19 - Taratibu Za Imaam Ash-Shaafi'iy Kwenye Kitabu Chake 'Ar-Risaalah'

TARATIBU ZA IMAAM ASH-SHAAFI'IY KWENYE KITABU CHAKE: AR-RISAALAH
Al-Imaam ash-Shaafi’iy alianza kitabu chake kwa kutanabahisha hali ya binaadamu kabla tu ya ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa kufanya hivyo, aliwagawa kwenye makundi mawili:-


 1. Ahl al-Kitaab “Watu wa Kitabu”; au, wafuasi wa uteremsho wa mwanzo ambao wamebadili maandiko yao na kuharibu pamoja na baadhi ya amri za kisheria. Kiuhalisia, watu hawa wameingia kwenye ukafiri na wengi wao baadaye kujaribu kuchanganya na Ukweli Aliouteremsha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
 2. Washirikina na Makafiri walioabudia masanamu badala ya Allaah.

Baadaye al-Imaam ash-Shaafi’iy alisema kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amewaokoa wanaadamu wote kwa kumleta wa Mwisho katika Mitume, na kumshushia Kitabu Chake, ili kwamba huenda wakapokea kupitia kwake, njia ya kuondokana na upofu wa ukafiri kwenda nuru ya uongofu:

{{Kwa hakika wale wanaoyakanusha mawaidha yanapowajia (Tutawaadhibu). Bila shaka hicho ni Kitabu kihishimiwacho.

Haitofikia batili (Kitabu hichi) toka mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hikima, Ahimidiwaye}} [41:41-42]

Baadaye al-Imaam ash-Shaafi’iy aliendelea kujadili kwa undani hadhi ya
Qur-aan ndani ya Uislamu na matamko yake mengi kuhusu nini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameruhusu na kuzuia, vipi mwanaadamu amuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), malipo ya wale wenye kumtii Yeye; adhabu kwa wale Wanaomtii Yeye na namna Alivyowaangamiza kwa kuwapa habari za waliotangulia.

Baadaye, al-Imaam ash-Shaafi’iy alieleza kwamba wanafunzi wanaotafuta elimu ya Kiislamu wajifunze mengi ndani ya Qur-aan na sayansi zake, kadri watakavyoweza; na kwamba pale nia zao zitakapokuwa safi, kwa pamoja wanaweza kunukuu aya zake na kufahamu maana yake kutokana nazo.

Mwisho wa utangulizi wake wa ar-Risaalah, al-Imaam ash-Shaafi’iy alisema: “Hakuna tatizo litakalomshambulia miongoni mwa wafuasi wa Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) isipokuwa kwamba kutakuwa na muongozo ndani ya Kitabu cha Allaah kuonesha njia sahihi. Kwani, Allaah, Mtukufu Aliye Bora, Amesema:

{{Kitabu Tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu katika giza uwapeleke katika nuru, kwa idhini ya Mola wao, uwafikirishe katika njia ya yule Mwenye kushinda (na) Mwenye kusifika (Naye ni Mwenyezi Mungu)}} [14:1]

Na pia Amesema:

{{(Tuliwaleta) Kwa Ishara zilizo wazi na kwa Vitabu. Na Tumekuteremshia mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri}} [16:44]

Na pia Amesema:

{{Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anaamrisha uadilifu, na kufanya ihsani, na kuwapa jamaa (na wengineo); na Anakataza uchafu na uovu, na dhulma. Anakunasihini ili mupate kufahamu (mfuate).}} [16:90]

Na:

{{Na namna hivi Tumekufunulia Wahyi kwa amri Yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini wala imani; lakini Tumefanya Kitabu hiki (Qur-aan) ni nuru, ambayo kwa (nuru) hiyo Tunamwongoza Tumtakaye katika waja Wetu. Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia iliyonyooka.}} [42:52]

Baadaye inafuatia Sura kuhusu al-Bayaan[53] ambapo neno hili linatafsiriwa kama ni neno la kisheria, na baadaye likagaiwa kwenye mafungu, kwenye kueleza katika njia ambazo uteremsho wa Qur-aan linamaanisha masuala yenye mnasaba wa kisheria. Mafungu hayo yapo matano:

