22 - Uswuul Al-Fiqhi Sura Ya Sita Na Ya Mwisho - Mada Zinazohusiana Na Ijtihaad

SURA YA SITA

MADA ZINAZOHUSIANA NA IJTIHAAD

Kiuhalisi, mada ya Ijtihaad ilichukua sura nzima ya kitabu cha al-Uswuul. Ndani ya sura hiyo, mwandishi (anatakiwa) aanze kwa kujadilii kuhusu Ijtihaad kwa kuitolea tafsiri, kuelezea masharti ya kutumika, na kuitofautisha baina ya aina tofauti za Ijtihaad. Hivyo, atajadili kama ndio au sivyo namna Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoitumia Ijtihaad kuwa ni muundo wa kuabudu ‘Ibaadah, kama ikiwa ilitumika au haikutumika na Swahaabah kuwa ni muundo wa‘Ibaadah wakati wa maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama ikiwa jibu moja tu linalotokana na Ijtihaad kwenye suala lolote linaweza kuwa sahihi, au kama inawezekana kuwepo majibu tofauti yaliyo sahihi, na pale Ijtihaad iliporuhusiwa na isiporuhusiwa. Baadaye, wanazuoni walijadili kuhusiana na mada ya Taqliyd kwa mtindo huo huo.

Mnamo karne ya nane Hijriyah, Ibraahiym bin Muusa ash-Shaatwibiy (Amefariki mwaka 790 H) aliandika al-Muwaafaqaat “Upatano”, ambacho alizungumzia kuhusu Ijtihaad kwa mnasaba wa kuwa ni zoezi la kitaalamu katika nguzo mbili. Nguzo ya kwanza ilikuwa ni elimu iliyokamilika ya sarufi na elimu ya kupanga maneno kwa sarufi ya lugha ya Kiarabu. Aliacha somo hili kwa wanazuoni wa lugha ya Kiarabu na waandishi wengine wa al-Uswuul. Nguzo ya pili ya Ijtihaad, kwa mawazo ya ash-Shaatwibiy, ilikuwa ni elimu ya malengo ya Sheria ya Aliyekuwa Mbora wa Hekima na Mtungasheria.

Waliomtangulia ash-Shwaatibiy kwenye uwanja wa al-Uswuul hawakupata kuweka maanani sana kwenye malengo haya. Isipokuwa, kikubwa walichokifanya kwenye mwelekeo huu ulikuwa ni kutafuta sababu kuu ‘Illah. Kwa upande mwengine, ash-Shaatwibiy, aliandika kitabu chake kwa lengo la kujadili kuhusiana na jambo hili muhimu. Hakika, elimu ya malengo Maqaaswid ya Shari’ah ni muhimu kwa ajili ya kuelewa Sheria ya Mtungasheria. Hata hivyo, wanazuoni wa al-Uswuul hawakupatapo kukipa kitabu hicho hadhi yake inayotakikana. Hili linawezekana kuelezwa kwa dhana iliyojengeka ndani ya akili za wanazuoni wengi kwamba hairuhusu (kuchunguza) sababu za sheria ya Mtukufu, sababu ambayo ni kwamba kuchunguza huko, hakuwezi kufanywa au kupatikana umakini.[70]Inapokuwa kesi hii, au kuendelea mbele kwa hoja za wanazuoni wengi wakubwa, somo la masuala hayo ni madogo mno kuliko mahitaji ya faragha asiyohitaji mwanazuoni.

Hata hivyo, kitabu cha ash-Shaatwibiy kipo kwenye chapa na kinapatikana sehemu kadhaa, na tunaweza tu kutaraji kwamba walimu wa al-Uswuul na wale wenye jukumu la kuweka mtaala watawaongoza wanafunzi wao kwa kuwaweka kitako kwenye kazi hii muhimu, haswa kwa wale wanaosoma al-Qiyaasat-Ta’lil na Ijtihaad. Wakati wetu, wanazuoni wakuu wawili, Ibn ‘Ashuur na ‘Allaal al-Fasi wameandika kwenye somo la malengo ya Shari’ah.

