068-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Swalah (1)

SWALAH

FASILI YAKE
"Swalah" kilugha ina maana ya du’aa. Na Swalah ya kishari’ah imeitwa hivyo kwa vile inakusanya du’aa. Hivi ndivyo walivyosema jamhuri ya mabingwa wa lugha na wahakiki wengineo.
Allaah Mtukufu Anasema:

((وصل عليهم))
Yaani waombee([1])
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا دعي أحدكم فليجب، فإن كان صائما فليصل...))
Yaani amwombee mwalikaji chakula.([2])
Ama kiistilahi ni kumfanyia ibada Allaah Mtukufu kwa maneno na vitendo maalumu, vikifunguliwa kwa takbirah na vikimalizwa kwa tasliym, pamoja na Niyah, kwa masharti mahsusi.


CHEO CHAKE KATIKA DINI
1- Swalah ndio faradhi iliyosisitiziwa na iliyo bora zaidi baada ya shahada mbili na ni moja kati ya nguzo za Kiislamu.

Imepokelewa na Ibn 'Umar kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( بني الإسلام على خمس: شهادة أن لا إله إلا الله، وأن محمدا رسول الله، وإقام الصلاة، وإيتاء الزكاة، وصوم رمضان، والحج)).
((Uislamu umejengewa juu ya (nguzo) tano: Kushuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji)).([3])

2- Allaah Ametoa onyo kali kwa mwenye kuacha Swalah kufikia mpaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumnasibisha na ukafiri, akasema:

(( إن بين الرجل وبين الشرك والكفر: ترك الصلاة))
((Hakika baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha Swalah)).([4])

Na anasema tena:

(( العهد الذي بيننا وبينهم الصلاة، فمن تركها فقد كفر))
((Ahadi iliyopo kati yetu na kati yao ni Swalah, mwenye kuiacha, basi amekufuru)).([5])

3- Swalah ndio nguzo ya dini, na dini haisimami ila kwa nguzo hii. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((رأس الأمر الإسلام، وعموده الصلاة، وذروة سنامه الجهاد في سبيل الله)).
((Kichwa cha mambo yote ni Uislamu, nguzo yake ni Swalah, na kilele cha juu kabisa ni kufanya jihadi katika Njia ya Allaah.([6])

4- Ni kitu cha kwanza atakachofanyiwa hisabu mja. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( أول ما يحاسب عليه العبد يوم القيامة الصلاة، فإن صلحت فقد أفلح ونجح، وإن فسدت فقد خاب وخسر))
((La kwanza atakalohisabiwa mja siku ya Qiyaamah ni Swalah. Ikiwa imefaa, basi amefaulu na kufuzu. Na ikiwa imeharibika, basi amepita utupu na amekula hasara)).

5- Swalah ilikuwa ndio kitulizo cha jicho kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yake. Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
(( وجعلت قرة عيني في الصلاة))
((Na kimefanywa kitulizo cha jicho langu katika Swalah)).

6- Swalah ilikuwa ndio wasiya wa mwisho aliousia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umati wake wakati wa kufariki kwake. Alisema:
(( الصلاة، وما ملكت أيمانكم)).
((Swalah, na iliowamiliki mikono yenu ya kuume)).

7- Ni ibada pekee isiyombanduka aliyebaleghe. Humganda maisha yake yote na wala hasameheki nayo vyovyote hali iwavyo.

8- Swalah ina sifa za kipekee kulinganisha na ibada nyinginezo. Kati ya sifa hizo:

(a) Allaah Mtukufu Aliifaradhisha Yeye Mwenyewe kwa kuzungumza moja kwa moja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa Miraji.
(b) Ni faradhi iliyotajwa zaidi katika Qur-aan Tukufu.
(c) Ni ibada ya kwanza Aliyoifaradhisha Allaah Mtukufu kwa waja Wake.
(d) Imefaradhishwa mara tano mchana na usiku kinyume na ibada na nguzo nyinginezo.


VIGAWANYO VYA SWALAH
Swalah ina vigawanyo viwili. Kuna Swalah za faradhi na Swalah za Sunnah

1- Swalah Za Faradhi
Ni zile ambazo mwenye kuziacha kwa kusudi, humwasi Allaah Mtukufu. Nazo ziko aina mbili:

(a) Fardhu ‘Ayn
Nazo ni zile ambazo ni lazima kwa kila aliyebaleghe na mwenye akili, mwanamke au mwanamume, aliye huru na mtumwa. Hizi ni kama Swalah tano.
(b) Fardhu Kifaayah
Ni zile ambazo baadhi ya watu wakiziswali, basi haiwapasi wengineo. Ni kama Swalah ya maiti.

2- Swalah Za Sunnah
Ni zile ambazo mwenye kuacha kuziswali kwa kusudi, hamuasi Allaah Mtukufu. Ni kama Sunnah zilizozoeleka na nyinginezo zitakazoelezewa katika milango ijayo. Lakini imesuniwa kuziswali Swalah za Sunnah, na kuziacha ni makruhu.
 
([1]) "Mawaaahib Al-Jaliyl" (1/277), "Al-Majmuu" (3/3/) na "KashShaaf Al-Qinaa"(1/122).
([2])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (1431) na itakuja.
([3])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al Bukhaariy (8) na Muslim (16).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (987), Abuu Daawuud (1658), An-Nasaaiy (1/231) na wengineo.
([5])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na At Tirmidhiy (2621), An Nasaaiy (1/231) Ibn Maajah (1079).
([6]) Imetolewa na At Tirmidhiy (2616) na Ibn Maajah (3973).

0 Comments