MLANGO WA TWAHARA : AINA YA NAJISI

Suali: Ni zipi Aina za Najisi ?
Jawabu: Najisi kwa mtazamo wa sheria zimegawanywa katika aina tatu zifuatazo :
1.NAJISI NZITO: Hii ni najisi ya mbwa na nguruwe na mnyama aliyezaliwa kutokana nao au mmoja wao (mbwa na nguruwe). Najisi hii imeitwa najisi nzito kutokana na uzito unaompata mtu katika kuiondosha
2.NAJISI KHAFIFU: Hii ni mkojo wa mtoto mchanga wa kiume aliye chini ya miaka miwili na hali ila maziwa ya mama tu. Najisi hii imeitwa Najisi khafifu kwa sababu ya wepesi unaopatikana katika uiondosha.
3.NAJISI YA KATI NA KATI: Hii imekusanya baki ya najisi nyingine ukiondoa najisi ya mbwa na nguruwe na mkojo wa mtoto mchanga wa kiume. Najisi hii imeitwa Najisi ya kati na kati kwa kuwa haiko kwenye uzito na wala haikufika kwenye ukhafifu.

NAMNA YA KUZIONDOSHA NAJISI HIZI:

Ni muhimu tukakumbuka kuwa ni haramu kujipakaza najisi na ni wajibu kuiondosha mara tu inapoingia mwilini, nguoni au mahala pake mtu.
Hutwahirishwa mahala palipoingiwa na najisi ya mbwa na nguruwe kwa kupaosha mahala hapo paliponajisika kwa kupaosha mara saba na mojawapo wa mara saba hizo iwe kwa kusugua na mchanga. Bwana Mtume amesema:
طُهُورُ إِنَاءِ أحَدِكُمْ إِذَا وَلَغَ فِيهِ الكَلْبُ أنْ يَغْسِلَهُ سَبْعَ مَرَّاتٍ أُولاَهُنَّ بِالتُّرَابِ. رواه مسلم

[Twahara ya chombo cha mmoja wenu atakapokiramba mbwa ni kukiosha mara saba, ya kwanza yake ( hizo mara saba) iwe ni kwa mchanga]      [Imepokewa na Muslim]
Najisi khafifu hutwahirishwa mahala paliponajisika kwa kuimwagia maji sehemu hiyo, maji yaenee.

عن أم قيس بنت محصن الأسدية أنها أتت بابن لها صغير لم يأكل الطعام إلى رسول الله صلى الله عليه وسلم ، فأجلسه رسول الله صلى الله عليه وسلم في حجره ، فبال على ثوبه ، فدعا بماء فنضحه على ثوبه ولم يغسله
Imepokewa hadithi kutoka kwa Ummu Qays Bint Mihswan-Allah amridhie- kwamba
[alimpeleka Mtume wa Allah mtoto wake mdogo wa kiume ambaye hajala chakula (ananyonya) akamkojolea (mtume) nguoni, akaagizia maji na kuyamiminia palipokojolewa na hakuiosha (nguo)].     [Imepokelewa na Bukhaariy na Muslim.]
Ama Najisi ya kati na kati, mahala paliponajisika kwa kuingiwa na najisi hii hutwaharishwa kwa kupaosha na maji twahara mpaka iondoke rangi, utamu na harufu ya najisi hiyo.
Haidhuru kubakia kimojawapo rangi au harufu ziloshindikana kuondoka.

0 Comments