046-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (8) Masuala Yanayohusiana Na Mwenye Janaba

MASUALA YANAYOHUSIANA NA MWENYE JANABA

- Inajuzu Kwa Mwenye Janaba Kuchelewesha Kuoga

Si lazima kwake kuoga mara tu baada ya kupata janaba ingawa kufanya haraka inakuwa ni bora zaidi na utakasifu zaidi.
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana naye katika njia moja ya Madiynah akiwa na janaba, naye akamhepa asimwone. Kisha alikwenda akaoga. Baadaye alikuja na Mtume akamwuuliza:

((أين كنت يا أبا هريرة؟))
((Ulikuwa wapi ewe Abuu Hurayrah?))

Akajibu: “Nilikuwa na janaba, nikaona uzito kukaa nawe nikiwa sina twahara”. Akasema:

((سبحان الله، إن المسلم لا بنجس))
((SubhaanaAllaah. Hakika Muislamu hanajisiki))(
[1]
).

Na imepokelewa na Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwazungukia wakeze usiku mmoja na ilhali wakati huo anao tisa(
[2]
).

Kisha kuharakisha kuoga janaba, bila shaka kwa ngazi ya kwanza kabisa kunakuwa ni kwa ajili ya Swalah. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa mara nyingine akilala kabla ya kuoga kama tutakavyoona baadaye.


Inajuzu Kwa Mwenye Janaba Kulala Kabla Ya Kuoga, Kama Atatawadha

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
((Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kulala hali ya kuwa ana janaba, huosha utupu wake na hutawadha wudhuu wa Swalah))(
[3]
).

Na ‘Abdullaah bin Qays alimwuuliza akimwambia: “Ni vipi alikuwa akifanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na janaba? Je, alikuwa akioga kabla ya kulala, au akilala kabla ya kuoga?” Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akamjibu:
((Yote hayo alikuwa akiyafanya. Huenda akaoga kisha hulala, na wakati mwingine hutawadha kisha hulala)).

Akasema ‘Abdullaah bin Qays: “Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyefanya wasaa katika jambo”(
[4]
).

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Umar bin Al-Khattwaab alipomwuuliza kuhusu janaba inayompata usiku:

((توضأ، واغسل ذكرك، ثم نم))
((Tawadha, uoshe utupu wako, kisha lala)).(
[5]
)


- Hakuna Ubaya Kwa Mwenye Janaba Kusoma Qur-aan Na Kugusa Msahafu

Haya yamekwishaelezewa katika mlango wa Wudhuu. Basi rejea huko.

  


(
[1]
) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (283) na Muslim (371).
(
[2]
) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (284) na Muslim (309).
(
[3]
) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (288) na Muslim (305).
(
[4]
) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (307).
(
[5]
) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (290) na Muslim (306).

0 Comments