Ibn Hammaam (Amefariki mwaka 861 H), ameandika at-Tahriyr “Uhariri” na mwanafunzi wake, Ibn ‘Aamir al-Hajj (Amefariki mwaka 879 H) ameiandikia ufafanuzi yenye jina la at-Taqriyr wa at-Tahbiyr. Vyote vipo kwenye chapa. At-Tahriyr ni, moja kati ya vitabu vilivyoandikwa kwa kuchanganya mtindo wa Hanafiyyah na Mutakallimuun. Kuna fafanuzi nyengine, iliyoandikwa na Amr Badshah, yenye jina la Taysiyr at-Tahriyr “Kuwepesisha Uhariri”

Al-Qaadhi ‘Ala’ ad-Diyn al-Mardaawi (Amefariki mwaka 885 H) ameandika fafanuzi ya Uswuul bin Muflih[71] (Amefariki mwaka 763 H) yenye jina la Tahriyr al-Manquul wa Tahdhiyb ‘Ilm al-Uswuul. Kazi hii imefanyiwa uchunguzi na kufanyiwa uhariri, na ipo tayari kuchapishwa hivi karibuni. Mchunguzi huyo huyo, pia amejihusisha na Uswuul bin Muflih.

Baadaye, Ibn an-Najjaar al-Futuuhi wa fikra za kisheria za mafunzo ya Hanbali aliandikia ufupisho wa Tahriyr al-Mardaawi, na aliandika fafanuzi iliyokuwa nzuri kabisa. Fafanuzi hii inatambulika kuwa ni moja kati ya iliyo bora na yenye mambo mengi ya vitabu vilivyopita kuhusu al-Uswuul. Toleo ambalo halijakamilika la kitabu hicho, lilichapishwa nchini Misr kabla ya kuchungzwa na kufanyiwa uhariri na Maprofesa wawili muhimu, Dr. Nazih Hamaad na Dr. Muhammad az-Zuhayli. Kazi yao ilichapishwa na Kituo cha Elimu ya Uchunguzi kwenye Kitivo cha Shari’ah huko mjini Makkah. Sehemu kubwa ya kitabu hicho kimeshachapishwa, na kilichobaki sasa ni kazi ya wapigaji chapa.

Kwenye karne ya kumi na mbili AH, Muhiyb Allaah bin Abdush-Shakuur al-Bihaariy, wa mafunzo ya Hanafi (Amefariki mwaka 1119 AH) aliandika kitabu chake maarufu kwenye Uswuul, Musallaam ath-Thubuut. Hichi ni kimoja kati ya kitabu kilicho makini na chenye mambo mengi kilichoandikwa na kizazi cha baadaye cha wanazuoni wa Hanafi. Kitabu kimechapishwa pamoja na fafanuzi nchini India, na halikadhalika kimechapishwa pamoja na fafanuzi yake maarufu ya Fawaatih ar-Rahamuut, kwa kuegemeza mara kadhaa kitabu cha al-Mustaswfa cha Imaam al-Ghazaaliy.

Vitabu vyote hivi viliandikwa kufuatana na mtindo uliotajwa hapo juu, na wote hao walikuwa makini kwenye kutetea Madh hab ya mwandishi na kukataa yale ya wapinzani wake. Kutoka karne ya sita hadi sasa, hakuna Uswuul al-Fiqh yenye sifa ya kuwa ni nyenzo ya kufanyia uchunguzi, ambacho kitawalinda Wanazuoni wa Kiislamu kutokana na kufanya makosa kwenye Ijtihaad; isipokuwa kutokana na kitabu kimoja maarufu kilichoandikwa katika kupasisha kitabu cha ash-Shaykh Mustafa ‘Abd ar-Razzaaq Tamhiyd li at-Taariykh al-Falsafa al-Islaamiyyah “Dibaji ya Historia ya Falsafa ya Kiislamu”. Mwanafunzi wake, alijaribu kueleza kitabu hichi maarufu ndani ya kitabu chake Manaahij al-Bahth “Mitindo ya Uchunguzi.”

Mnamo karne ya kumi na tatu Hijriyah, Al-Qaadhi ash-Shawkaani’ (Amefariki mwaka 1255 H) aliandika kitabu chake maarufu kwenye UswuulIrshaad al-Fuhuul “Muongozo wa Wakuu”. Ijapokuwa juzuu zake ni ndogo, kitabu hichi kinawakilisha mawazo tofauti kwenye uwanja wa al-Uswuul, na ushahidi uliotumika na wasomi wa kila mmoja ni kwa njia ya ufupi lakini kwa mtindo safi kabisa, mwandishi pia anaeleza mawazo gani yeye anapendelea. Kitabu hichi, ambacho kimeshachapishwa mara kadhaa, ni chenye manufaa kwa mwanafunzi wa Uswuul al-Fiqh na kwa masomo ya kupambanisha (comparative) kwenye maarifia ya Sheria. Hata hivyo, kwa muono wetu wa elimu, hakijaingizwa kwenye mtaala wa taasisi yoyote, ingawa ni kitabu muafaka.

