kutozidisha juu yake”.


Ninasema:
Na hili ni mashuhuri katika madhehebu ya Ahmad na masahibu wa Maalik. Shaykh wa Uislamu amelikhitari hili. Na Jamhuri wamestahabbu kufanya mara tatu.


Faida Ya Pili

Hukumu Ya Kusugua Viungo Vya Kuoga([19])
Maulamaa wamekhitalifiana:
Je, ni sharti kupitisha mkono katika kiwiliwili kizima wakati wa kuoga? Au yatosha kumimina maji tu katika kiwiliwili chote hata kama mtu hakupitisha mkono wake katika kiwiliwili chake?

Au kwa maana nyingine tunasema: Je, kuoga kunatimu kwa kujimiminia maji tu au ni lazima pia kusugua juu ya kitu?

Jamhuri ya Maulamaa – kinyume na Maalik na Al-Muzaniy – wanaona kuwa hakuna ulazima kusugua, bali ni mustahabbu. Na lau kama mtu atajimwagia maji mwenyewe katika kiwiliwili chake, basi atakuwa ametekeleza aliyowajibishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Hali kadhalika, akipiga mbizi majini na maji yakaupata mwili wake wote.

Dalili za makundi mawili katika suala hili ni zile zile zilizokwishatangulia kuelezewa katika hukumu ya kusukutua na kupaliza maji puani.

Na lililo wazi ni kuwa kusugua ni jambo mustahabbu na wala si wajibu.

Na Hadiyth ya ‘Imraan ibn Haswiyn – pamoja na Hadiyth ya Ummu Salamah inayatilia nguvu madhehebu haya katika kisa cha “Al-Muzaadatayn”. Humo panaelezwa: ((… na mwisho wa hilo ulikuwa ni kumpa chombo chenye maji yule ambaye imempata janaba, akasema: Nenda, halafu ujimiminie”.([20])

Na kwa haya, lau akisimama mtu chini ya bafu la manyunyu (bomba/mfereji wa kuogea) na maji yakafika katika kiwiliwili chake chote, basi kuoga kwake ni sahihi kukiambatana na niyah.
([1]) Angalia marejeo ya mas-ala katika “Nguzo za Wudhuu”.
([2]) Hadiyth Mawdhuu’i (ya kutungwa): Ameitoa Ad-Daar Qutwniy (1/115). Pia imepokelewa Mursal. Tazama kitabu cha “Naswb Ar-Raayat” (1/87).
([3]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (249), Ibn Maajah (599) na Ahmad (1/94). Angalia “Adh-Dhwa’iyfah” (930).
([4]) Hadiyth Dhaifu: Ameitoa Ibn Maajah (598) kwa sanadi dhaifu. Tazama “At-Talkhiysw” (1/142).
([5]) Surat Al-Maaidah : 6
([6]) “Fat-h Al-Baariy” (1/443).
([7]) “Fat-h Al-Baariy” (1/432).
([8]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na At-Tirmidhiy (124), Abuu Daawuud (233), An-Nasaaiy (1/171) na wengineo kwa njia tofauti. Yenye nguvu zaidi ni ya Abuu Qulaabah toka kwa ‘Amr bin Bijdaan toka kwa Abuu Dharri ikiwa Marfuu kama ilivyo katika “Al-‘Ilal” ya Ad-Daara Qutwniy (1113) na Ibn Abii Haatim (1/11) na ‘Amr ambaye hajulikani. Hadiyth hii ina ushahidi toka kwa Abuu Hurayrah na pana mvutano wa yeye kuifanya Hasan. Lakini katika “Al-Irwaa”, Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi.
([9]) Hadiyth Sahihi: Imeelezewa karibuni.
([10]) Ash-Shawkaaniy amenukulu toka kwa Al-Haafidh kauli yake: “Neno lake (Basi hapo ninakuwa nishatwaharika), halina asili yoyote sawasawa katika Hadiyth Sahihi au Hadiyth Dhaifu.
([11]) Katika riwaya ya Muslim (316) kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), mwishoni mwa Hadiyth hii anasema: “..kisha akamimina juu ya kiwiliwili chake chote, kisha aliosha miguu yake miwili”. Ni ziada ambayo haikuhifadhiwa. Tazama “Ilal Muslim” ya Hiraawiy (69), “At-Tamhiyd” (22/93) na “Fat-h Al-Baariy” ya Ibn Rajab (1/234).
([12]) “Fat-h Al-Baariy” ya Ibn Hajar (1/362), “Al-Mughniy” (1/288), “Sharh Al-‘Umdah” (1/371) na “Al-Khilaafiyaat” cha Al-Bayhaqiy (2/425).
([13]) Ni chombo kinachoenea mkamuo mmoja wa maziwa ya ngamia (Maalim As-Sunan) cha Al-Khatwaabiy (1/69).
([14]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (258) na Muslim (318).
([15]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (277).
([16]) “Al-Muhalla” (2/33), “Al-Awswat” (2/127) na “At-Tamhiyd” (22/95).
([17]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (168) na Muslim (268).
([18]) “Fat-h Al-Baariy” (1/439).
([19]) “Al-Muhalla” (2/30), “Al-Istidhkaar” (3/63), “Al-Mughniy” (1/290), “Bidaayat Al-Mujtahid” (1/55) na “As-Sayl Al-Jarraar” (1/113).
([20]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (344).

0 Comments