060-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutayamamu (12)

MWENYE KUKOSA VITWAHARISHO VIWILI (MAJI NA MCHANGA)

Kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa kuhusiana na mtu aliyekosa vitwaharisho viwili (maji na mchanga) ni kuwa ataswali katika hali aliyonayo katika wakati wa Swalah na wala hatoirejesha.
Huu ni mwelekeo wa Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm. Ibn Taymiyyah ameukhitari mwelekeo huu([1]).

Hoja yao ni kauli Yake Allaah Mtukufu:
((فاتقوا الله مااستطعتم))
((Basi mcheni Allaah mwezavyo)).([2])

Na Neno Lake Allaah Mtukufu:
((لا يكلف الله نفسا إلا وسعها))
((Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa uwezo wake)).([3])

Na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((إذا أمرتكم بأمر فائتوا منه مااستطعتم))
((Nikiwaamuruni jambo, basi lifanyeni kwa uwezo wenu)).([4])

Wamesema: “Huyu amefanya alichoweza katika Swalah, na jambo la kujitwaharisha ambalo hakuliweza, limemwondokea. Na kwa hilo, anakuwa ametekeleza aliloamuriwa, na mwenye kutekeleza aliloamuriwa, basi hatolipa”.

Ninasema: “Na huenda mwelekeo huu unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtuma Asyad bin Al-Khudhayr – na hali mimi nasikia – kukitafuta kidani nilichokipoteza. Ukafika wakati wa Swalah, nao wakaswali bila ya Wudhuu. Kisha wakamjia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakamweleza hilo, na hapo ikateremshwa Aayah ya tayammum”.([5])

Na ushahidi hapa ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakubalia – wakati walipokosa maji – kuswali bila ya Wudhuu na wala hakuwaamuru kurejesha Swalah. Na endapo kama watakosa mchanga vile vile, basi hukumu ni hiyo hiyo. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

Na kwa upande mwengine, Abuu Haniyfah, Asw-haabur Ra-ay, Maalik na Al-Awzaa’iy, wao wanaona kwamba hatoswali mtu mpaka apate maji ya kutawadhia au mchanga wa kutayamamia, hata kama wakati utatoka.([6])
 
([1]) “Al-Mughniy” (1/157), “Al-Majmuu” (2/321), “Al-Muhalla” (2/138) na “Al-Fataawaa” (21/467).
([2]) Surat At-Taghaabun: 16
([3]) Surat Al-Baqarah: 286.
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (3199).
([5]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5882) na Muslim (795).
([6]) “Al-Awswat” (2/45), “Al-Istidhkaar” (3/150) na “Al-Muhallaa” (2/139).

0 Comments