07 - Taratibu Za Kupata Hoja Kutoka Kwenye Vyanzo

Ama kwa Quraan…

Qur-aan ilisomwa na kueleweka kwa Swahaaba bila ya wao kuhitaji msaada wa kuhitaji kukimbilia katika kanuni rasmi za sarufi. Vile vile, wamejaaliwa kuwa na muoni ulio msafi, akili za uwerevu na zilizo makini. Walikuwa na uwepesi wa kufahamu malengo ya Mtoa Sheria (Allaah) na hekima zilizomo ndani ya Sheria Zake.

Hakika ni mara chache Maswahaba walikuwa wakimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na jambo lolote isipokuwa yeye mwenyewe alitaje kwanza.

Imesimuliwa kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema “Sijapata kuona watu bora kuliko Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kupitia kipindi cha kazi yake, mpaka alipofariki. Wamemuuliza kuhusiana na mambo kumi na tatu, yote ambayo yametajwa ndani ya Qur-aan. Kwa mfano [maana ya]:
“Wanakuuliza (hukumu ya) kupigana vita katika miezi mitakatifu…” [2:217)
na “Wanakuuliza juu ya hedhi….” (2:222)”

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema, “Walikuwa wakimuuliza yeye kwa mambo ambayo yalikuwa na azma ya uhakika kwao[1].”

Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwa hili alisema: “Usiulize kwa jambo ambalo halikutokezea, kwani mimi nimemsikia baba yangu ‘Umar Ibn al-Khattwaab akisema: Mlaani yule aliyeuliza jambo ambalo halikutokezea.[2]

Qaasim (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema (kukiambia kizazi cha tatu cha Waislamu): “Munauliza kuhusu vitu tusivyowahi kuuliza, na kugombana kuhusu vitu ambavyo hatujawahi kugombana navyo. Hata munauliza kuhusu vitu ambavyo mimi sina maarifa navyo. Lakini kama tutajua, haitoruhusiwa kwetu kubakia kimya kuhusiana navyo[3].”

Ibn Is-haaq (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Nimekutana na zaidi ya Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko mtu mwengine yeyote, na sijapata kuwaona watu walioishi maisha ya kawaida au ambao ni wachache wa kudai juu yao wenyewe[4].”

‘Ubaadah bin Nusay al-Kindi (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Nimejuana na watu ambao ugumu wao haukuwa imara kama wa kwenu, na masuala yao yalikuwa kimya tofauti na yale munayouliza nyinyi[5].”

Abu ‘Ubaydah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema ndani ya kitabu chake cha Majaaz al Qur-aan: “Haikuwahi kusimuliwa kwamba Swahaabah yeyote alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa elimu yoyote ambayo inawezekana kupatikana ndani ya Qur-aan[6].”


Ama kuhusu Sunnah…

Sehemu ya Sunnah ambazo zina lafudhi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa ndani ya lugha za Maswahaba, hivyo walitambua maana zake na kuelewa maneno yaliyomo ndani ya aya (phrase) na yale maneno mengineo ambayo hudhihirisha maana yake (context).

Namna ulivyo mwenendo wa Mtume, waliweza kushuhudia (huo mwenendo), baadaye kuwaambia wengine vile vile kama walivyoona. Kwa mfano, mamia ya watu walimuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya wudhuu na wao kufuata mwenendo wake bila ya kumuuliza kutaka maelezo. Kama baadhi ya vitendo kwenye wudhuu yalikuwa ni lazima na vyengine kupendekezwa, ambavyo kwa uwazi vimeruhusiwa na vyengine havikutajwa. Vivyo hivyo, walishuhudia (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya Hijjah na Swalah, na vitendo vyengine vya ibada.

Watu walisikika wakimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa Fataawakuhusiana na masuala tofauti, na alifanya hivyo. Kesi zilipelekwa kwake, na yeye alitamka hukumu. Matatizo yatatokea miongoni mwa Maswahaba, na yeye alitoa jibu la hakika. Aidha matatizo hayo yalihusiana na mahusiano ya pamoja, tabia binafsi, au masuala tofauti ya kisiasa. Walishuhudia mazingira yote haya na walifahamu maana (ya mazingira yaliyotokea). Ili kwamba hekima na malengo ya hukumu za Mtume zisifichwe mbali nao.

