063-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Hedhi Na Nifasi (2)

YALIYOHARAMISHWA KWA MWENYE HEDHI NA NIFASI

1-    KUSWALI

Maulamaa wote wamekubaliana kwamba ni haramu kwa mwenye Hedhi au Nifasi kuswali, sawasawa ikiwa ni Swalah ya Faradhi au ya Sunnah. Wamekubaliana kwamba ufaradhi wa Swalah huporomoka, na kuwa hatozilipa atakapotwaharika([1]).
Imepokelewa toka kwa Abu Saiyd akisema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أليس إذا حاضت لم تصل ولم تصم؟ فذلك نقصان دينها))
((Je, si anapoingia Hedhini haswali wala hafungi? Basi hilo ni upungufu wa Dini yake)).([2])

Na imepokelewa na Mu'aadhah kwamba mwanamke mmoja alimwambia ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):
"Je, inamtosheleza mmoja wetu Swalah yake anapotwaharika?" Akamjibu: "Je, wewe ni Ahruriyyah?([3]) Sisi tulikuwa tukiingia Hedhini tukiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuwa akituamrisha, au akasema: Hatuiswali"([4]).


FAIDA

1-   Endapo mwanamke ataingia Hedhini muda mfupi kabla ya kuingia Swalah ya Alasiri kwa mfano, na hakuwa ameswali Adhuhuri, je itamlazimu alipe Swalah ya Adhuhuri baada ya kutwaharika?

Ikiwa kwa mfano itamjia muda mfupi kabla ya Alasiri na hakuwa ameswali Adhuhuri, basi atailipa Swalah hiyo ambayo ilimwajibikia kabla ya kupata Hedhi wakati anapotwaharika. Hii ndio rai ya Jamhuri ya Maulamaa. Sababu ni kuwa Swalah ilikuwa imemwajibikia, na ni lazima ailipe madhali wakati wake uliingia hali ya kuwa yuko twahara kwa kiasi cha rakaa. Hii ni kwa neno Lake Allaah Mtukufu:

((إنَّ الصَّلاةَ كَانَتْ عَلَى المُؤْمِنِينَ كِتَاباً مَّوْقُوتا))
((Hakika Swalah ina wakati wake maalumu kwa Waumini))([5])

Kuna kauli nyingineyo isemayo kwamba haimlazimu kuilipa Adhuhuri. Wenye kusema hivi wanatoa dalili inayoashiria kuwa wanawake wakati wa enzi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakipata Hedhi nyakati zote, lakini haikupokelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru mwanamke yeyote kuswali Swalah iliyompita kabla ya kupata Hedhi anapotwaharika.
Shaykh wa Uislamu anasema katika Al-Fataawa (23/235):
"Dalili yenye nguvu zaidi ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maalik isemayo kuwa halazimiwi na chochote, kwani kulipa kunapasa kwa jambo jipya, na hapa hakuna lolote linalompasa kulipa, mbali na kuwa alichelewesha ucheleweshaji usio wa kuzembea".
Ama aliyelala hata kama hakuzembea, basi analolifanya si kulipa, bali huo ni wakati wa Swalah yake wakati anapoamka na akakumbuka."


2-   Anapotwaharika mwenye Hedhi muda mfupi kabla ya Alasiri kwa mfano, kisha baada ya kuoga wakati wa Alasiri ukawa umeshaingia, je, ni lazima aswali Adhuhuri?

Anapotwaharika na Hedhi na Nifasi kabla ya kuingia Magharibi, itamlazimu aswali Adhuhuri na Alasiri za siku hiyo. Vile vile, anapotwaharika kabla ya kuchomoza Alfajiri, itamlazimu aswali Magharibi na ‘Ishaa za usiku huo kwa vile wakati wa Swalah ya pili ndio wakati wa Swalah ya kwanza katika hali ya udhuru.
Katika Al-Fataawa 2/334, Shaykh wa Uislamu anasema:
"Na kwa haya, ndivyo yalivyo madhehebu ya Jamhuri ya Maulamaa kama Maalik, Ash-Shaafi'iy na Ahmad, na kwamba mwenye Hedhi anapotwaharika mwishoni mwa mchana, atazisali Adhuhuri na Alasiri zote. Na anapotwaharika mwishoni mwa usiku, ataswali magharibi pamoja na ‘Ishaa. Na hivi ndivyo ilivyonukuliwa toka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Abu Hurayrah na Ibn 'Abbaas, kwa vile wakati ni mmoja kati ya Swalah mbili katika hali ya udhuru. Hivyo basi, akitwaharika mwishoni mwa mchana, wakati wa adhuhuri hubakia na ataiswali kabla ya alasiri. Na akitwaharika mwishoni mwa usiku, basi wakati wa Magharibi hubakia katika hali ya udhuru na ataiswali kabla ya isha." Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.


3-   KUFUNGA

Imekubalika kwa Ijmaa’ ya Maulamaa kuwa mwenye Hedhi na Nifasi hafungi, lakini atazilipa siku za Ramadhaan.
‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: "Hilo lilikuwa likitupata (Hedhi) na tunaamrishwa kulipa Swawm, lakini hatuamrishwi kulipa Swalah".([6])


FAIDA

1- Mwenye Hedhi akitwaharika kabla ya Alfajiri na hakuoga, je, atafunga?
Ikiwa mwenye Hedhi atatwaharika kabla ya Alfajiri na akanuia kufunga, basi Swawm yake ni sahihi, kwani kusihi kwa Swawm yake hakutegemei kuoga, kinyume na Swalah. Na hii ni kauli ya Jamhuri.([7])


2-    Akitwaharika mwenye Hedhi kabla ya kuchwa jua, je, atafunga mchana uliobakia?

Si lazima ajizuie kula mchana uliobakia, kwani alikwishafungua tokea mwanzo, lakini atailipa siku hiyo.

Imepokelewa toka kwa Ibn Jurays akisema: "Nilimwambia 'Atwaa: Mwanamke akiingia Hedhini, kisha akatwaharika sehemu ya mchana, je atakamilisha? Akasema: Hapana, bali atalipa".

 
([1]) Al-Majmuu ya An-Nawawiy (2/351) na Al-Muhalla (2/175) ya Ibn Hazm.
([2])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al Bukhaariy (1951), Muslim (80) na wengineo.
([3]) Ni sifa ya mwenye kufuata madhehebu ya Khawaariji. Baadhi yao walikuwa wakiwajibisha kulipa Swalah kwa mwenye Hedhi.
([4])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (321) na Muslim (uk. 265).
([5]) Surat An-Nisaa: 103.
([6]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (265) na Abu Daawuud (263).
([7]) Fath Al Baariy (1/192).

0 Comments