1)     Yale ambayo Allaah Ametolea maamuzi kama ni kifungu cha sheria mahsusi kisichohitaji maana nyengine zaidi ya tafsiri yake halisi (literal). Fungu hili la al-Bayaan halihitaji ufafanuzi mwengine zaidi ya Qur-aan wenyewe.
2)     Yale ambayo inayataja Qur-aan ambayo yanaweza kutolewa maana katika njia tofauti, na yale ambayo Sunnah imetoa maelezo ya kuweka wazi, ipi iliyokusudiwa.
3)     Yale ambayo yameelezwa bayana kuwa yana ulazima, na yale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ameeleza kwa matamshi ya vipi, kwanini, ni juu ya nani, na wapi kutumika na wapi kutotumika.
4)     Yale ambayo yameelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini hayakutajwa ndani ya Qur-aan. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameamrisha ndani ya Qur-aan kwamba atiiwe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na amri zake zikubaliwe. Hivyo yanayotamkwa kutoka mamlaka ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yanatambulika kuwa ni mamlaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
5)     Yale ambayo yanahitaji viumbe Wake kutafuta kupitia Ijtihaad. Hii ni Qiyaas. Kwa mujibu wa al-Imaam ash-Shaafi’iy, Qiyaas ni utaratibu wa kufikia ufumbuzi wa kisheria kwa msingi wa ushahidi (hukumu zilizowahi kutolewa kabla na kukubaliwa) ambapo hutumika hoja maarufu au sababu inayofaa.

Al-Imaam ash-Shaafi’iy kisha aliendelea kuelezea mafungu haya matano kwenye sura tano tofauti, akitoa mifano na ushahidi wa kila moja. Hivyo, ar-Risaalah hiyo ilikuwa na sura zifuatazo:-

 • Aya za Jumla zilizoteremshwa ndani ya Qur-aan zinakusudiwa kuwa na mambo ya ujumla‘Aam, lakini yamo pia Mahsusi Khaasw.
 • Aya za Jumla zilizo Wazi za Qur-aan ambazo zinaonesha kuwa ni Jumla lakini zinadhamiriwa kuwa Mahsusi moja kwa moja.
 • Fungu la al-Bayaan ndani ya Qur-aan kwa utaratibu ambao maana inadhihirishwa kwa kutumia maneno au aya nyengine.
 • Fungu la al-Bayaan ndani ya Qur-aan kwa utaratibu wa maneno, ambao unaonesha zaidi maana iliyofichikana al-Baatwin kuliko maana iliyo wazi adh-Dhwaahir.
 • Yale, ambayo Qur-aan yaliteremshwa kama ni Jumla lakini Sunnah ikatanabahisha kuwa yana maana Mahsusi.

Katika Sura iliyotajwa hapo juu, al-Imaam ash-Shaafi’iy alieleza uhalali wa Sunnah kama ni ushahidi na hadhi yake ndani ya dini. Kwa sababu hii, baadaye alihitimisha sura zifuatazo:-

 • Wajibu uliowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ndani ya Qur-aan kufuata Sunnah ya Mtume Wake.
 • Amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akiamrisha utiifu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yote yanajumuisha kuwa ni utiifu Kwake na amri zilizotolewa zenye kujitegemea.
 • Masuala ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameamrisha utiifu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
 • Namna Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alivyoweka wazi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelazimika kufuata yale yaliyoteremshwa kwake na kutii chochote atakachoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), na kwamba Allaah Atamuongoza yeyote anayemfuata Yeye.

Ndani ya Sura hii, al-Imaam ash-Shaafi’iy amethibitisha kwamba sehemu ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimejadiliwa na kuhusishwa na Qur-aan, wakati sehemu nyengine zimeeleza masuala yaliyohusika, ambayo hakuna maandiko yanayonasibiana nayo ndani ya Kitabu. Al-Imaam ash-Shaafi’iy pia ameonesha kwamba Sunnah ipo huru na Qur-aan, na kunukuu ushahidi ili kuwakosoa wale ambao hawakubaliani naye kwenye suala hilo. Kisha akasema: “Nitafafanua yale ambayo nimekwisha yaeleza kuhusu Sunnah, (kama) ni sehemu ya Qur-aan au sheria nyengine kwa mambo ambayo hayakubainishwa humu, pia hili litapambanua yale niliyojadili hapo juu, Allaah Akipenda. Kwanza, nitazungumzia Sunnah kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah, kwa kutumia, njia ya kurasa za Qur-aan zenye kutengua al-Naasikh na kutenguliwa al-Mansuukh. Baada ya hapo, nitabainisha Fardh-wajibu (ndani ya Qur-aan) na kwa mnasaba wake Sunnah; Fardh-wajibu zilizotolewa kwa maneno ya Jumla ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya Mahsusi kupitia kwake kufafanua maelezo kuhusiana na vipi na wapi; maandiko ya Jumla ambayo yalikusudiwa kueleweka kama ni Jumla, na maandiko ya Jumla ambayo yalikusudiwa kueleweka kama ni Mahsusi, na mwisho; Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo hakuna maandiko ya juu kutoka Kitabu cha Allaah.”