Watu walimuona namna Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiona tabia za Maswahaba wake na wengineo. Hivyo, kama yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsifu yeyote, walitambua ya kwamba tendo la huyo mtu lilikuwa ni zuri, na kamaatamlaumu yeyote, walitambua kwamba kuna kosa fulani kwa namna huyo mtu alivyofanya.

Juu ya hivyo, simulizi zote kuhusiana na Fataawa za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), maamuzi na kukubali au kutokubali baadhi ya masuala inaonesha kwamba yalitokea mbele ya watu wengi. Ni kama mfano wa anavyotambua daktari na wenziwe, kutokana na mjumuiko wa muda mrefu na kutambua wenyewe mazoea[7] sababu za yeye kuelekeza dawa fulani. Hivyo, hata Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walitambua hakika sababu na hekima zilizomo ndani ya maamuzi yake.


Ama kwa Ijtihaad…

Maelekezo ya kwamba Ijtihaad inaruhusika na inafaa kwa matumizi ya misamiati ya leo ni mengi. Kwa mfano, Mu’adh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaeleza kwamba wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipompeleka Yemen, aliuliza:

“Utafanya nini kama suala limeletwa mbele yako kwa hukumu?” Mu’adh akasema: “Nitahukumu kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah” Mtume akauliza: “Kama hukupata suluhisho ndani ya Kitabu cha Allaah?” Mu’adh akasema: “Basi nitahukumu kwa Sunnah ya Mtume.” Mtume akauliza: “Na kamahukupata kitu ndani ya Sunnah ya Mtume?” Mu’adh akasema: “Basi nitafanya Ijtihaad kutengeneza hukumu yangu mwenyewe.” Mtume alikipiga piga kifua cha Mu’adh na akasema: “Sifa zote ni za Allaah Ambaye Amemuongoza mjumbe wake kwa lile ambalo linamfurahisha Yeye na Mtume Wake[8].”

Ijtihaad hii na kutumia hukumu yake mtu mwenyewe kama ilivyotajwa na Mu’adh, pia inaelezwa katika ushauri wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliompa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomteua kama ni Jaji: “Hukumu itolewe kwa mujibu wa maelezo ya shurti za Qur-aan au mwenendo uliowekwa na Sunnah…” Kisha akaongeza:

“Hakikisha unaelewa vizuri kila kesi ambayo imeletwa kwako ambayo hamna maandiko yanayohusiana nayo kutoka kwenye Qur-aan au Sunnah. Kwako, baadaye, ni jukumu la kuoanisha na kufananisha, ili kutofautisha mifano kwa lengo la kufikia hukumu ambayo ipo karibu na uadilifu na bora mbele ya Allaah[9].”

Hapo hapo, al-Imaam ash-Shafi’iy ameeleza “rai” kama ni maana ya Ijtihaad na Ijtihaad kama nial-Qiyaas. Amesema “Hayo ni majina mawili kwa kitu kimoja[10].”

Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), Khaliyfat Rasuul Allaah, amesema: “Namna Mtume alivyo, rai zake daima zilikuwa ni sahihi kwa sababu Allaah daima Akimuongoza. Ama katika kesi yetu, tunadhania na tunakisia.[11]

Hivyo, tunaweza kusema kwamba dhana ya Ijtihaad au “rai”, kwenye kipindi hicho, haikwenda mbali zaidi ya moja zifuatazo:

a)    Kutumia maana moja au nyingine zinazowezekana katika kesi ambapo hukumu inaweza kujikubali yenyewe katika tafsiri zaidi ya moja. Mfano, pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaamrisha Waislamu kuswali sehemu ya Banu Quraydhwah[12].
b)   Mlinganyo, Qiyaas, ambayo inahusu suala kwa kulifananisha na jengine, pia suala hilolinazungumzwa ndani ya Qur-aan au Sunnah. Kwa mfano Qiyaas ya ‘Ammaar aliyepambanisha kesi ya Tayammum akiwa katika hali ya Janaabah kwa Ghusl, na hivyo kupangusa (kujisiriba) mwili wake wote kwa vumbi[13].
c)     Ijtihaad ya kutia maanani kitu ambacho kinawezekana kuwa na manufaa au kuzuia kitu ambacho kinaweza kupelekea kwenye ubaya, au kuchukua uamuzi fulani kutoka kwenye matamko ya jumla, au kutumia tafsiri maalum, na mengineyo zaidi.

