047-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (9)

Je, inajuzu kwa mwenye hedhi na mwenye janaba kuingia msikitini na kukaa humo?

Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo – kinyume na Adh-Dhwaahiriyyah – wanasema kuwa ni haramu kwa mwenye hedhi, mwenye nifasi na mwenye janaba kukaa Msikitini. Hayo yamepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas'uud .([1])

Wenye kupinga hili wametoa dalili zifuatazo:

1-    Ni neno Lake Allaah (Subhaanahuu wa Ta’ala):

((يا أيها الذين آمنوا لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلو))ا

((Enyi mlioamini! Msikaribie Swalah hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge)). ([2])

Wanasema kuwa makusudio ya Swalah hapa ni sehemu za kuswalia, nazo ni Misikiti. Na katika Aayah, mwenye janaba anazuiliwa kuingia humo isipokuwa tu kama ni msafiri. Kisha wakawaweka mwenye hedhi na mwenye nifasi katika kipimo kimoja na mwenye janaba!!


Wenye kujuzisha hili wamewajibu wakisema:

Hii ni moja kati ya taawili mbili za masalaf katika Aayah hii. Na taawili nyingine ni kuwa makusudio ni Swalah yenyewe, na si Msikiti. Kwa hivyo basi, maana inakuwa:
Na wala msikaribie Swalah mkiwa na janaba ila baada ya kuoga, isipokuwa kama mko safarini, basi hapo, swalini kwa kutayamamu. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema baada ya hapo:

((و,إن كنتم مرضى أو على سفر....فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini………na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi)).

Kisha kuna mlahadha katika kipimo cha mwenye hedhi kwa mwenye janaba, kwani mwenye hedhi ana udhuru na hawezi kuoga kabla ya kutwaharika damu, na wala hawezi kuiondosha hedhi yake kinyume na mwenye janaba ambaye anaweza kuoga.

2- Ni Hadiyth ya Jisrah binti Dujaajah toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إنى لا أحل المسجد لحائض ولا جنب))

((Hakika mimi sihalalishi Msikiti kwa mwenye hedhi wala kwa mwenye janaba)).([3])


Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hadiyth hii ni dhaifu, haifai kutolea hoja, kwani Hadiyth imezungukia kwa Jisrah, naye hawezi kuwa amepokea Hadiyth peke yake.

3- Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyya kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuwatoa vijizee vikongwe, waliotawishwa na wenye hedhi katika Swalah ya ‘Iyd ili washuhudie kheri na du’aa ya Waislamu, na wenye hedhi hukaa kando na sehemu ya kuswalia.([4]) 
Wamesema: Na ikiwa hali ni hii kwa upande wa sehemu za kuswalia, basi Misikiti ni awla zaidi kuzuiwa.


Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Makusudio ya “Al-Muswalla” katika Hadiyth ni Swalah, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wake walikuwa wakiswali ‘Iyd uwanjani na si Msikitini, na ardhi yote ni twahara, na haijuzu kuzuiliwa huko kuihusu baadhi ya Misikiti tu bila ya mingine.
Kisha imepokelewa Hadiyth hiyo hiyo kwa tamko:

((فأما الحيض فيعتزلن الصلاة))

((Ama wenye hedhi, hao hukaa mbali na Swalah)).

Na Hadiyth hii iko katika Swahiyh Muslim na kwingineko.

4- Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akielemeza kichwa chake kwangu nailhali yuko jirani na Msikiti, nami namweka sawa nikiwa hedhini.”
Wamesema: Akajizuilia kumweka sawa Msikitini kwa vile yeye ana hedhi.


Wenye kujuzisha wamejibu wakisema:

Hili walilolitolea dalili haliko wazi. Inawezekana kuwa hakuingia kutokana na sababu nyingine isiyokuwa hedhi kama kuwepo wanaume Msikitini na kadhalika.([1]) “Al-Majmuu” (2/184) na baada yake, “Al-Mughniy” (1/145) na “Al-Lubaab Sharh Al-Kitaab” (1/43). Ash-Shaafi’iy na Ahmad wamejuzisha kupita Msikitini bila kukaa, na “Al-Muhalla” (2/184) na baada yake.
([2]) Surat An-Nisaa: 43.
([3]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (232), Al-Bayhaqiy (2/442), Ibn Khuzaymat (2/284). Tazama “Al-Irwaa” (193).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (324) na Muslim (890).

0 Comments