Muhammad Swiddiyq Khaan (Amefariki mwaka 1307 H), ameifupisha kazi hii kwenye kitabu chenye jina la Huswuul al-Ma’muul min ‘Ilm al-Uswuul “Kuyafikiria kwa Yale Yaliyotegemewa Kwenye Sayansi ya al-Uswuul” ambacho kipo katika chapa.

Hakika, Irshaad al-Fuhuul kinakadiriwa kuwa ni ufupisho mwanana kabisa wa al-Bahr al-Muhiytwya az-Zarkhaasi. na Tas-hiyl al-Uswuul ya al-Mahallaawi inakadiriwa kuwa ni ufupisho wa Irshaad al-Fuhuul.

Baada ya kipindi hichi, tunaona kwamba, somo la al-Uswuul limefuata moja kati ya mielekeo mikuu ifuatayo:

1)    Kuandika miongozo ya masomo, ufupisho na hati (notes). Hili limefanywa na Maprofesa wa vitivo tofauti vya Shari’ah na Sheria, ili kulifanya somo la Uswuul al-Fiqh kuwa ni jepesi kwa wanafunzi wao; baada ya kutambua kwamba wanafunzi wao hawakuweza au hawakuwa tayari kulisoma somo hili. Matokeo yake, hati hizi haziwakilishi aina yoyote ya elimu ya juu kwenye uwanja huu; na kwenye kesi nyingine ni kule kujaribu tu kubadilisha masuala ya al-Uswuul al-Fiqh katika njia nyepesi na ya kisasa. Wanazuoni wafuatao: Marsafi; al-Mahallaami; al-Khudari, ‘Abdul-Wahhaab Khallaaf, ash-Shinqiti, as-Sayis, Mustafa ‘Abdul-Khaaliq, ‘Abdul-Ghani, ‘Abuu Zahrah, Abuu Nuur Zuhayr, Ma’ruuf ad-Dawaalibi, ‘Abdul-Kariym az-Zaydah, Zaki ad-Diyn Sha’baan, Muhammad Salaam Madhkuur, na wengineo wote, wameandika vitabu ambavyo kiuhalisi ni mihadhara ambayo wameitoa ndani ya vitivo walivyosomesha vya Shari’ah na Sheria.
2)    Muelekeo wa pili ulikuwa ni uandishi wa chunguzi (researches) za Vyuo Vikuu kwenye aina tofauti za sayansi hii, na uchunguzi na uhariri wa maandiko yasiyochapishwa. Bila ya shaka, aina zote mbili za mielekeo ni yenye manufaa makubwa, na hakika mimi sitokuwa na nia ya kuzibeza nguvu za yeyote. Lakini mielekeo hii inaangukia kuwa si chochote katika kufanikisha maendeleo ya ndani ya uwanja huu, na sanyansi ya Uswuul al-Fiqh inabaki kuwepo sehemu ile ile ambayo waliotutangulia wameiacha ndani ya Karne ya Sita Hijriyah.

Kutokana na maelezo ya hapo juu, tunaweza kupata hitimisho zifuatazo:

1.     Hakuna somo, ambalo sasa linajulikana kama Uswuul al-Fiqh, lililopata kuibuka likiwa na misamiati yake wakati wa enzi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘Anhum) zake.

Hata hivyo, takriiban mienendo ya Ijtihaad za aina tofauti zilizotumika wakati wa vipindi hivi viwili, ziiliweza kuwekwa chini ya misingi inayozunguka sayansi hii. Sababu za hili, ni kwamba walikuwa wakifikia maelezo ya kina ya hukumu zao kisheria kwenye suala maalum kutokana na vyanzo vya Sheria kama ni aina isiyokuwa na kanuni maalum, kama vile wanavyozungumza Kiarabu bila ya kanuni, au bila ya kuelewa kanuni za sarufi ambazo bado zilikuwa hazitambuliki wakati huo.

2.     Mwanazuoni wa mwanzo kukusanya kitabu kuhusu kanuni za sayansi ya Uswuul al-Fiqh alikuwa ni al-Imaam Muhammad bin Idriys ash-Shaafi’iy (150-204 H).

Kitabu cha mwanzo chenye maarifa ya kina kwenye somo hili kilikuwa ni Risaalah, ambacho ameandika kwa kuitikia ombi kutoka kwa al-Imaam ‘Abdur-Rahmaan bin al-Mahdi (135-198 H). Hii ilikuwa baada ya mafunzo maarufu ya Fiqh, mafunzo ya Ahl al-Hadiyth, yakiongozwa na al-Imaam Maalik bin Anas (93-179 H), na mafunzo ya Ahl ar-Ra-ay yakiongozwa na al-Imaam Abuu Haniyfah (70-150 H), yamepata kuanzishwa na kuenea mno.