Baadaye inafuata sura iliyoitwa, “Asili ya Kutengua na Kutenguliwa”; ambayo inaeleza kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametumia utenguzi kuifanya (Shariah) nyepesi na yenye kubadilika zaidi. Sura hii pia inabainisha kwamba aya ya Qur-aan inaweza tu kutenguliwa kwa aya nyengine ya Qur-aan; na kwamba Sunnah inaweza tu kutenguliwa kwa Sunnah nyengine.

Kisha akajadili kwa pamoja; kutengua na kutenguliwa. Ambazo zinabainishwa ndani ya sehemu ya Qur-aan, na ndani ya sehemu ya Sunnah.

Baada ya hapo inabainishwa kuhusu Fardh-wajibu wa Swalaah na maelezo ndani ya Qur-aan na Sunnah kuhusiana na wale ambao wanaweza kuwa na udhuru wa kutoiswali, na wale ambaoSwalaah haikubaliki kwa sababu ya kitendo kiovu ambacho huenda wamekitenda.

Kisha, al-Imaam ash-Shaafi’iy ameandika Kutengua na Kutenguliwa ambazo zinatajwa ndani ya Sunnah na al-Ijmaa’,

 • Zile za Fardh-wajibu ambazo Allaah Ameziweka ndani ya maandiko ya Qur-aan.
 • Zile za Fardh-wajibu zilizowekwa ndani ya maandiko ya Qur-aan ambapo pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amezijadili ndani ya Sunnah.
 • Zile Fardh-wajibu zilizowekwa ndani ya maandiko ya Qur-aan ambapo Sunnah imebainishwa kuwa zilikusudiwa kutumika Mahsusi.
 • Zile Fardh-Wajibu kwa jumla zilizo wazi na kukusudiwa kuwa ni lazima, na ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa maelezo ya namna ya kuzitekeleza, mfano SwalaahHajjZakaah, idadi ya wake, mwanamke ambaye haruhusiki kuolewa, na kizuizi cha mlo wa siku (dietary).

Kwenye sura inayofuata, amejadili kuhusu dosari ndani ya Hadiyth, na kueleza kwamba mgongano baina ya Hadiyth unaweza kutokea kwa sababu zilizo nyingi. Ameendelea kueleza baadhi ya sababu hizi. Kwa mfano, mgongano unaweza kutokea kwa sababu Hadiyth moja imetenguliwa na nyengine, au kwa sababu ya makosa yaliyotokea ndani ya upokezi wa Hadiyth hiyo. Ameelezea makosa ambayo huenda yamesababisha migongano ndani ya Hadiyth, na sababu nyenginezo nyingi zilizopelekea migongano kama hiyo. Kisha amezungumzia aina tofauti za uzuiaji, na kueleza kwamba baadhi ya Hadiyth zinabainisha nyengine.

Al-Imaam ash-Shaafi’iy pia ameweka sura kuhusu elimu, na kueleza kwamba kuna aina mbili za elimu. Ya kwanza; ni aina ya elimu maarufu ambayo hakuna uwezekano wa kutoifahamu kwa mtu mzima na mwenye akili timamu. Elimu yote ya aina hii inawezekana kupatikana na kutajwa ndani ya maandiko ya Qur-aan, na kila Muislamu anaelewa yote hayo kwa sababu imeteremshwa kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kila kizazi kilchotangulia. Hakuna (mjadala) kuhusiana na usahihi wa elimu hii, na wote wanakubali kwamba ni lazima. Hakika, asili ya elimu hii ni kwamba, hakuna uwezekanao wa kuwepo makosa katika kufika kwake au kutafsiri.

Aina ya pili ya elimu ni ya maelezo yanayotokana na mzizi wa ulazima, na sheria mahsusi zinazotokana nazo. Hizi hazijatajwa ndani ya maandiko ya Qur-aan, na nyingi katika hizo hazitajwi ndani ya maandiko ya Sunnah achilia mbali kutokana na mapokezi ya mmoja-pekee, Ahad.

