044-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (6) Kuoga Mwanamke Janaba, Hedhi Na Nifaas, Na Kukausha Viungo Baada Ya Kuoga

KUOGA MWANAMKE JANABA

Anavyooga mwanamke janaba ni sawa na anavyooga mwanamume. Na mwanamke kama amesuka nywele zake, basi haimlazimu kuzifumua bali atalazimika tu kuhakikisha kuwa maji yanafika hadi kwenye mizizi ya nywele. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Maymuuna aliyesema:

“Ewe Mtume wa Allaah! Mimi ni mwanamke ninayependa sana kusuka nywele zangu. Je, nizifumue kwa ajili ya kuoga janaba?”
Mtume akamwambia:

(( لا، إنما يكفيك أن تحثي على رأسك ثلاث حثيات ثم تفيضين عليك الماء، فتطهرين))
((Hapana. Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji, kisha utajimiminia maji, na hapo unakuwa umetwaharika)). ([1])

Na imepokelewa na ‘Aaishah aliyesema:
“Tulikuwa tukioga tukiwa na “adh-dhimaad”([2]) nailhali tuko na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sawasawa tukiwa tumehirimia au hatujahirimia”.([3])

Na ‘Aaishah alimkosoa na kumlaumu ‘Abdulaah bin ‘Amr alipowaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga.([4])KUOGA MWANAMKE HEDHI NA NIFASI ([5])

Namna ya kuoga hedhi na nifasi ni sawa na kuoga janaba. Lakini pamoja na hivyo, wakati wa kuoga hedhi na nifasi huongezewa yafuatayo:


1- Atumie sabuni na mfano wake kama mada za kusafishia pamoja na maji.

Hii ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyeeleza kwamba Asmaa alimwuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kuoga hedhi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((تأخذ إحداكن ماءها وسدرتها فتطهر، فتحسن الطهور، ثم تصب على رأسها فتدلكه دلكا شديدا حتى تبلغ شئون رأسها، ثم تصب عليها الماء، ثم تأخذ فرصة ممسكة فتطهر بها))
((Mmoja wenu atachukua maji na mkunazi wake ajitwaharishe. Ajitwaharishe vizuri na kikamilifu, kisha ajimiminie maji kichwani mwake na akisugue kichwa msuguo wa nguvu mpaka afikilie mashina ya kichwa chake. Kisha atamwagia juu yake maji, kisha atachukua kitambaa kilichotiwa miski ajitwaharishe nacho)).
Asmaa akasema: “Ni vipi anajitwaharisha nacho?!”
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

((سبحان الله تطهرين بها))
((Subhaana Allaah! Unajitwaharisha nacho)).

‘Aaishah akasema kana kwamba hataki hilo lisikike: “Utafuatisha kwacho athari ya damu”.([6]  


2- Afumue nywele ili maji yafike hadi ndani ya mashina yake.

Ni kutokana na neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia:
((فتدلكه دلكا شديدا حتى تبلغ شئون رأسها ...))
((akisugue kichwa msuguo wa nguvu…))

Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa haitoshi tu kujimwagia maji kama ilivyo katika josho la janaba, na hasahasa pakizingatiwa kuwa katika Hadiyth yenyewe Asmaa alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kuoga janaba naye akasema:

((ثم تصب على رأسها فتدلكه حتى تبلغ شئون رأسها))
((kisha ajimiminie maji kichwani mwake na akisugue mpaka afikilie katika mashina ya kichwa chake ))

Na hapa hakutaja kusugua kwa nguvu, na kwa hivyo, akapambanua kati ya josho la janaba na josho la hedhi.

Maulamaa wametofautiana kuhusu hukumu ya kufumua nywele wakati wa kuoga hedhi.
Madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Maalik na Abuu Haniyfah yanasema kuwa jambo hilo ni mustahabbu na wala si wajibu.([7]) Hoja yao ni:

1- Kuwa Hadiyth haielezei waziwazi kuhusu wajibu wa kufumua nywele zilizosukwa.

2- Hadiyth ya ‘Aaishah iliyopo katika kisa cha hijja ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Anaelezea akisema:
“Basi ikanikuta siku ya ‘Arafah nami niko hedhini. Nikashtakia kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema:

(( دعي عمرتك وانقضي رأسك وامتشطي وأهلي بالحج))
((Acha ‘Umrah yako, fumua nywele zako uzichane uhirimie hijja))([8])

Maulamaa hawa wanasema kuwa josho hili ni la ihraam na wala si josho la hedhi. Kwa hivyo, Hadiyth hii haiwezi kuwa ni dalili.

3- Ama Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia wakati yuko hedhini:

((انقضي شعرك واغتسلي))
((Fumua nywele zako na uoge))([9])

Maulamaa hawa wanasema: “Hadiyth hii inarejeshwa katika Hadiyth iliyotangulia, kwani ni Hadiyth moja. Na kwa hivyo, wameongeza tamshi la ((na uoge )) na wakalichanganya juu ya josho la ihraam.

4- Ni ‘Aaishah kumlaumu na kumkosoa ‘Abdullaah bin ‘Amri alipowaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga.