Kutokana na kuenea sehemu tofauti kwa mafunzo haya mawili ya fikra za sheria, kukaibuka baina ya wafuasi wa mafunzo haya mawili, kwa kuongezea migongano ya kisiasa, kifikra na kinadharia iliyokuja juu wakati huu, ambayo yalikuja kutambulika kama ni “Mabishano ya Fiqh”.[72]

3.     Uswuul al-Fiqh ni nyenzo ya kufanyia uchunguzi kwa wanazuoni[73] na sehemu yake ya Fiqh inafanana na ile ya Dhana ndani ya Filosofia[74] (Logic in Philosophy). Hivyo, ilitolewa tafsiri kama ni “Mkusanyiko unaotambulika wenyewe, kuwa ni thibati za Shari’ah na ushahidi, kwamba, inaposomwa kisawasawa, utapelekea ama kwenye elimu maalum ya hukumu za Shari’ah au kwa uchache fikra za dhana zenye hoja kuhusiana na hilo hilo, tabia ambazo thibati hizo zinapatikana, na hadhi ya mthibitishaji.”[75]

Hivyo, Uswuul al-Fiqh inatoa muongozo wa kina unaomlinda Mujtahid kufanya makosa kwenye mitindo tofauti inayotumia chanzo halisi kwa lengo la kufikia hukumu za kisheria.[76] Juu ya hivyo, haikutumika kwa njia hii hadi al-Imaam ash-Shaafi’iy alipoiweka kwenye matumizi ndani ya Fiqh yake “Mpya”.[77]

4.     Ukweli muhimu ambao unaweza kuwekwa akilini ni kwamba wanazuoni wamesoma Fiqh na kutolea matamko kuhusiana nayo, kabla ya yeyote kuanza kuzungumzia kuhusiana nayo hiyo Uswuul(achilia mbali kazi ya Fiqh “Mpya” ya al-Imaam ash-Shaafi’iy).

Hivyo, majukumu waliyopewa na wengine kwa Uswuul al-Fiqh yalikuwa ni kidogo, kuliko yale ya kuthibitisha matamko ya kisheria Fataawa, ambazo walizitoa kwenye masuala maalum, na uzito wa hoja na mjadala baina yao. Hawakuangalia Uswuul al-Fiqh kama ni muongozo wenye maarifa ya kina ya Sheria au kama ni mtindo unaoweza kutumika katika muundo wote wa sheria. WanazuoniFuqaaha, walipoendewa na masuala pamoja na migogoro, walikuwa wakirudi nyuma moja kwa moja kwenye ushahidi ulio mnasaba, bila ya kuona haja ya kutumia kanuni za jumla zinazotumika ndani ya Uswuul al-Fiqh.

Hivyo, al-Imaam Abuu Haniyfah alitoa Fataawa zinazokaribia kufikia nusu milioni,[78]ambazo wanafunzi wake walisoma na kufaulu. Lakini, kanuni za kisheria ambazo al-Imaam Abuu Haniyfah aliegemezea Fataawa hizi, hazikuonekana chochote kama ni mstari usioingiliwa na mamlaka yake,[79] ukiacha simulizi chache ambazo alielezea kwa baadhi ya vyanzo vyake vya Ijtihaad. Alisema, ndani ya simulizi zake:

“Ninafuata Kitabu cha Allaah, na kama sikupata suluhisho humo, ninafuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kama sikupata suluhisho ndani ya Qur-aan au Sunnah, ninafuata matamko yoyote ya Swahaabah ninayopendelea mimi, na kuachana na yeyote ninayetaka. Kama kuna tamko kwenye suala maalum na Swahaabah yeyote, sitotumia mawazo mengine yoyote yaliyotumika na mwanazuoni yeyote. Lakini, kama nitapata suluhisho pekee kwenye mawazo ya Ibraahiym, ash-Sha’bi, Ibn Siyriyn, Hasan al-Baswriy, Atwa’a Sai’iyd bin al-Musayyab, nitafanya Ijtihaad kama walivyofanya wao.”[80]

Pale watu walipojaribu kumfanyia uadui Abuu Haniyfah dhidi ya Khaliyfah, al-Mansuur, aliandika kumpelekea Khaliyfah:

