054-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (6)

KUTAYAMAMU MGONJWA AMBAYE ANAJIHOFIA KUHILIKI KAMA ATATUMIA MAJI

Jamhuri ya Maulamaa (Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ibn Hazm na wengineo), wanaona kuwa ikiwa mgonjwa atajihofia nafsi yake kuhiliki ikiwa atatumia maji, basi inajuzu kwake kutayamamu kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((وإن كنتم مرضى أو على سفر.....فلم تجدوا ماء فتيمموا))
 ((Na mkiwa wagonjwa au safarini……na hamkupata maji, basi tayamamuni)).([1])
Amesema Mujaahid: “Nayo ni kwa mgonjwa aliyepatwa na janaba. Akijihofia nafsi yake, basi ana ruhusa ya kutayamamu kama msafiri anapokosa maji”.([2]) Na kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم))
((Na wala msiziue nafsi zenu)).([3])

Hii ni katika wakati ambapo ‘Atwaa([4]) na Al-Hasan wamekataza mgonjwa kutayamamu isipokuwa katika hali ya kukosekana maji tu kutokana na dhahiri ya Aayah.
Na jibu la hili ni kuwa Aayah ni hoja ya kutupa sisi nguvu na takdiyri yake ni:
((Mkiwa wagonjwa mkashindwa au mkahofia kutumia maji, au mkawa safarini na hamkupata maji, basi tayamamuni)).([5])


AKIHOFIA MGONJWA KUZIDI UGONJWA WAKE AU KUKAWIA KUPONA KWA KUTUMIA MAJI, JE, ATATAYAMAMU?

Jamhuri ya Maulamaa([6]) (Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili na Ibn Hazm), wanaona kwamba si lazima mgonjwa ahofie kuhiliki ndipo atayamamu, bali hata yule ambaye Wudhuu unamwongezea ugonjwa au unachelewesha kupona, basi atayamamu kutokana na ‘umuum ya Aayah ya Surat Al-Maaidah. Na pia kutokana na Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((يريد الله بكم اليسر ولا يريد منكم العسر))
((Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito)).
Ibn Hazm amesema: “Dhiki na uzito vimeondoka – na Sifa zote njema ni za Allaah – sawasawa ikiwa ugonjwa utazidi au haukuzidi. Kadhalika, ikiwa atahofia kuzidi ugonjwa, basi hilo ni uzito na dhiki vilevile”.

Na imepokelewa toka kwa Ahmad na Ash-Shaafiiy katika moja ya kauli zake mbili kwamba imeshurutishwa kuhofia kuhiliki ili kuruhusika kutayamamu. Na madhehebu ya Jamhuri ndio sahihi zaidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
([1]) Surat Al-Maaidah : 6
([2]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Abdur-Raaziq kwa sanadi sahihi.
([3]) Surat An-Nisaa: 29.
([4]) Abdur-Raaziq amelipokea hili katika “Al-Muswannaf” (861) kwa sanadi sahihi.
([5]) “Al-Majmuu” (2/330).
([6]) “Al-Mabswuut” (1/121), “Al-Majmuu” (2/331), Al-Muhalla (2/116), Al-Awswat (2/26) na Majmuu Al-Fataawa (21/399).

0 Comments