Ama Imaam Ahmad, Al-Hasan na Twaawuus, madhehebu yao yanasema kuwa ni lazima mwanamke afumue nywele wakati anapooga hedhi na nifasi kutokana na Hadiyth zilizotangulia. Suala hili limehakikiwa na Mwanachuoni Arifu na Mweledi Ibn Al-Qayyim – Allaah Amrehemu([10])– na amekujibu kupinga kwa Jamhuri kwa haya yafuatayo:

1- Ama kauli yao kuhusu Hadiyth ya ‘Aaishah katika hijja yake, ni sahihi kuwa kweli alikuwa katika ihraam. Lakini hata hivyo, josho la hedhi ni katika majosho yaliyopewa uzito zaidi, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamrisha katika josho hilo mambo mengineyo ambayo hakuamrisha katika majosho mengineyo kama kujitwaharisha zaidi na kuingia kwa kina zaidi. Hivyo basi akamwamuru azifumue nywele kwa ajili ya kutanabahisha juu ya wajibu wa kuzifumua ikiwa kuzifumua huko kutaondosha hadathi hiyo kwa njia ya ufanisi zaidi.

2- Ama Hadiyth yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia wakati akiwa na hedhi:

 ((((انقضى شعرك واغتسلي
((Fumua nywele zako na ukoge))
basi kuwa kwake si Hadiyth ya hijja, ni jambo linalowezekana sana na hasahasa pakizingatiwa kuwa wapokezi wa Hadiyth ni kati ya waliopokea Hadiyth nyingi.  

3- Ama ‘Aaishah kumlaumu na kumkosoa ‘Abdullaah bin ‘Amri, hilo bila shaka lilikuwa pale alipowaamrisha wanawake kufumua nywele wakati wa kuoga janaba. Alisema:
“Ajabu gani hii ya Ibn ‘Amri?! Anawakataza wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga! Kwa nini basi asiwaamuru kunyoa vichwa vyao?! Hakika nilikuwa naoga mimi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika chombo kimoja…”([11]).

Bila shaka alikuwa akioga pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) janaba ambayo wote wawili walikuwa nayo lakini si hedhi!!
Na juu ya msingi huu, ni lazima mwanamke afumue nywele zake na hasahasa wakati akioga hedhi na nifasi. Na hili ndilo la akiba zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


3-Afuatishie athari za damu kwa kipande cha kitambaa chenye miski na mfano wake.

Ni jambo linalopendeza kwa mwanamke kutumia kipande cha kitambaa au pamba yenye miski kidogo. Atakiingiza kipande hicho ndani ya utupu wake baada ya kuoga. Vile vile, atatia manukato sehemu zote za mwili zilizopatwa na damu. Hayo yote ni kwa ajili ya kuondosha harufu mbaya toka sehemu husika. Haya yamethibiti katika Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia.
Mwanamke anaruhusiwa kuyafanya haya hata kama yuko katika kipindi cha eda ya mumewe au maombolezo ya mtu wake anayemhusu aliyefariki. Haya ni kutokana na Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyya akizungumzia anayokatazwa mwenye kukaa eda:
((… Wala hatujitii manukato, wala hatuvai nguo za rangi rangi ila nguo ya rangi moja tu. Tulipewa ruhsa wakati wa kujitwaharisha anapooga mmoja wetu hedhi, achukue kidogo katika manukato…))([12])

KUKAUSHA (KUFUTA) VIUNGO BAADA YA KUOGA

Maymuuna katika Hadiyth yake iliyotangulia inayozungumzia namna alivyokuwa akioga Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((Nikampa nguo (na katika riwaya nyingine: handikachifu), naye hakuichukua ilhali anakung’uta mikono yake))([13]).

Kwa Hadiyth hii, pametolewa dalili kuwa ni karaha kukausha viungo baada ya kuoga. Lakini dalili hii haina hoja kutokana na mambo yafuatayo([14]):

1- Ni tukio la hali ambayo inaguswa na uwezekaniko. Inajuzu ikawa kuwa hakupokea kitambaa hicho kwa jambo jingine lisilohusiana na ukaraha wa kufuta viungo bali kwa linalohusiana na kitambaa chenyewe, au pengine mwenyewe alikuwa na haraka au jinginelo.

2- Katika Hadiyth hiyo, kuna dalili kuwa yalikuwa ni mazoea ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujifuta. Na kama si hivyo, basi Maymuuna asingelimletea handikachifu.

3- Kukung’uta maji kwa mkono wake kunaonyesha kuwa si karaha kukausha viungo, kwani yote mawili yanazingatiwa kuwa ni kuondosha maji.

Kwa kumalizia tunasema:
“Hakuna ubaya wowote wa kukausha viungo baada ya kuoga, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.


 
([1]) Hadiyth Sahihi: Imeshatajwa mara nyingi nyuma.
([2]) Ni dawa kama gundi ya kupaka kwenye nywele na kuzifanya zikamatane na zitulie na kuwa kama rasta.
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (254) na Al-Bayhaqiy (2/182).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (331), An-Nasaaiy (1/203) na Ibn Maajah (604).
([5]) Ni kutoka kitabu changu cha “Fiqh As-Sunnah lin-Nisaai” (uk. 49) na “Jaami’i Ahkaam An-Nisaai” cha Shaykh wetu (1/116 na ya baada yake) pamoja na nyongeza kidogo.
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (314) na Muslim (332) na tamko ni lake.
([7]) “Al-Mughniy” (1/227), “Al-Muhalla” (2/38), “Nayl Al-Awtwaar” (1/311) na“Tahdhiyb As-Sunan” (1/293).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (317) na Muslim (1211).
([9]) Isnaad yake ni Sahihi: Imetolewa na Ibn Maajah (641). Tazama pia “Al-Irwaa”(1/167).
([10]) “Tahdhiyb As-Sunan” (1/293 na yanayofuatia) kwa msaada wa Allaah Mwenye kuabudiwa.
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (331), An-Nasaaiy (1/203) na Ibn Maajah (604).
([12]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (313).
([13]) Hadiyth Sahihi: Imekwishatajwa sehemu nyingi.
([14]) “Al-Fath” (1/432). Tizama pia katika “Al-Majmuu” (1/459).

0 Comments