“Hali ilivyo sivyo kama ulivyoisikia, Ewe Amiyr al-Mu’miniyn! Nimefanya kazi kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah, kisha kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume, kisha kwa mujibu wa hukumu za Abuu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy, kisha kwa mujibu wa hukumu za Swahaabah waliobaki. Kisha, kama kutakuwa na mgongano baina ya matamshi yao, ninayatuliza kwa al-Qiyaas. Hakuna kiumbe wa Allaah aliye na urithi wa karibu Kwake Yeye kuliko mwengine.”[81]

Pale alipotuhumiwa kupendelea zaidi matumizi ya al-Qiyaas kuliko maandiko yaliyo wazi Nassndani ya Qur-aan, alijibu: “Naapa kwa Allaah, wale wanaosema kwamba tunapendelea al-Qiyaaskuliko Nassw wamesema uongo na wametusengenya. Je, kuna haja yoyote ya al-Qiyaas baada (kupata iliyo dhahiri) ya Nassw?”[82]

5.     Ni uwazi ulio dhahiri kwamba tokea hapo awali mwa kipindi cha Umaawi hadi kuporomoshwa kwaKhaliyfah wa Kiislamu, mamlaka na uongozi ndani ya Ummah ulikuwa ndani ya mikono ya wale wasio na sifa za kuifanyia kazi Ijtihaad, wakati huo huo, majukumu ya Ijtihaad yalipelekwa kwa‘Ulaama’ wasio na mamlaka. Na si rahisi kupata mbadala wa jambo hili, isipokuwa kwa Khaliyfah‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziyz, ambaye kutokana naye, hukumu nyingi zinahusiana na masuala ya maarifa ya sheria za Kiislamu zimesimuliwa. Hali hii ilikuwa na athari kubwa sana ya kuigwa Fiqhna Uswuul yake kutoka katika mandhari ya matendo ya maisha ya Muislamu, ili kwamba, kwenye kesi zilizo nyingi, masomo haya yalikuja kuwa ni ya kinadharia na kifikra.[83] Kimsingi, masomo yote yalikuja kuwa ni maelezo ya namna maisha ya Muislamu yanavyotakiwa yawe; sio namna ilivyokuwa, au namna itakavyokuwa baadaye.

6.     Waandishi na wanahistoria wa sayansi waliweka miongoni mwa sayansi za Shari’ah ambazo zimeegemezwa kwenye ushahidi uliotoka sehemu moja kwenda nyengine,[84]ijapokuwa baadhi ya waandishi walisema kwamba kanuni zake zimechukuliwa kutoka kwenye lugha ya Kiarabu, sayansi ya mawazo, na taratibu nyengine za Kiislamu.[85]Mmoja miongoni mwa waandishi waliobobea kwenye uwanja huu, ni al-Imaam al-Ghazzaaliy, ameandika:-

“Sayansi za kusifiwa ni zile ambazo sababu ‘Aql na ushahidi uliopokewa Sama’ zinashikana pamoja, na ambazo hitimisho linaegemezwa katika hoja zikiambatana na zile zilizoegemezwa kwenye uteremsho. Sayansi ya Fiqh na Uswuul yake ni moja miongoni mwa sayansi hizi. Inachukua sawa sawa kutoka uhalisi wa uteremsho na hoja bora. Hata hivyo, haitegemei kiuhalisi kwenye hoja hadi kufikia kwamba haitokubaliwa mbele ya sheria ya uteremsho, na wala haiegemezwi kiurahisi kwenye aina ya kukubali kwa upofu ambapo haitoshikana na hoja.[86]

Matamko ya al-Imaam al-Ghazaaliy na waandishi wengine kwenye somo la al-Uswuullinatuwezesha sisi kuwaza kwamba kuna vyanzo vitatu vya Fiqh:

i)                   Wahy uteremsho ulio Mtukufu: hii inahusisha vyote viwili, iliyokusanya Qur-aan isiyoigika, na wahyi usiyokusanywa, au Sunnah.
ii)                  ‘Aql au hoja: kuelezea maandiko, kutafuta njia ambazo zinaweza kutumika na njia ambazo sehemu tofauti zinaweza kuunganishwa kama kitu kimoja, kutafuta hoja zilizo kwenye sheria ambazo zinaonesha kuwa hazina hoja, kupata sheria kwenye mambo ambayo Mtungasheria hakuweka hukumu zilizo wazi ndani ya maandiko, na mambo mengine yanayofanana ambayo yanaweza kutafsiriwa na kuelezewa.
iii)                Uzoefu, mila na manufaa ya jamii.

