062-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Hedhi Na Nifasi (1)

HEDHI NA NIFASI

Damu za kimaumbile zinazomtoka mwanamke zinagawanyika vigawanyo vitatu:
1- Damu ya hedhi
2- Damu ya nifasi
3- Damu ya istihadha


DAMU YA HEDHI([1])

Ni damu nyeusi nzito yenye harufu mbaya. Inamtoka mwanamke toka sehemu maalumu katika nyakati maalumu.
Hedhi ni jambo ambalo Allaah Amewaumbia  wanawake wote kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwambia  Aaishah kama ilivyo katika sahihi mbili:

(( إن هذا أمر كتبه الله على بنات آدم....))
((Hakika hili ni jambo, Allaah Amelihukumia kwa mabinti wa Aadam)).

Bali Hawwaa Amani iwe juu yake alianza kuipata. Imepokelewa kwa isnadi sahihi toka kwa Ibn 'Abbaas akisema:
“Hedhi ilianza kutoka kwa Hawwaa baada ya kushushwa toka peponi”.

Na hakuna mpaka wa uchache wala wingi wa hedhi, bali hilo linategemea maumbile ya mwanamke, kwa vile hakuna dalili yoyote sahihi toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayobainisha uchache wa hedhi au wingi wake.

Shaykh wa Uislamu katika Kitabu cha Al-Fataawa (21/623) anasema:
“Ama wale wanaosema kwamba wingi wa hedhi ni siku kumi na tano na uchache wake ni siku moja kama Ash-Shaafi’iy na Ahmad, au wanaosema kuwa hedhi haina mpaka maalumu kama Maaliki, hakika wao wanasema hayo, lakini halijathibiti lolote kuhusiana na hilo toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Maswahaba zake. Na marejeo ya yote hayo ni maumbile ya mwanamke kama tulivyosema, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.”([2])


KUANZA NA KUMALIZIKA KWA HEDHI([3])

1- Kuanza kwa hedhi kunajulikana kwa msukumo wa damu wakati wake, nayo ni damu nyeusi, nzito yenye harufu mbaya.

2- Kumalizika kwake hujulikana kwa kukatika damu, kuwepo unjano na rangi yenye kumili weusi. Na hili linatokana na mambo mawili:

(a) Ukavu; nako ni kutoka kikiwa kikavu kilichoingizwa katika njia ya uzazi. Yaani ikiwa mwanamke ataingiza kitambaa au pamba katika utupu wake, basi hutoka kikiwa kikavu.

(b) Kuwepo maji meupe yanayotoka katika njia ya uzazi wakati wa kukatika damu ya hedhi. Imepokelewa na mwachwa huru wa ‘Aaishah akisema:

“Wanawake walikuwa wakimwendea na kitambaa chenye pamba yenye unjano utokanao na damu ya hedhi, kisha wanamuuliza kama wanaweza kuswali, naye huwajibu akisema: “Msifanye haraka mpaka mwone maji meupe”.
Hapa anamaanisha kwamba wametwaharika na hedhi([4]).


NINI HUKUMU YA UNJANO NA RANGI YENYE KUMILI WEUSI BAADA YA KUTWAHARIKA NA HEDHI?

Unjano na rangi yenye kumili weusi ni maji anayoyaona mwanamke mithili ya usaha. Na hii ni baada ya kukatika damu au baada ya ukavu na kujitwaharisha. Hapo ataswali, atafunga na mumewe atamwingilia.

Dalili ya hili ni Hadiyth ya Ummu 'Atwiyyah aliposema:
“Tulikuwa - baada ya kujitwaharisha - hatushughulishwi chochote na rangi yenye kumili weusi au unjano”([5]).

 

(1)Majina mengineyo ya hedhi ni:
 الطمث – العراك – الضحك – الإكثار – الإعصار. (Al-Muhadh-dhab 1/341).

(2)Jaami'i Ahkaam An-Nisaa (1/179),
angalia Al-Muhalla (2/191) na Al-Mughniy (1/308).

(3) Jaami'i Ahkaam An-Nisaa (1/200)
na kurasa zinazofuatia.

(4)Ni Hadyth Hasan kwa nyingine. Imetolewa na Maalik (uk 59), Al-Bukhaariy akitoa maelezo (1/420 - Fath) na ‘Abdur-Raaziq (1/302) kwa sanadi yenye udhaifu ingawa ina ushahidi kwa Ad-Daaramiy (1/214), na Al-Bayhaqiy (1/337). Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

(5) Imetolewa na Abu Daawuud (307), An-Nasaaiy (1/186), Ibn Maajah (647) na wengineo. Al-Bukhaariy ameitoa bila ya ziada (326).

0 Comments