048-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuoga (10)

Kisha wenye kujuzisha kuingia mwenye janaba na hedhi Msikitini wametoa dalili zifuatazo:

1- Ni utwaharifu wa asilia, pale ambapo hakuna cha sahihi chenye kukataza, kwani asili ni kuruhusika. Na bila shaka imeruhusiwa kwa Muislamu kuswali mahala  popote inapomkuta Swalah.

2- Imethibiti kwamba washirikina waliingia Msikitini na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafungia humo wakati ambapo Allaah Mtukufu Anasema:

« إنما المشركون نجس فلا يقربوا المسجد الحرام بعد عامهم هذا»

» Hakika washirikina ni najisi, kwa hivyo wasiukurubie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu«([1])

Ama Muislamu, kwa hali yoyote yeye ni twahara kutokana na neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam):

 ((إن المسلم لا ينجس))

((Hakika Muislamu hawi najisi)).([2])

Basi vipi Muislamu akatazwe kuingia na kafiri aruhusiwe?!


Wenye kupinga hili wamejibu wakisema:

Kwamba shari’ah imefarikisha kati ya Muislamu na kafiri na kwa hivyo ikasimama dalili juu ya kuharamisha kukaa mwenye janaba na hedhi!! Na imethibiti kufungiwa makafiri humo. Na kama shari’ah imepambanua, basi haijuzu kuwafanya sawa. Na hiki ni kipimo chenye kuambatana na matini, nacho hakifai!!
Ninasema: Hii ikiwa imethibiti matini kama isivyofichikana!!

3- Ni Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) isemayo:
“Hakika kijakazi mweusi alikuwa katika kitongoji cha Waarabu, kisha wakamwachilia huru. Halafu alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasilimu, akapatiwa chumba ndani ya Msikiti.”([3])
Wamesema: “Mwanamke huyu alikaa ndani ya Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na ilivyozoeleka kwa wanawake ni kuingia hedhini, lakini hata hivyo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumzuia na wala hakumwamrisha kujitenga na Msikiti wakati wa hedhi yake.


Wenye kukataza wamejibu:

Inavyoonekana ni kuwa mwanamke huyu hakuwa na watu wake wala makazi isipokuwa Msikiti, hivyo akalazimika kuishi Msikitini. Na kwa ajili hiyo, mwanamke mwengine hawezi kufanyiwa kipimo kwake. Na hili ni tukio la hali maalumu, na dalili ya wazi hailipingi katika kuzuia!!

4- Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusu mwanamke aliyekuwa akifagia Msikiti. Alipofariki, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuulizia.([4])
Mwanamke huyu hakulazimika kufagia Msikiti wakati wote na wala Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumzuia kujitenga na Msikiti wakati wa hedhi.

5- Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusu kulala kwa Ahlus Swafah ndani ya Msikiti wakati wa enzi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).([5])


Wenye kupinga wamejibu:

Kwamba Ahlus Swafah hawakuwa na jamaa wala mali kama inavyoonekana katika matini ya Hadiyth.

6- Imethibiti katika Hadiyth Sahihi kuwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akilala Msikitini nailhali ni kijana kapera asiye na jamaa zake.([6]) Na kijana huota mara nyingi, na wala hakukatazwa kukaa Msikitini wakati wa janaba.


Wenye kupinga wamejibu:

Haikuelezwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alilijua hili kwa Ibn ‘Umar na akamkubalia!!


Wenye kujuzisha wamejibu:

Lingefichikana hili kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), basi halifichikani kwa Allaah Mtukufu. Hivyo ilitakikana wahyi umtaarifu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili amkataze Ibn ‘Umar.


Hili limejibiwa:

Si lazima wahyi uteremke ili kumjulisha kila kosa linalofanywa na Swahaba. Ni makosa mengi waliyoyafanya Maswahaba kwa kutojua kwao dalili iliyokuja katika suala fulani katika enzi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

7- Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipopata hedhi wakati wa Hijja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamruhusu kufanya yote anayoyafanya mwenye kuhiji isipokuwa kutufu Al-Ka’bah([7]), hilo limeonyesha kuwa inajuzu kwake kuingia Msikitini, kwani mwenye kuhiji inambidi hilo.


Wenye kupinga wamejibu:

Bila shaka ametaka kumfundisha kwamba inajuzu kwa mwenye hedhi kufanya ‘amali zote za Hijja isipokuwa kutufu tu. Ama hukumu ya kuingia kwake Msikitini, bila shaka Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anajua kwamba hilo limekatazwa, kwani yeye ndiye mpokezi wa Hadiyth. Kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) hakumkataza kuswali ilhali ana hedhi – nailhali wenye kuhiji wanaswali - , basi je, tunaweza kusema kuwa ni lazima aswali na huku ana hedhi?!!


Ninasema:

“Jibu hili lina mwelekeo mzuri lakini kama itathibiti Hadiyth ya kukataza. Na Hadiyth hii ni dhaifu”.

8- Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) aliniambia:

ناوليني الخمرة من المسجد

((Nipatie jamvi toka msikitini))
Nikamwambia: Nina hedhi. Akasema:
إن حيضتك ليست في يدك
((Hedhi yako haiko katika mkono wako)).([8])

Na hili linaonyesha kuwa jamvi lilikuwa Msikitini naye akasisitiza Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aingie humo ili ampatie.


Wenye kupinga wamejibu:

Hadiyth imekuja kwa tamko jingine lisemalo:
((Wakati ambapo Mtume wa Allaah alikuwa Msikitini alisema: “Ewe ‘Aaishah! Nipatie nguo”. Akasema: “Nina hedhi”. Akasema: ‘Hedhi yako haiko katika mkono wako”([9]).
Na hii ni wazi kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa Msikitini wakati ‘Aaishah alikua nje pamoja na jamvi.  Hapo akamwamuru aingize mkono wake na si yeye kuingia.


Ninasema:

“Hadiyth hii inabeba uwezekano huu na ule. Kwa hiyo inatakikana kuipomosha kutokana na dalili za makundi mawili.

9- Athar ya ‘Atwaa bin Yasaar aliyesema: “Niliwaona wanaume katika Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) wakikaa Msikitini nailhali wana janaba wanapotawadha wudhuu wa Swalah”.([10])


Ninasema:

“Baada ya kuzipitia hoja za wenye kupinga na wenye kujuzisha kukaa Msikitini kwa mwenye janaba, mwenye hedhi na mwenye nifasi, ninaloliona mimi ni kuwa dalili za wenye kupinga hazifikilii uharamisho wa moja kwa moja ingawa nitasimama kuchekecha na kusubiri zaidi hapokatika suala hili. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi lililo sawa.”
 
([1]) Surat At-Tawbah : 27
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetangulia si mbali.
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (439).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (458) na Muslim (956). Ndani yake mna shaka kama alikuwa ni mwanamke au mwanamme. Lakini inatiliwa nguvu ya kuwa alikuwa ni mwanamke kutokana na tamshi la Hadiyth ya Ibn Khuzaymah na Al-Bayhaqiy (4/48) kwa sanadi nzuri.
([5]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6452) na At-Tirmidhiy (479).
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (3035) na Muslim (2479).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1650). Itakuja katika mlango wa “Hijja”.
([8]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Muslim (298), Abu Daawuud (261), At-Tirmidhiy (134) na An-Nasaaiy (2/192).
([9]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Muslim (299) na An-Nasaaiy (1/192).
([10]) Isnadi yake ni nzuri: Imetolewa na Sa’iyd bin Mansour katika (Sunan) (4/1275).

0 Comments