Hivyo, al-Imaam ash-Shaafi’iy ametoa utangulizi wa somo jipya, upokezi wa mmoja-pekee, Khabar al-Waahid. Al-Imaam ash-Shaafi’iy baadaye akaeleza nini kinachokusudiwa kwa neno hili, na masharti ambayo yataitambua kama ni upokezi au sio upokezi wa aina ya mmoja-pekee. Tofauti baina ya kiapo na habari, Shahaadah na Riwaayah, imeelezwa. Ama kwa masuala ambayo yanaweza kukubalika kupitia upokezi wa mmoja-pekee, na kwa zile ambazo Khabar al-Waahidhaitoshi peke yake.

Baadaye, al-Imaam ash-Shaafi’iy amejadili hadhi ya Khabar al-Waahid, na kama habari hizo zinaweza kutumika kama ni ushahidi. Hitimisho lake, linakubalika kwa hoja zilizo nzuri na makini, ni kwamba; hakika zinaweza kutumika. Hivyo, al-Imaam ash-Shaafi’iy ametangulia katika kufuta mashaka yote yaliyokuzwa na wanaompinga kwenye suala hili.

Sura zifuatazo zinafuatia:-

 • Kuhusu al-Ijmaa’. Maana yake, na nafasi yake kisheria.
 • Kuhusu al-Qiyaas. Maana yake na asili, kuhitajia kwake, aina ya Qiyaas, na nani mwenye na asiye na uwezo wa kuitumia.
 • Kuhusu Ijtihaad: Kwanza namna ilivyoegemezwa kwenye Qur-aan, na baadaye kwenye Sunnah, (sura) inahusisha Ijtihaad sahihi na isiyo sahihi.
 • Kuhusu Istihsaan; Hiari ya Mwanachuoni: ash-Shaafi’iy alikuwa ni mwangalifu kueleza kwamba Muislamu yeyote haruhusiwi kuitumia al-Istihsaan kwa lengo la kuingilia/kukosoa Hadiyth, wala hakujaribu kutamka hukumu yeyote ya kisheria isiyoegemezwa kwenye Qur-aan, Sunnah, al-Ijmaa’ na al-Qiyaas. Pia alielezea tofauti baina ya al-Qiyaas na al-Istihsaan.
 • Kuhusu kutokubaliana miongoni mwa Wanazuoni: al-Imaam ash-Shaafi’iy ameeleza kwamba, kutokubaliana huku ni katika aina mbili; aina ambayo zinazuiwa na zile zisizozuiwa.

Aina ya kutokubaliana ambazo haziruhusiwi na zile kuhusiana na masuala ambayo Allaah Ametoa ushahidi ulio wazi ndani ya maandiko ya Qur-aan au Sunnah. Kutokubalina kwa aina ambazo zinaruhusiwa, inahusiana na masuala ambayo yanaweza kutafsiriwa kwa kutumia njia tofauti na zile ambazo kila mwanazuoni anatumia aina yake ya kutoa hoja. Al-Imaam ash-Shaafi’iy kisha akatoa mfano wa aina zote, ametoa mifano ya masuala ambayo Maswahaba hawakukubaliana, kama vile ‘Iddah, viapo na mirathi. Ndani ya sura hii, al-Imaam ash-Shaafi’iy ametaja kitu kuhusiana na utaratibu wa kutumika hiari kwa maoni ya Maswahaba pale wanapohitalifiana.

Ar-Risaalah inahitimishwa kwa ufafanuzi wa mawazo ya ash-Shaafi’iy kwenye “mafungu ya ushahidi” yaliyoelezwa hapo juu.

“Tunaegemeza hukumu zetu kimsingi kwenye Qur-aan na Sunnah iliyokubaliwa kuhusiana na yale ambayo hayana mgogoro, nasema: “Hii ndio hukumu yetu baada ya kusoma kwa pamoja maana zilizo wazi na zilizofichikana ndani ya maandiko.” Baadyae, kama inatubidi tunukuu kwenye Sunnah ambayo imesimuliwa na baadhi tu ya watu wachache na kuhusiana na ile ambayo hakuna makubaliano, tunasema: “Tunaikubali Hadiyth kama ilivyo, lakini tupo makini kwamba yawezekana kuwepo makosa yaliyofichikana ndani ya wasimuliaji.” Baadaye, tutanukuu kwenye al-Ijmaa’ kisha kwenye al-QiyaasQiyaas ni dhaifu kuliko Ijmaa’ na inatumika pale tu inapohitajika, kwasababu sio halali kuitumia al-Qiyaas wakati kuna mapokezi kuhusiana na suala linalojadiliwa.”