Uswuul zote, ambazo zile wanazuoni walizokubaliana na zile zinazohusiana na kutokubaliana, zinaweza kugaiwa chini ya mada tatu kama ifuatavyo; Qur-aan, Sunnah, al-Ijma’al-Qiyaas, fikra ambayo kimsingi ni kuhusiana na yenye manufaa yanaruhusiwa na yaliyo na madhara. Kimsingi yanayozuiwa, al-Istis-haab na al-Istihsaan. Kwa kuongezea, matamshi ya Swahaabah yalikuwa ni maarufu miongoni mwao na hakuna yeyote miongoni mwao aliyeyakataa, kanuni za daima (zilikuwa ni) kutumia mbadala wa isiyokuwa tata japo kwa hali ya chini; kusoma kesi kidogo zinazoweza kupatikana na zenye mnasaba kwa lengo la kupambanisha, manufaa ya umma na mila ambazo wala hazikuamrishwa au kuzuiwa ndani ya vyanzo vya Kiislamu; hitimisho kwamba hakuna sheria ambapo hakuna kitu cha kuonesha sheria yoyote, sheria za mataifa kabla ya Uislamu, na kuufunga mlango kuhusiana na hoja zilizo thibati.

  1. Kulikuwa na sababu fulani ndani ya historia yetu, baadhi yake, zimetajwa juu, kwamba, vyote vilipelekea kuwekwa vikwazo vingi juu yetu. Hivyo, lengo la akili zetu za Kiislamu na fikra na mantiki yalipelekwa kwenye masuala madogo, na kwamba tulikuwa tumezuiliwa kufikiri kwenye mambo mengi sifa zilizoonekana kuwa ni sura za mawazo ya Kiislamu. Hili lilikuwa na athari ya mbali kwenye namna tunavyojihusisha na Fiqh na suluhisho tunazotoa, na hizi nazo pia zimezaa sifa na sura hizo hizo.

  1. Ni jambo linalojulikana kwamba kwenye kila sayansi na maisha ya dunia, kuna mambo ambayo kiuhalisi yanakubali maendeleo, kwamba mara nyingine inahitaji kuwepo mpangilio ili kutambua uwezekano wake kamili. Hata hivyo, kuna baadhi ya mambo ambayo yameganda na hayakubali mabadiliko. Kwa mujibu wa nadharia za Kiislamu, hayo mambo mawili ni lazima yaunganishwe. Hivyo, Uswuul al-Fiqh zina sheria imara zisizobadilika, ambazo haziwezi kubadilishwa, na nyengine zinategemea kwenye maendeleo yenye kuendelea na kuzifanya mpya. Hili lipo wazi kutokana na mjadala wetu tulioenda nao kwenye Ijtihaad.

Hivyo, wakati tunapohimiza wanazuoni wote wa Kiislamu kutoanza kwa kukumba ila waanze kwenye kufaidika na hoja na Ijtihaad za wanazuoni ambao walizipitia kabla yao. Tunathibitisha kwamba, hakuna aliyedai kwamba hili ni jambo la lazima kulifuata kwa kila Mujtahid kwenye mambo ambayo matamshi yake yaliegemea tu kwenye hoja zake binafsi. Kubwa tunaloweza kusema kwenye jambo hili kwamba matamko yake ni: “ushauri, na ushauri unaweza kutumiwa”.[87]

  1. Kutokana na kusoma mitindo ya Waislamu wa kale, ni uwazi kwetu kwamba lengo kuu halikuwa rahisi katika kuichambua sheria na baadaye kutoa Fataawa. Hapo hapo, kwa upande mwengine dhumuni lao daima lilikuwa ni kusimamisha Mamlaka ya Allaah kupitia matumizi ya sheria Zake. Hili maana yake, kimsingi ni kwamba mazingira yaliyozunguka matumizi ya sheria hayawezi kutenganishwa na masharti yaliyoambatanishwa nayo.

Kama, kwa kuelewa hayo juu, tunahitaji kurudisha sayansi hii katika sehemu yake iliyo sahihi miongoni mwa sayansi za Kiislamu na kuibadilisha kwenye mtindo wa uchunguzi kwenye chanzo cha ushahidi wa Shari’ah ambapo huko tunaweza kupata hukumu, na masuluhisho, ya matatizo yetu ya kisasa, (hivyo kuendeleza kisawasawa Mamlaka ya Shari’ah), ni lazima tufanye yafuatayo:-

