058-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (10)

ANAYEAMKA USINGIZINI, MUDA WA SWALAH UKAWA MFINYU, JE, ATAYAMMAMU ILI AUWAHI WAKATI?

Kuna mielekeo miwili katika suala hili mfano wa ile iliyoko katika suala lililotangulia:

Wa kwanza:
Atatayammamu na ataswali ndani ya wakati. Hili limesemwa na Maalik, Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy na Ibn Hazm.

Wa pili:
Ataoga na ataswali na hata baada ya kutoka wakati. Huu ni msimamo wa Jamhuri, na Shaykh wa Uislamu ameukhitari.  
Msimammo huu ndio wenye nguvu zaidi, kwani wakati kwa mwenye kulala ni pale anapoamka.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((أما إنه ليس في نوم تفريط، إنما التفريط على من لم يصل الصلاة حتى يجئ وقت الصلاة الأخرى، فمن فعل ذلك فليصلها حين ينتبه بها))

((Ama hakika, hakuna uzembe kwa aliyelala, bali uzembe ni kwa yule ambaye hakuswali mpaka ukaingia wakati wa Swalah nyingine. Mwenye kufanya hivyo, basi aiswali anapoikumbukia)).([1])

Ibn Taymiyah amesema (22/35):
“Na kama ni hivyo, kama ataamka kabla ya kuchomoza jua na hakuweza kuoga na kuswali ila baada ya kuchomoza, basi anakuwa ameiswali Swalah katika wakati wake na wala hazingatiwi kuwa ameipitisha. Ni kinyume na yule aliyeamka mwanzoni mwa wakati. Huyu wakati wake ni kabla ya kuchomoza jua, atahadhari asiuachie wakati wa Swalah ukamtoka.
 
([1]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (1532) na Abuu Daawuud (437). Na imekuja katika Swahiyh Mbili katika Hadiyth Marfuu iliyopokelewa na Abuu Hurayrah:
من نسي صلاة فليصلها إذا ذكرها لا كفارة لها إلا ذلك
((Aliyeisahau Swalah, basi aiswali anapoikumbuka, hakuna kafara yake ila hilo)).

Na katika tamshi la Muslim katika Hadiyth ya Anas:

من نسي صلاة أو نام عنها فكفارتها أن يصليها إذا ذكرها
((Aliyeisahau Swalah, au akalala ikampita, basi kafara yake ni kuiswali anapoikumbuka)).

0 Comments