065-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Hedhi Na Nifasi (4)

HEDHI NA NIFASI 4

MAMBO YANAYORUHUSIWA KWA MWENYE HEDHI


1- Kusoma Nyiradi Na Qur-aan
Kama ilivyotangulia nyuma, inajuzu kwa mwenye hedhi au janaba kufanya hivyo kwa kauli yenye nguvu zaidi. Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na mashuhuri katika madhehebu ya Ash-Shaaf'iy na Ahmad.([1])
Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (1/77, 78) anasema:
"Kusoma Qur-aan, kusujudu kwenye Aayah ya Sajdah, kuugusa Msahafu na kufanya nyiradi, hayo ni matendo ya kheri, yaliyosuniwa na yenye thawabu. Basi mwenye kudai kwamba hilo halifai, basi alete dalili".


2- Kusujudu Kama Atasikia Aayah Ya Sajdah
Hakuna ubaya mwanamke mwenye hedhi kusujudu anaposikia Aayah ya Sajdah, kwani Sajdah si Swalah, na wala si lazima awe na twahara.
Imethibiti katika Swahiyh Al-Bukhaariy (4862) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Suurat An-Najm, akasujudu yeye, kisha wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na wanaadamu.
Ni mbali kusema kuwa wote walikuwa na Wudhuu, kisha Sajdah ya kisomo si Swalah. Az-Zuhriy na Qataadah wamesema hayo hayo kama ilivyo katika Muswannaf wa Abdur-Rraaziq (1/321).([2])


3- Kugusa Msahafu
Hatuijui dalili yoyote ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kugusa Msahafu ijapokuwa Maulamaa wengi wanasema kuwa haijuzu kwa mwenye hedhi kugusa msahafu. Na haya yashaelezewa kwa urefu nyuma.


4- Mume Kusoma Qur-aan Akiwa Baina Ya Mapaja Ya Mkewe  Mwenye Hedhi
Ni kwa Hadiyth ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiisoma Qur-aan na kichwa chake kipo baina ya mapaja yangu nami niko hedhini".([3]) 


5- Kuhudhuria Swalah Za ‘Iyd Mbili
Hili halina ubaya, bali ni jambo mustahabu kwa wenye hedhi watoke ili kuhudhuria Swalah ya ‘Iyd, lakini watakaa kando ya uwanja wa Swalah.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((يخرج العواتق وذوات الخدور والحيض وليشهدن الخير ودعوة المؤمنين، ويعتزل الحيض المصلى))
((Watoke wazee wakongwe, waliotawishwa na wenye hedhi. Na waishuhudie kheri na dua za Waumini, lakini wenye hedhi wawe kando ya uwanja wa Swalah)).([4])


6- Kuingia Msikitini
Suala hili lina mvutano mkubwa kati ya Maulamaa, nalo limeshachambuliwa hapo kabla.([5])
Tunachoweza tu kusema ni kuwa sisi hatujagundua dalili yoyote sahihi na ya wazi inayomzuia mwenye hedhi kuingia Msikitini. Na asili ya jambo lolote ni uhalali mpaka liwepo la kuliharamisha. Lakini pamoja na hayo, bado tunaendelea kufanya istikhara kwa Allaahu Ta'alaa kuhusu suala hili.


7- Kulishana Na Kunyweshana Na Mumewe
Imepokelewa toka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
"Nilikuwa nikinywa huku niko hedhini, kisha nampa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala pa kinywa changukisha anakunywa. Na ninang'ata mnofu wa nyama nikiwa hedhini, kisha ninampa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye anaweka kinywa chake mahala pa kinywa changu."


8- Kumtumikia Mumewe
Ni kama kumwosha kichwa au kuchana nywele. Imepokelewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
"Nilikuwa nikimchana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nywele nami niko hedhini".


9- Kulala Na Mumewe Ndani Ya Shuka Moja
Imepokelewa toka kwa mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema:
"Wakati nikiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tumelala katika shuka, nilipata hedhi, kisha nilijichomoa nikachukua nguo yangu ya hedhi. Akaniuliza: Je, umepata hedhi? Nikamjibu: Ndio, halafu akaniita nikalala naye ndani ya qatifa".
Katika Sharh Muslim (1/954) An-Nawawiy anasema: "Inajuzu kulala  na mwenye hedhi katika blanketi moja."

([1])  Yamenukuliwa haya na Shaykh wa Uislamu katika "Al-Fataawa" (21/459).
([2]) Jaami’ Ahkaam An-Nisaa (1/174) kwa maana yake.
([3]) Imetolewa na Al-Bukhaariy (7549) na Muslim (uk. 246) na wengineo.
([4])  Imetolewa na Al-Bukhaariy katika sehemu tofauti, kati yake ni nambari (324).
([5])  Ni mwisho wa mlango wa kuoga.

0 Comments