i)                   Kupitia upya mada zilizohusishwa ndani ya sayansi hii na kuzuia zile ambazo zisizo na uhusiano na wanazuoni wa kisasa au mwanachuoni. Hizi zinaweza kuwa Hukm al-Ashyaa Qabl ash-Shar’“Hukumu kabla ya Shari’ah” Shukr al-Muniym “Namna mtu anavyotakiwa Kumshukuru Mwenye Nguvu Mwingi wa Rehema”. Mabaahith Hakimiyyatul ash-Shar’ “Masomo Kuhusiana na Mamlaka ya Shari’ah”, na kujihusisha sana na tafsiri. Ni lazima pia tutolee maamuzi migogoro kuhusiana na yasiyo kawaida Qira-aat Shadhdhah “Usomaji ulio Mbadala” wa Qur-aan, na asili ya Kiarabu ya Qur-aan nzima. Vivyo hivyo, ni lazima sasa tumalize msururu mrefu wa kutokubaliana kuhusu Hadiyth ya msimulizi-mmoja kwa kusema kwamba, kama simulizi hiyo itathibitishwa kwamba inaendana pamoja na masharti ya kuwa Swahiyh, itakubaliwa, na sheria zinaweza kupatikana humu.

Juu ya hivyo, ni lazima tupitie tena masharti yote, yaliyowekwa na baadhi ya wanazuoni wa kale, ambao wanaonekana kuathiriwa na mazingira. Kwa mfano, sharti ya kwamba Hadiyth isigongane na kanuni za jumla walizoweka, kwamba isisimuliwe na asiyekuwa mwengine ila ni Faqiyh, kwamba isigongane na al-Qiyaas, au utamaduni wa watu wa Madiynah, na maana zilizo waziDhwaahir za Qur-aan. Au sharti ya kwamba Hadiyth, kama inahusiana na suala la kawaida au gumu au lililo na taabu, ni lazima lijulikane na walio wengi. Masharti yote haya yatupiliwe mbali, na mtindo huu huu ufanyike kwa sharti nyengine. Kwa sababu yalikuwa na yataendelea kuwa ni mkanganyo na chanzo cha kutokubaliana baina ya Waislamu, na ambayo bado yanakula muda wa wanazuoni.

ii)                  Kuchukua somo la lugha kuhusiana na Fiqh ambalo litaangalia mitindo ya misamiati iliyotumika na Waarabu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuangalia hatua za maendeleo, ambapo mitindo hii baadae ilipitia, na maana tofauti zilizonasibishwa kwenye maneno katika matumizi ya wakati huo. Hili, linatuwezesha kuelewa maandiko kama yanavyotakiwa kueleweka.
iii)                Kuwa makini na mitindo na kanuni zilizomo katika kuitekeleza Ijtihaad, kama vile al-Qiyaasal-Istihsaanal-Maswlahah, na nyenginezo, na kuzisoma kwa uoni wa historia, na kuweka akilini mazingira yaliyowapelekea kutamka matamko kutoka kwa Mujtahiduun. Ni lazima pia tujaribu kuingiza mhimili wa akili za wanazuoni kwa wale ambao wanafanya uchunguzi ndani ya mwanga wa al-Faqiyh na al-Uswuul.
iv)               Kuelewa kwamba kwa wakati huu, haiwezekani kuwepo Mujtahid Mutwlaq, na mwenye mamlaka ya kisheria (kwenye kutoa tafsiri ya vyanzo) katika haki yake mwenyewe, kutoa hukumu kwenye masuala. Kwa umbali wa tutakapofika kuhusu hili, labda ilio karibu na mbadala ni Mabaraza ya Kitaalamu.

Ili kuweza Mabaraza haya kutatua mahitaji ya Ummah kwenye masuala ya sheria, ni lazima yawe na jopo la wataalamu ambao uzoefu wao umo kwenye vitengo tofauti vya maisha, na ambao wataweza kwa uwazi kuona tatizo lolote lililopelekwa kwao. Kwa kuongezea hili, itawabidi kuwa na maarifa kamili ya maamuzi ya msingi na kanuni za Shari’ah ya Kiislamu. Mabaraza kama hayo ni lazima pia yawe na wanazuoni wengi wenye hadhi iliyo juu kabisa inayoweza kuwa, katika maarifa ya vyote viwili, sayansi ya Shari’ah na chanzo cha ushahidi kilicho na maelezo ya kina. Labda, mmoja miongoni mwa wanazuoni alikuwa akimaanisha fikra hii pale alipokutana na mtu aliyetaka kufungua Swawm yake ndani ya mwezi wa Ramadhaan na mwanazuoni alimwambia mtu huyo kutafuta mawazo ya daktari Muislamu aliye muaminifu, na kwa kuongezea kwamba; kama daktari huyo atatambua kuwa Swawm hiyo ni yenye dhara kwa afya yake, basi itaruhusiwa kwake yeye kujizuia kufunga Swawm.

