050-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (2)

NI KIPI KINATOSHELEZA KUTAYAMAMU?

Kutayamamu kunakuwa ni badala ya Wudhuu na josho la janaba wakati maji yanapokosekana au kuwa vigumu kuyatumia. An-Nawawiy amesema:
“Haya ndiyo madhehebu yetu. Na hivi ndivyo walivyosema Maulamaa wote katika Maswahaba, Taabi’ina na waliokuja baada yao isipokuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, Abdullaah bin Mas’uud([1]) na Ibraahiym An-Nakhi’y ambaye ni Taabi’i. Hawa wamelizuia, yaani wamezuia kutayamamu kwa ajili ya hadathi kubwa”.

Ibn As-Swibaagh na wengine wamesema kuwa inasemekana kuwa ‘Umar na Abdullaah waliachana na msimamo wao.

Jamaa zetu hawa na Jamhuri wametoa dalili ya kauli Yake Allaah Mtukufu:
((إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا وجوهكم))
((Mnaposimama kuswali, basi osheni nyuso zenu)).

Hadi Neno Lake:
((وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا))
((Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni)).

Kisha Allaah Mtukufu Akasema:
((فلم تجدوا ماء فتيمموا))
((na hamkupata maji, basi tayamamuni)).
Na hili linarejea kwa wote wawili; mwenye hadathi na mwenye janaba.([2])


Ninasema:
Kuna dalili nyingine juu ya ushari’ah wa kutayamamu kwa ajili ya hadathi kubwa. Ni Neno Lake Allaah Mtukufu:
((أو جاء أحد منكم من الغائط أو لامستم النساء فلم تجدوا ماء فتيمموا صعيدا طيبا)) 
 ((Au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi)).([3])

Makusudio ya kugusana hapa ni tendo la kujamii kwa mujibu wa kauli ya mjumuiko wa Maulamaa akiwemo Ibn ‘Abbaas.([4])

Kisha kuna Hadiyth Sahihi zilizopokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinazofahamisha kuwa kutayamamu hutosheleza janaba. Kati ya Hadiyth hizo ni:

1- Hadiyth tuliokwisha ielezea ya ‘Imraan bin Haswiyn wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia mwenye janaba:
((عليك بالصعيد فإنه يكفيك))
((Tumia mchanga, kwani unakutosha)).([5])

2- Hadiyth ya ‘Ammaar bin Yaasir, amesema: “Nilipata janaba, kisha nilijigaragaza mchangani, nikamjulisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya hilo, akaniambia:
((إنما كان يكفيك هكذا:
وضرب يديه على الأرض، ومسح وجهه وكفيه)).
((Hakika ilikuwa inakutosha hivi:
Akapiga mikono yake miwili juu ya ardhi, akosha uso wake na viganja vyake viwili)).([6])


JE, MAITI HUTAYAMAMISHWA MAJI YAKIKOSEKANA?

Maiti hutayamamishwa kama aliyehai maji yakikosekana, kwani kuoshwa kwake ni jambo la lazima. Tumekwishaeleza hapo kabla kuwa mchanga hutwaharishiwa kama maji hakuna.([7]) 
([1]) Imekuja katika Sahihi ya Al-Bukhaariy (345) na Muslim (796) kuwa Ibn Mas’uud amekataza kutayamamu kwa ajili ya janaba na kuwa Abu Muusa alimpinga kwa Aayah.
Ninasema: “Huenda Ibn Mas’uud kulipinga hilo, kumetolewa juu ya yale yaliyo sahihi kwake toka kwa At-Twabariy (9606) wakati alipolifasiri Neno Lake Allaah Mtukufu: ((أو لامستم النساء)) akisema kuwa الملامسة ni chini ya kujamii.
([2]) Al-Majmuu (2/240).
([3]) Surat An-Nisaa: 43
([4]) ((Tafsir At-Twabariy)) (9583) kwa sanadi sahihi kutoka kwake.
([5]) Imekubaliwa na wote. Imeelezewa karibuni.
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukaariy (338) na Muslim (798).
([7]) Angalia “Al-Muhalla” (2/158).

0 Comments