045-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (7) Masuala Yanayohusiana Na Kuoga

MASUALA YANAYOHUSIANA NA KUOGA


-         Si Lazima Kutawadha Baada Ya Kuoga

Aliyeoga josho la kishari’ah na akataka kuswali, basi si lazima atawadhe hata kama alikuwa hajatawadha wakati akioga, kwani twaharisho la janaba linaondosha vile vile twaharisho la hadathi ndogo (kutokuwa na wudhuu). Hii ni kwa vile vizuizi vya janaba ni vingi zaidi kuliko vizuizi vya hadathi ndogo. Hivyo basi, kidogo humezwa na kingi.

Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
((Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa hatawadhi baada ya kuoga janaba)).([1])

Na katika riwaya nyingine:
((Anaoga na anaswali rakaa mbili, na wala simwoni akifanya wudhuu baada ya kuoga)).([2])

Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
“Kama hukugusa utupu wako baada ya kumaliza kuoga, basi ni wudhuu gani ulio kamili zaidi ya kuoga”.([3])

Ninasema:
Juu ya haya, inachepukia nukta kwamba si lazima kwa mwenye kuoga janaba kunuia kuondosha hadathi ndogo. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri na Ibn Taymiyah([4]).
Ama Mahanbali, wao wanaona kwamba akinuia twahara mbili, basi zote mbili zitamtosheleza. Lakini akinuia kuoga janaba tu, basi hana ila hilo alilolinuia tu([5]).


- Yakikusanyika Mawili Yenye Kuwajibisha Kuoga Kama Hedhi Na Janaba, Au Janaba Na Ijumaa

Hapa josho moja tu litamtosheleza yote mawili kama atayanuia yote mawili. Hii ni kauli ya Mafuqahaa wengi([6]).


- Mwanamke Akiwa Na Janaba Kisha Akaingia Hedhini Kabla Hajaoga

Kauli sahihi zaidi ya Maulamaa ni kuwa haimlazimu kuoga janaba, bali itamlazimu aoge janaba na hedhi kwa pamoja na ayanuie yote mawili wakati damu ya hedhi inapokatika. Haya ni madhehebu ya Ahmad([7])  
Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba itamlazimu kuoga janaba, kisha hedhi inapokatika, ataoga josho la hedhi. Haya ni madhehebu ya ‘Atwaa, An-Nakh’iy na Al-Hasan.
Baadhi wengine wamesema kuwa itamlazimu aoshe utupu wake, kisha damu inapokatika, aoge.
Kauli zote hizi mbili hazina dalili yoyote, na lililo sahihi na sawa ni kauli ya kwanza.
Na hili halipingi kuwa akitaka kuoga janaba au kuuosha utupu wake, kisha aoge damu inapokatika, basi atafanya hivyo na hakuna kosa lolote kwake, lakini si lazima.


- Inajuzu Kwa Mwanamume Kuogea Maji Yaliyosalia Ya Mkewe

Hili limekwishahaririwa katika mlango wa (Hukumu za Maji)


- Inajuzu Mume Kuoga Pamoja Na Mkewe 

Inajuzu wote wawili kuangaliana tupu zao bila ya ukaraha wowote. Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
((Nilikuwa naoga mimi na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika chombo kimoja [naye ananiwahi nami namwambia: niachie mimi niachie] wote tukiwa na janaba))([8])


-         Haijuzu Kuoga Uchi Hadharani

Kama akijisitiri watu wasimwone, basi hakuna ubaya. Tumekwishaitaja Hadiyth ya Mama wa Waumini Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
((Nilimwekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maji ya kuoga [na pazia yake] akaosha mikono yake miwili…..)).
Na imethibiti toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Muusa (‘Alayhis Salaam) alioga uchi([9]), hali kadhalika Ayyuub (‘Alayhis Salaam)([10]). Lakini hili ni faraghani.


- Anayepatwa Na Hadathi Wakati Wa Kuoga

Mwenye janaba akipatwa na hadathi kabla ya kumaliza kuoga, basi atakamilisha wala hatoanza upya, kwani hadathi haitengui josho, hivyo basi kuwepo kwake hakuathiri josho bali ni juu yake kutawadha.

Na hii ni kauli ya Maulamaa wengi akiwemo ‘Atwaa na Ath-Thawry. Ibn Qudaamah na Ibn Al-Mundhir wamelikubali hilo(11).([1]) Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy (107), An-Nasaaiy (1/137) na Ibn Maajah (579).
(00[2]) Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na Abuu Daawuud (250) na Ahmad (6/119).
([3]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Abdur-Razaaq katika “Al-Muswannaf” (1039).
([4]) “Al-Mabswuut” (1/44), “Ash-Sharh As-Swaghiyr” (1/65), “Al- Ummu” (1/36), “Majmuu Al-Fataawa”(21/397) na “Al-Muhalla” (2/44).
([5]) “Al-‘Uddat Sharh Al-‘Umdah” (uk.48).
([6]) “Al-Mughniy” (1/292) bali imenukuliwa Ijmaa’ juu yake katika ((Rahmat Al-Umma fi Khtilaafi Al-Aimmah)) (uk 51). Na Ijmaa’ hii imetenguliwa kinyume na Ibn Hazm katika “Al-Muhalla” (uk.42-47). Mwanachuoni Arifu na Mweledi Al-Albaaniy amekubaliana naye katika “Tamaam Al-Minnah” (uk 126).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321).
(9) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (278) na Muslim (339).
(10) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (279).
(11) “Al-Mughniy” (1/290) na “Al-Awswat” (2/112).

0 Comments