064-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Hedhi Na Nifasi (3)

3- KUMWINGILIA SEHEMU YA UTUPU

Maulamaa wote([1]) wamekubaliana kwamba haijuzu kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu. Allaah Mtukufu Ameliharamisha hilo katika Kauli Yake:

((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))
((Basi waepukeni wanawake katika hedhi))([2])

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)anasema:

(( اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))
((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujamii))([3]).

Shaykh wa Uislamu katika Al-Fatawaa (21/624):
"Kuwaingilia wenye nifasi ni kama kumwingilia mwenye hedhi, na hilo ni haramu kwa makubaliano ya Maimaam.


FAIDA
1-    Ikiwa Muislamu ataitakidi kuwa ni halali kumwingilia mwanamke mwenye hedhi katika utupu wake, basi atakuwa ni kafiri aliyeritadi. Na lau kama mtu atalifanya hilo bila kuitakidi kuwa ni halali; ima kwa kusahau au kutojua kuwepo hedhi, au hajui kuwa hilo ni haramu, au akalazimishwa, basi hana makosa, na hatoi kafara.

Na ikiwa atamwingilia kwa kukusudia akijua kwamba mkewe yuko mwezini na kuwa hilo ni haramu na bila kulazimishwa, basi atakuwa ametenda dhambi kubwa, na ni lazima atubie([4]).


Na Je, Atawajibika Kutoa Kafara Kwa Kufanya Hivyo?
Jamhuri ya Maulamaa – kinyume na Ahmad – wanasema kuwa hapaswi kutoa kafara.

Ninasema:
"Hili ndilo sahihi. Ama Hadiyth ya Ibn 'Abbaas aliyoipokea toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa anasema kuhusiana na mtu anayemwingilia mkewe akiwa hedhini kwamba ((Anatoa Swadaqah dinari moja au nusu dinari))*, basi ni Hadiyth dhaifu kwa kauli yenye nguvu. Na kuchukua mali ya Muislamu ni haramu kiasili, na si halali kuitwaa mali hiyo ila kwa matini.

2-    Kinachokatazwa kustarehe na mwenye hedhi ni tupu basi**. Mume anaruhusiwa kumchezea popote atakapo isipokuwa kuingiza dhakari yake katika utupu.  
Na dalili ya hilo ni Hadiyth ya Anas. Anasema kwamba iliposhuka Kauli Yake Allaah Mtukufu:
((فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي المَحِيضِ))
((Basi waepukeni wanawake katika hedhi))([5])

Hapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
((اصنعوا كل شيئ إلا النكاح))
((Fanyeni kila kitu isipokuwa kujamii))([6])

Na imepokelewa toka kwa baadhi ya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakisema:
"Alikuwa anapotaka kitu kwa mwenye hedhi, hutupia nguo juu ya utupu wake".([7])


Ninasema:
"Lenye kutilia nguvu zaidi kauli hii ni Hadiyth ya Masruuq. Alimwambia mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): "Ninataka kukuuliza jambo lakini naona hayaa. Akasema: Mimi ni mama yako, na wewe ni mwanangu. Akasema: Ni jambo lipi ambalo mtu anaweza kulifanya kwa mkewe akiwa hedhini? Akasema: Anaweza kufanya mambo yote, isipokuwa utupu wake".([8])

Na hakuna shaka kuwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ndio mjuzi zaidi wa hukumu ya suala hili, kwa kuwa yeye ndiye mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).


Tanbihi
Kauli nyingine ya Maulamaa inasema kuwa linalojuzu kwa mwanamume kustarehe na mkewe wakati wa hedhi ni kila kitu, isipokuwa sehemu iliyopo kati ya kitovu na magoti. Kauli hii ina dalili zake([9]), lakini kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu. Na Allaah Mtukufu Ndiye Ajuaye Zaidi.


3-    Mwanamke anapotwaharika hedhi, haijuzu kwa mumewe kumwingilia mpaka aoge. Allaah Mtukufu Anasema:

 ((ولا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّى يَطْهُرْنَ فَإذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))
))Wala msiwakurubie mpaka watwaharike, na wanapotwaharika, basi waingilieni pale Alipowaamrisheni Allaah)).([10])

Mujaahid anasema: "Wanawake wana twahara mbili; twahara ya Kauli Yake Allaah Mtukufu:


((حَتَّى يَطْهُرْنَ))
Yaani wanapooga, na hahalaliki kwa mumewe mpaka aoge.

Anasema:

((فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّهُ))
Pale inapotoka damu, na kama hakumwingilia pale Alipoamrisha Allaah, basi si katika wenye kutubia wala wenye kujitwaharisha"([11]).
Maulamaa wote wamekubaliana kwamba mwanamke haingiliwi na mumewe – hata kama damu imekatika – mpaka aoge, kinyume na Ibn Hazm.


· Ikiwa mke wa Muislamu ni Ahlul-Kitaab, je atalazimishwa kuoga?
Atalazimishwa kuoga, na mumewe haruhusiwi kumkurubia mpaka baada ya kuoga, kwani aayah haimbagui mwanamke Muislamu na asiye Muislamu([12]).


4-    Ni lazima mwanamke mwenye hedhi amgomee mumewe akitaka kumwingilia, lakini kama atazidiwa nguvu, basi habebi jukumu, bali ataomba maghfira kwa Allaah Mtukufu([13]).


4- KUTUFU
Kwa Ijmaa’ ya Maulamaa, ni haramu kwa mwenye hedhi kutufu. Na dalili ya hili ni Hadiyth ya mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba alipopata hedhi wakati wa kufanya ‘amali za Hijjah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

(( إفعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت حتى تطهري))
((Fanya ayafanyayo mwenye kuhiji, lakini usitufu Nyumba (Ka'bah) mpaka utwaharike))([14]).
 
([1]) Al-Muhalla (2/162), Majmuu Al-Fataawaa (21/624) na Tafsiyr At-Twabariy(4/378).
([2])Surat Al Baqarah : 222
([3])Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (203), Abu Daawuud, An Nasaaiy, At Tirmidhiy na Ibn Maajah.
([4]) An-Nawawiy katika Sharh Muslim (3/204).
*  Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Abu Daawuud (264), An Nasaaiy (1/153), na Ibn Maajah (640).
**  Ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Ahmad na Is-haaq. Pia Muhammad bin Al-Hasan na Atw-Twahaawiy katika Mahanafi, na baadhi ya wafuasi wa Maalik. Vile vile ni moja ya kauli mbili za Ash-Shaafi'iy. Aidha, limeungwa mkono na Ibn Al-Mundhir na An-Nawawiy (Fa-th Al-Baariy) (1/404). Ni madhehebu ya Ibn Hazm vile vile.
([5])Surat Al Baqarah: 222.
([6]) Imegusiwa kabla.  
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abu Daawuud (272) kwa sanadi sahihi.
([8]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Atw-Twabariy katika ((At-Tafsiyr)) (4/378) kwa sanadi sahihi, nayo ina njia kadhaa.
([9]) Haya ni madhehebu ya Maulamaa wengi. Angalia kwenye Jaami’ Ahkaam A- Nisaa (1/140) na kurasa zinazofuatia.
([10])Surat Al-Baqarah: 222.
([11]) Imetolewa na Abdur-Raaziq (1272) na Al-Bayhaqiy (1/310) kwa sanadi sahihi hadi kwa Mujaahid.
([12]) Tafsiyr ya Atw-Twabariy (3/90).
([13]) Jaami’ Ahkaam An-Nisaa (1/180).  
([14]) Imetolewa na Al Bukhaariy (1650).

0 Comments