055-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (7)

NINI ATAFANYA MWENYE JERAHA (KIDONDA)?

Suala hili lina matawi juu ya asli. Ni kuwa, je, hukusanywa kati ya asili na badala, yaani Wudhuu – au ghusli – na Tayammumi au haikusanywi?
Na hili lishazungumziwa.([1])

Waliopinga kukusanya kati ya viwili (asili na badala) kama Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo tulilolitilia nguvu katika mlango uliopita, wameelekea kufuata kilicho kichache zaidi kwa kilicho kingi zaidi. Ina maana kuwa endapo sehemu kubwa ya mwili ina majeraha, basi mtu atatayamamu bila kuviosha viungo vizima vilivyobakia. Na ikiwa sehemu kubwa ya mwili ni nzima, atauosha mwili na ataacha sehemu yenye majeraha.([2])

Ama wale waliojuzisha kukusanya kati ya ghusli na tayammumi, wanasema kuwa ataosha sehemu nzima ya mwili na yenye majeraha ataifanyia Tayammumi. Ash-Shaafi’y na Ahmad wamelisema hili, na Shaykh wa Uislamu anaonekana kama amelikhitari.([3])

Ninasema: “Inavyoonekana ni kuwa rai ya kwanza ndio sahihi zaidi kama ilivyotangulia, na hakuna katika mlango huu Hadiyth yoyote sahihi iliyopokelewa toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Lakini pamoja na haya, kuna Hadiyth ya Jaabir iliyopokelewa. Anasema: “Tulitoka kwenda safari. Mtu mmoja kati yetu alijeruhiwa na jiwe kichwani. Kisha baadae aliota usingizini, na alipoamka aliwauliza wenzake: “Je, mwaweza kunipatia ruhusa ya kutayamamu? Wakasema: “Hatuwezi kukuruhusu kutayamamu nailhali unaweza kuyatumia maji.” Mtu yule alioga akafa. Tulipokuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alijulishwa hilo na akasema:
((Wamemwua, Awaue Allaah! Kwa nini wasiulize kama hawajui? Kwani hakika ponyo la asiyejua ni kuuliza. Hakika ilikuwa inamtosheleza Tayammumi)).([4])
Hadiyth hii ni dhaifu. Walioidhoofisha ni Al-Bayhaqiy, Ibn Hazm na wengineo ingawa Al-Albaaniy ameifanya kuwa Hasan.

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, amesema: “Endapo kama jeraha halikufungwa, ataosha sehemu za pembeni yake na wala hatoliosha.”([5])

Na imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa ‘Ubayd bin ‘Umayr kuhusiana na mtu aliyepatwa na janaba akiwa na jeraha: “Aoshe sehemu ya pembeni na wala maji yasikurubie jeraha lake”([6]).

Na hili liko sanjari na madhehebu ya Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo lenye nguvu. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
([1]) Rejea nyuma.
([2]) “Al-Mabswuut” (1/112) na “Al-Majmuu” (2/333).
([3]) “Al-Mughniy” (1/162), “Al-Majmuu” (1/162) na “Majmuu Al-Fataawaa”(21/466).
([4]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (336), Ad-Daar Qutniy (1/190) na Al-Bayhaqiy (1/237). Sanadi yake ni dhaifu. Al-Albaaniy ameifanya kuwa ni Hadiyth Hasan kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyopo kwa Abuu Daawuud (337) na Ibn Maajah (572).  Hadiyth hii ni “Munqatwi” na haifai kutolewa ushahidi.
([5]) Isnadi yake ni dhaifu: Imetolewa na Al-Bayhaqiy.
([6]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Abdur-Raaziq (865).

0 Comments