Bidii ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwahamasisha Maswahaba kufanya Ijtihaad na kuwafundisha katika matumizi yake inaweza kuonekana kwenye maneno ya Hadiyth hii:
“Hakimu anapofanya Ijtihaad na kufikia kwenye hukumu sahihi, anapata ujira mara mbili, na kama hitimisho lake si sahihi, pia anapata ujira mmoja.[14]

Ijtihaad ya Maswahaba wengi ilikuwa ni makini na kwamba kwenye kesi nyingi, uteremsho wa Qur-aan ulihakikisha huo umakini. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikubali. Bila ya shaka, ukaribu wao na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ulitosheleza wepesi wa kutambua malengo ya Mwingi wa Busara na Mtunga sheria, madhumuni makuu yaliyo ndani ya Sheria za Qur-aan, na maana ya maandiko. Nafasi ambayo waliokuja baada yao hawakufaidi moja kwa moja.


[1] Angalia ‘Abdullaah Ibn ‘Abdur-Rahmaan ad-Daarimiy, Sunan, I, uk. 51.
[2] Ad-Daarimiy, Sunan, I, uk. 50.
[3] Ad-Daarimiy, Sunan, I, uk. 49.
[4] Ad-Daarimiy, Sunan, I, uk. 51
[5] Ad-Daarimiy, Sunan, I, uk. 51
[6] Imenukuliwa na Shaykh ‘Aliy Abdur-Razzaq ndani ya Tamhiyd li Taariykh al-FalsafahCairouk. 152.
[7] Ad-Dahlawiy: HujajatuLlaah al-Baalighah, (Misri), I, uk. 289.
[8] Kwa maelezo kuhusiana na usahihi wa kunukuu Hadiyth kama ushahidi, angalia waandishi, Al-Ijtihaad wa at-Taqliyd, (Cairo, Dar al Ansar), uk. 23-24, na sura kuhusiana na Ijtihaad kitabu cha Al-Mahswuul.
[9] Angalia Ibn Qayyim, I’laam al-Muwaqqi’iyn
[10] Angalia al Imam ash-Shaafi’iy, Ar-Risaalah, (Cairo), uk. 476
[11] Ibn Qayyim, I’laam al-Muwaqqi’iyn, I, uk. 54, Ibn ‘Abd al-Basr, Jami’ Bayaan al ‘ilm, II, uk. 134.
[12] Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha kundi la Waislamu pamoja na maelekezo: “Simamisheni Swalah ya Laasiri sehemu ya Banu Quraydhwah.” Wakitoa tafsiri yao kuhusiana na hili, kundi moja la Waislamu ndani ya kundi wakaendelea na safari yao mpaka jua lilipozama (machweo), bila ya kusimama kwa ajili ya Swalah ya Laasiri kwa wakati wake. Hata hivyo, kundi la pili waligandia kufuata nafsi zao kuliko maagizo ya Mtume, walisimama mbali kidogo kabla ya sehemu ya Banu Quraydhwah ili kuweza kutekeleza Swalah katika wakati wake. Alipofahamishwa walivyofanya kuhusu kila kundi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kwamba wote walikuwa sahihi.
[13] Hadiyth ni maarufu na ni sahihi, na iliingizwa ndani ya vitabu vya Imaam al-Bukhaariy, Abu Dawud, al-Nasaaiy, Ibn Maajah, na Ahmad katika mkusanyiko wa Hadiyth.
[14] Hadiyth hii ni ya maana na ilipokewa na al-Bukhaariy, Muslim, na wengineo katika mkusanyiko wao wa Hadiyth sahihi.

0 Comments