052-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (4)

MWENYE MAJI AMBAYO HAYATOSHI ILA KWA BAADHI YA VIUNGO VYAKE

Katika suala hili, Maulamaa wamehitilafiana katika mielekeo miwili:


Wa Kwanza:

Ataosha viungo awezavyo kuviosha na vilivyobaki atatayamamu. Haya ni madhehebu ya Ahmad, Ibn Hazm([1]) na moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy. Hoja yao ni Neno Lake Allaah Mtukufu:

((فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ))
((Mwogopeni Allaah muwezavyo)).([2])

Na kauli yake Mtume Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam:

      ((إدا أمرتكم بأمر فائتوا منه مااستطعتم))
((Nikiwaamuru jambo, basi lifanyeni kiasi muwezavyo)).([3])

Ibn Hazm amesema:
“Na huyu anaweza kuviosha baadhi ya viungo vyake vya Wudhuu au kuoga sehemu ya kiwiliwili chake, lakini hawezi sehemu zilizosalia, hapo ikafaradhishwa kwake aoshe kwanza viungo anavyoweza kuviosha katika Wudhuu au josho hadi kiungo atakachokifikia, na maji yanapoisha, itamlazimu kutayamamu kwa viungo vilivyosalia kwa kulazimika. Na hilo ni lazima, kwani yeye hana maji ya kujitwaharishia. Basi ni wajibu kwake kufidia kwa mchanga kama Alivyoamuru Allaah Mtukufu”.


Wa Pili:

Atatayamamu tu moja kwa moja. Mwelekeo huu ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Maalik na moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy. Pia mjumuiko wa Masalaf wamesema hili hili.([4])


Wamesema:
“Ni kwa vile haikusanywi pamoja twahara ya maji na twahara ya tayamumi; ni ima hii au ile.
Ibn Al-Mundhir ametoa dalili kuunga mkono mwelekeo huu akisema:([5])
“Allaah Mtukufu Anasema:

((وإن كنتم جنبا فاطهروا))
((Mkiwa na janaba, jitwaharisheni))

Amewajibisha kwa mwenye janaba kuoga kwa maji, na kama hakuyapata, basi atayamamu. Na Amewajibisha kwa mwenye kumfanyia mkewe dhihaar, amwache huru mtumwa, na kama hakumpata, basi afunge miezi miwili. Na alipokuwa mwenye kumiliki sehemu ya mtumwa lakini kiilivyo ni kama hammiliki na Allaah Akamfaradhishia kufunga, basi mwenye  maji ya kuoshea baadhi ya viungo vyake tu amekuwa ni kama asiyenayo Akamfaradhishiwa kutayamamu. Na jibu kuhusu mwenye kufanya tamattui na ana fedha pungufu za kununulia mnyama wa kuchinja, au aliyevunja kiapo chake na uwezo wake uko chini ya kuwalisha masikini kumi, hukumu yao ni kama ya hao tuliowataja.
Ama kufaradhiwa faradhi mbili kwa hao tuliowataja, hilo halijuzu.”


Ninasema:
“Na huenda lililo dhahiri zaidi ni kuwa atatayamamu tu moja kwa moja ili kutokusanya kati ya asili na badala. Pia ni kwa vile, lau kama hana maji ya kutosha kwa viungo vyake vyote vya Wudhuu au vya josho na akatumia badala (kutayamamu), basi anakuwa amefanya lile aliloliweza katika Amri ya Allaah na Mtume Wake pia.
Na linalonidhihirikia mimi ni kuwa huyu ambaye anatayamamu baada ya kuosha baadhi ya viungo vyake, bila shaka anakuwa ameipata twahara kwa kutayamamu tu, na wala si kwa kuosha na kutayamamu kwa pamoja, kwani kuosha baadhi ya viungo vyake kunakuwa hakuna maana yoyote baada ya kuwa na uhakika kwamba maji aliyonayo hayamtoshi. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.MWENYE MAJI, AKAHOFIA KUKABILIWA NA KIU YEYE MWENYEWE, AU MWENZAKE AU MNYAMA WAKE KAMA AKIYATUMIA

Ibn Al-Mundhir ([6]) amesema:
“Kila tuliyemhifadhi katika Maulamaa, wote wamekubaliana kuwa msafiri akijihofia nafsi yake kiu naye ana kiasi kidogo tu cha maji ya kujitwaharishia, basi atayabakisha maji yake kwa ajili ya kunywa, na atatayamamu”.

Na Ibn Qudaamah([7]) amesema:
“Mwenye kuhofia wanyama wake, huhofia kupotea mali yake. Mfano wake ni kama mtu kuyapata maji, na kati yake na maji hayo kukawa na mwizi anayeweza kupora chochote katika mali yake au mnyama mkali anayeweza kumdhuru mnyama wake. Na kama akimkuta mwenye kiu anayemhofia kufa, itamlazimu amnyweshe na yeye atatayamamu”.

  
 
([1])“Al-Muhalla” (2/137), “Al-Mughniy” (1/150) na “Al-Awswat” (2/32).
([2]) Surat At-Taghaabun : 16.
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (3199).
([4])“Al-Majmuu” (2/312) na “Majmuu Al-Fataawaa” (21/453).
([5])“Al-Awswat” ya Ibn Al-Mundhir (2/34).
([6])“Al-Awswat” (2/28).
([7])“Al-Mughniy” (1/165). Tazama “Al-Majmuu” (2/281).

0 Comments