Kutoka kwenye maandiko ya al-Imaam ash-Shaafi’iy, tunatambua vyanzo vya Maarifa ya Sheria za Kiislamu yalivyokubaliwa, na vile ambavyo vilisababisha kutokubaliana kwa wakati huo.

Vyanzo ambavyo vilikubaliwa vilikuwa ni: Kwa ujumla ni Qur-aan na Sunnah.

Vyanzo ambavyo vilihusiana na kutokubaliana vinajumuisha Sunnah yote kwa pamoja, na baadhi ya mapokezi Khabar al-Waahid (ambayo al-Imaam ash-Shaafi’iy ameitaja kama ni al-Khaaswah) mahsusi. Lakini mchango wa al-Imaam ash-Shaafi’iy ulikuwa kwamba, alichunguza masuala haya mawili kwa pamoja ndani ya ar-Risaalah na ndani ya Jima’ al-‘Ilm.

Masuala mengine ambayo yalihusiana na kutokubaliana yalikuwa ni:-

1.     Al-Ijmaa’: Kulikuwepo kutokubaliana kuhusiana na uhalali wa matumizi yake kama ni ushahidi kuhusiana na aina tofauti za al-Ijmaa’Ijmaa’ ya nani ikubalike kama ushahidi, masuala ambayoal-Ijmaa’ inaweza kutambulika kama ni ushahidi; na namna jamii inavyoweza kutanabahishwa kwamba kuna Ijmaa’ kwenye suala mahsusi.
2.     Al-Qiyaas na al-Istihsaan: Kulikuwa na mgogoro kuhusiana na maana ya tafsiri hizo, asili yake, uhalali wa matumizi yake kama ni sheria, uwezekano na utaratibu wa kuzitumia, na ama vitendo vya Maswahaba vinaweza kutambulika kama ni Qiyaas au Istihsaan.
3.     Pia kulikuwa na kutokubaliana kulikokuwa bayana kuhusiana na uhalisi wa amri za Qur-aan na uzuiaji, maana zake na athari zake kwenye kanuni nyengine, hukumu za Fiqh. Tunaweza kutambua kwamba katika kipindi hichi, Maimamu Wanne wa Sunni hawakutumia maana ya maneno yaliyojifunga kama vile Tahriym “uzuiaji”, al-Ijaab “uwajibu”, n.k. Kwani maneno haya hayakutumika kwenye misamiati yao. Isipokuwa aina hii ya maneno ya kisheria yalijitokeza baadaye, kama Ibn Qayyim alivyoeleza.[54]
4.     Vyanzo vyengine vya Maarifa ya Sheria za Kiislamu ambavyo vina tofauti, (ilikuwa) ni mara chache kujadiliwa kwenye kipindi cha wanazuoni wa mwanzo. Kwa mfano, kama maneno ya al-‘Urf,al-‘Aadah na al-Istis-haab yalikuwa sio sehemu ya misamiati yao.
[53] Ndani ya utangulizi wa tafsiri ya ar-Risaalah, Profesa Maajid Khadduuri anajadili maana ya al-Bayaan, na kunukuu tafsiri zilizotolewa na wanazuoni wa kuheshimika. Profesa Khadduuri ameandika:-

“Wengine wanasema, ina maana tu ya uteremsho unaojumuisha vifungu vya kisheria: Wengine wanajadili kwamba sio tu ni uteremsho, lakini pia kuwaweka wazi. Ash-Shaafi’iy, hata hivyo, anaonekana kutilia mkazo maudhui ya kisheria ya vifungu kwa hoja za kwamba mawasiliano yote ya Qur-aan yapo wazi, ‘ingawa baadhi yake yapo kwa ukali kuliko mengine’ na kwa wale tu wasiojua lugha ya Kiarabu yanakuwa baadhi ya mawasiliano yanaonekana kuwa hayapo wazi kuliko mengine.”

Kiuhakika, neno al-Bayaan linatafsiriwa na Profesa Khadduuri kama “uteremsho ulio bayana”. Angalia, Khadduuri, Islamic Jurisprudence (Maarifa ya Sheria za Kiislamu), Iliyochapishwa na Johns Hopkins Press, uk. 32-33.
[54] Ibn Qayyim, I’laam al-Muwaqqiy’in, I, uk.32.

0 Comments