056-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (8)

JE, ANAYEOGOPA MAJI BARIDI INAJUZU KWAKE KUTAYAMMAMU KAMA ANA JANABA?

Anayejihofia kufa kutokana na ubaridi wa maji, inajuzu kwake kutayammamu kwa vile anakuwa katika ngazi ya mgonjwa. Huu ni mwelekeo wa Jamhuri ya Maulamaa.([1]) Hoja yao katika hili ni:

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم إن الله كان بكم رحيما))
((Wala msiziue nafsi zenu, hakika Allaah ni Mrehemevu mno kwenu)).([2])

2- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa ‘Amru bin Al-‘Aas kwamba wakati alipopelekwa katika vita vya Dhaati As-Salaasil alisema: “Niliota katika usiku wa baridi kali, nikahofia kufa kama nitaoga. Nikatayammamu, kisha nikaswali na wenzangu Swalah ya Alfajiri. Tulipowasili kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wao walimweleza hilo, akasema:

((يا عمرو، صليت بأصحابك وأنت جنب؟))
((Ewe ‘Amri! Hivi umeswali na wenzako ukiwa na janaba?))

Nikamwambia: “Nililikumbuka Neno la Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم إن الله كان بكم رحيما))
Nikatayammamu kisha nikaswali. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akacheka, na hakusema neno)).([3])

Hadiyth hii ina mvutano, na lenye nguvu ni kuwa ni dhaifu. Lakini pamoja na hivyo, kaida za kishari’ah zinaitolea ushahidi. Vile vile mwelekeo huu unaungwa mkono na Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ما يريد الله ليجعل عليكم من حرج))
((Hataki Allaah kuwafanyieni uzito)).([4])

Na hii ni baada ya kutaja Tayammumi. Kana kwamba Ameashiria kuwa Tayammumi inakuwa ni shari’ah panapokuwepo uzito wa kutumia maji. Na hakuna shaka kuwa ubaridi mkali wa maji ni katika uzito huo. Lakini inatakikana kutanabahisha kuwa kutayammumi hakuwi ni shari’ah – katika hali hii – ila baada ya kushindwa kupasha maji moto. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
([1]) “Al-Mabswuut” (1/122), “Al-Majmuu” (2/330), “Al-Istidhkaar” (3/173), “Al-Mughniy” (1/163),” Al-Muhalla” (2/134) na “Majmuu Al-Fataawaa” (21/399).
([2]) Surat An-Nisaa: 29
([3]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (334), Ahmad (3/203), Ad-Daar Qutniy (1/178), Al-Haakim (1/177) na Al-Bayhaqiy (1/225). Sanadi na matni yake, zimetiwa doa. Al-Albaaniy katika Al-Irwaa (1/182) amesema kuwa ni sahihi.
([4]) Surat Al-Maaidah: 6

0 Comments