051-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (3)

HALI AMBAZO KUTAYAMAMU KUNARUHUSIWA

Inaruhusika kutayamamu katika hali mbili:

1.     Maji yanapokosekana, sawasawa ikiwa ni safarini au mjini.
2.     Inapokuwa vigumu kuyatumia. Na hili lina picha mbalimbali zitakazoelezewa baadaye In shaa Allaah.

Allaah Mtukufu Anasema:

((وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا ))
((Na mkiwa na janaba, basi jitwaharisheni, na mkiwa wagonjwa au mkiwa safarini, au ametoka mmoja wenu chooni, au mmewagusa wanawake na hamkuyapata maji, basi tayamamuni)). ([1])SI LAZIMA SAFARI IWE NDEFU ILI MSAFIRI AWEKEWE SHARIY'AH YA KUTAYAMAMU

Endapo maji yatakosekana, itampasa msafiri atayamamu sawasawa ikiwa safari ni ndefu au fupi katika kauli mbili sahihi zaidi za Maulamaa([2])kwa vile safari katika Aayah Tukufu ni mutlaki.

Ushahidi wa hilo ni:

1- Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Allaah Amridhie), amesema:
“Tulitoka na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika baadhi ya safari zake. Tulipokuwa Baydaa au Bidhaat Al-Jaysh, kidani changu kilikatika. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipiga kambi ili kukitafuta, na watu nao wakapiga kambi pamoja naye, hawako sehemu yenye maji na wala hawana maji…. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akalala mpaka akapambaukiwa bila kuwepo maji. Na hapo Allaah Mtukufu Akateremsha Aayah ya kutayamamu:
((فتيمموا صعيدا))
((Basi ukusudieni mchanga)).([3])


2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Allaah Amridhie) kwamba yeye alitokea Al-Juruf mpaka alipofika Al-Mirbad alitayamamu. Alipangusa uso wake na mikono yake miwili na akaswali Alasiri. Kisha aliingia Madiynah nailhali jua limepanda. Hakurejesha Swalah.([4])
Ash-Shaafi’iy amesema: Al-Juruf ni sehemu karibu na Madiynah.


SI LAZIMA SAFARI IWE HALALI

Ni sahihi kuwa msafiri hutayamamu katika safari yake – yanapokosekana maji – sawasawa ikiwa alisafiri safari ya halali au safari ya haramu. Kwa kuwa kutayamamu ni faradhi, haijuzu kukuacha kinyume na ruhusa nyinginezo. Na kwa vile kutayamamu ni hukumu isiyohusiana na safari, kwa ajili hiyo, imeruhusiwa katika safari za haramu kama kupukusa siku na usiku wake.([5])

Ninasema:

Na kwa vile faradhi haipomoki kwa msafiri, imekuwa ni lazima kwake afanikishe sharti ya kusihi kutayamamu, lakini madhambi atayapata kutokana na safari yake ya haramu. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 
([1]) Surat Al-Maaidah : 6
([2])“Al-Muhalla” (2/116) na “Al-Mughniy” (1/148).
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (334) na Muslim (764).
([4]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Maalik (Twahara uk.73) na Al-Bayhaqiy (1/224).
([5])“Al-Muhalla” (2/137), “Al-Mughni” (1/150) na “Al-Awswat” (2/32).

0 Comments