v)                Ni lazima tufanye urahisi kwa wataalamu kwenye nyanja nyengine kusoma yale wanayohitajia katika sayansi ya Shari’ah.
vi)               Ni lazima tuwe wazoefu na Fiqh ya Swahaabah na Taabi’un, na zaidi ni kanuni ambazo walitumia kutolea maamuzi yao. Kwa uhalisi, Fiqh ya Khulafaa ar-Raashiduun na wafuasi wao inahitaji kusomwa kwa undani. Baadaye, elimu hii inaweza kuwakilishwa kwa wale ambao kazi yao ni kutengeneza sheria na kutoa hukumu ili kujibu mahitaji ya jamii ya Waislamu ya kisasa.
vii)             Ni lazima kuwa na mapenzi ya kuelewa malengo na madhumuni ya Shari’ah, na kuliendeleza somo hili kwenye masuala haya, kwa kuweka kanuni na miongozo.


Na Allaah Ndie Mtoaji wa Tawfiyq (ya Mafanikio na Khayr).


[70] Sababu nyingine ni ule uonekano kwamba mwanazuoni anajaribu Kumuaguwa Mtukufu “kwa mara ya pili”.
[71] Sehemu ya kazi hii imehaririwa na mwanafunzi kwa kutunikiwa uchunguzi wa shahada ya pili (Master’s thesis); na anakifanyia uhariri sehemu iliyobaki kwa kutunikiwa shahada ya tatu (Doctoral).
[72] Angalia Ibn Khalduun, Al-Muqaddimah, III, uk. 1163-64.
[73] An-Nashshar, Manaahij al-Bahth, uk. 55.
[74] Angalia Musallam ath-Thubuut na fafanuzi zake zikiambatana na kitabu cha al-Ghazzaaliy al-Mustaswfa, I, uk. 9-10. Mwandishi alikana kwamba dhana zilikuwa kama hizi, na kudai kwamba nafasi ya dhana kwenye uhusiano wa yote, hiyoUswuul al-Fiqhi na filosofia ulikuwa sawa. Inawezekana ameathiriwa na mawazo kwamba dhana ni kiwango cha sayansi zote.
[75] Angalia Sura ya Kwanza ya kazi hii.
[76] Angalia ar-Raazi, Manaaqib ash-Shaafi’iy, uk. 98, na an-Nashshaar, Manaahij al-Bahth, uk. 55.
[77] Jina la Fiqh “Mpya” la kazi ya al-Imaam ash-Shaafi’y kwenye kazi yake kisheria limetolewa baada ya kuishi Misr. Hakika, kazi hii inawakilisha fikra zake zilizobobea kutokana na kipindi kirefu cha masomo yake chini ya mafunzo yote ya fikra za sheria za madhehebu ya ki-Maalik na ki-Hanafi.
[78] Angalia Mustafa ‘Abd ar-Razzaaq, al-Imaam ash-Shaafi’iy, uk. 45
[79] Angalia ad-Dahlaawi, Al-Insaaf na Abuu Zahrah, Abuu Haniyfah, uk. 223.
[80] Angalia Taariykh Baghdaad, Juzuu ya XXXI, uk. 368, al-Intiqa’, uk. 142, naMashaayikh Balkh al-Hanafiyyah, uk. 190.
[81] Angalia as-Samarqandi, Miizaan al-Uswuul, I, uk. 52; Taaqi’ ad-Diyn al-Ghazzi,at-Twabaqaat as-Saniyah, I, uk. 43 na Mashaayikh Balkh, uk. 193.
[82] Rudia rejeo (footnotes) nambari 81.
[83] Angalia Muhammad Yuusuf Muusa, Taarikh al-Fiqh, uk. 160.
[84] Angalia al-Khawarizmi, Mafaatih al-‘Uluum, Juzuu ya VI, VIII; na Ibn Khalduun,Al-Muqaddimah, III, uk. 1125-1128, 1161-1166.
[85] Angalia Miftaah as-Sa’adah.
[86] Angalia al-Ghazzaaliy; al-Mustaswfa, Juzuu ya Kwanza, uk. 3 na al-Mankhuul, pia Shifa’ al-Ghaliyl fiy Bayaan ash-Shibk wa al-MalkhiylMaswaalih at-Ta’liyl, naTahdhiyb al-Uswuul, vyote ni vitabu muhimu kwenye Uswuul.
[87] Msemo maarufu unaonasibishwa na Khalifyah ‘Umar bin al-Khatwwaab.

0 Comments