066-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Damu Ya Nifasi (5)

DAMU YA NIFASI

Ni damu inayomtoka mwanamke kwa sababu ya kujifungua.


1- MUDA WAKE
Hakuna uchache wa muda wa kutoka kwake. Maulamaa wote([1]) wamekubaliana kuwa wakati wowote mwanamke anapoona utwahara – hata kabla ya kumalizika siku arobaini – basi ataoga, ataswali na mumewe anaweza kumwingilia.

Ama upeo wa juu zaidi wa muda anaosubiri mwanamke endapo damu ya nifasi itaendelea, Jamhuri ya Maulamaa wanaona kuwa ni siku arobaini, kisha ataoga na kuswali. Hili wamelitolea dalili kwa Hadiyth ya mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
"Wakati wa enzi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam), wanawake wenye nifasi walikuwa wakikaa siku arobaini au masiku arobaini baada ya nifasi"([2]).

2-Maulamaa wote wamekubaliana kuwa nifasi ni kama hedhi katika yote yanayohusiana na yaliyohalalishwa, yaliyoharamishwa, yaliyo makruhu na yaliyo mandubu.([3])

3- Nifasi inatofautiana na hedhi kwa kuwa eda haihesabiwi, kwani eda humalizika kwa kujifungua kabla ya kutoka damu ya nifasi.([4])


([1])  Imenukuliwa na At-Tirmidhiy katika As-Sunan (1/429).
([2]) Imetolewa na Abuu Daawuud (307), At-Tirmidhiy (139) na Ibn Maajah (648).
Wametofautiana katika kuifanya Hadiyth Hasan, lakini kauli yenye nguvu ni kuwa ni Hadiyth Dha’iyf.
Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. Lakini pamoja na hivyo, inafanyiwa kazi.
)[3](  Nayl Al-Awtwaar ya Ash-Shawkaaniy (1/386).
([4])  Al-Mughniy ya Ibn Qudaamah (1/350).

0 Comments