057-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (9)

AMBAYE WAKATI UMEKUWA MFINYU KWAKE NA WAKATI WA SWALAH UTAMPITA KAMA ATATUMIA MAJI, JE, ANAWEZA KUTAYAMMAMU?

Kuna kauli mbili za Maulamaa katika suala hili:


Ya kwanza:

Haijuzu kutayammamu hata kama wakati utampita. Limesemwa hili na Mashaafi’iy, Mahanbali na Abuu Yuusuf([1]). Dalili zao ni:

1- Neno Lake Allaah Mtukufu:

((إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا وجوهكم.... فلم تجدوا ماء فتيمموا))
((Mnaposimama kuswali, basi osheni nyuso zenu….na hamkupata maji, basi tayammamuni)).([2])

Wanasema: “Hapa kukosa maji kumefanywa kuwa ni sharti ya kuhalalika kutayammamu”.

2- Hadiyth ya Abuu Hurayrah ikiwa Marfuu:

((لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ))
((Allaah Hakubali Swalah ya mmoja wenu anapokuwa na hadathi mpaka atawadhe)).([3])

3- Hadiyth ya Ibn ‘Umar ikiwa Marfuu:

((لا تقبل الصلاة بغير طهور ولا صدقة من غلول))
((Swalah haikubaliwi bila ya Wudhuu, wala Swadaqah ya mali haramu)).([4])

Hapa mtu kaamuriwa kutumia maji. Ikiwa ataiwahi Swalah, basi vizuri, na kama itampita kwa kuzembea kwake, basi hayo amejitakia mwenyewe.


Ya pili:

Ni shari’ah kwake kutayammamu na kuswali kabla wakati haujampita.
Wamelisema hili Ahlu Rra’ayi, Al-Awzaa’iy, Maalik, Ibn Hazm. Shaykh wa Uislamu amelikhitari hili.([5])
Mahanafi wameliwekea hili sharti ya kuwa ni lazima liwe kwa Swalah ambayo haina badala yake kama Swalah ya maiti. ([6])

Hoja zao ni:
1- Hadiyth ya Abu Juhaym Al-Answaariy, amesema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja akitokea upande wa kisima cha Jamal. Mtu mmoja alikutana naye akamsalimia. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuitikia mpaka alipokwenda ukutani, akapukusa uso na mikono yake. Kisha akamjibu salamu”.([7])

Wamesema: Na hii ni asili katika kujuzu kutayammamu kwa ajili ya kuhofia kupitwa na faradhi.

2- Ibn Abdil-Barri amesema katika “Al-Istidhkaar” (3/171):
“Kila ambaye hakuyapata maji na akachelea kupitwa na Swalah, anaweza kutayammamu kama ni mgonjwa au msafiri kwa matini. Na kama ni mkazi, basi ni kwa maana. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

3- Shaykh wa Uislamu amesema:
“Kauli sahihi zaidi ya Maulamaa ni kuwa atatayammamu kwa kila lile analolichelea kupitwa nalo kama Swalah ya maiti, Swalah za ‘Iyd mbili na kadhalika. Swalah kwa kutayammamu ni bora zaidi kuliko kuipitiza…”

Na amesema tena:
“Vile vile, kama hakuweza kuswali Swalah ya jamaa ya faradhi ila kwa kutayammamu, basi ataiswali kwa kutayammamu”.

Ninasema:
“Na huenda lililo wazi zaidi ni kuwa mtu atatayammamu ili aiwahi Swalah, kwani Tayammumi imewekwa kwa ajili ya kuuwahi wakati wa Swalah na kuchelea kupitwa ili kuulinda wakati. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
 
([1]) “Al-Mughniy” (1/166), “Al-Majmuu” (2/280), “Al-Istidhkaar” (3/171) na“Tamaam Al-Minnah” (uk.132).
([2]) Surat Al-Maaidah : 6
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6954) na Muslim (526).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (524, At-Tirmidhiy (1) na Ibn Maajah (272).
([5]) “Al-Mughniy” (1/166), “Al-Muhalla” (2/117), “Majmuu Al-Fataawaa”(21/439,456) na “Al-Awsatw” (2/30).
([6]) “Al-Mabsuutw” (1/118,119).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (337) na Muslim (800).

0 Comments