NIYYAH YA SWAWM NI KWA KILA SIKU AU MARA MOJA INATOSHA

SWALI:
kuna nukta chache ningependa ufafanuzi zaidi. 


Kuhusu nia, nimetatizika kidogo maana masheikh wetu huku wanatuambia inabidi kunuia kila siku. Na kama mfano bahati mbaya mtu akalala bila kunuia siku hiyo basi hana Swaum. Kama kasahau kunuia usiku huo haruhusiwa kula na inabidi aje kuilipa siku hiyo.
Naomba ufafanuzi, usahihi ni vipi kuhusu nia, ukitia nia siku ya kwanza yatosha kufunga mwezi mzima ama lazima kila siku unuie kama kesho wafunga?


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa hili ni suala sahali lakini kwa sababu ya kutaka kuongeza mambo katika Dini yetu tunawapatia ugumu Waislamu wa kawaida bila ya kuwa na haja aina yoyote.
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) hata kwa mwezi wa Ramadhaan Anatutakia usahali pale Aliposema:
Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi atayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allaah kwa kuwa Amekuongoeni ili mpate kushukuru” (2: 185). 

Na katika hali zote Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini” (22: 78).
Shari'ah za Kiislamu zimekuja kuhafifisha na kuondoa uzito mwingi uliokuwepo.
Ya kustaajabisha ni kuwa utakuta katika mambo mengi tunarudisha ugumu usiokuwepo. Mfano ni mas-ala niyyah katika Funga ya Faradhi, kulipa Funga ya Faradhi au Kafara. Katika Swawm zote hizo ni lazima Muislamu atie niyyah na bila niyyah mfungaji hatokuwa na Swawm.
Lakini je, niyyah inatiwa namna gani? Utakuta katika sehemu nyingi ulimwengu watu wanatilishwa niyyah na ima Imaam au Muadhini au Shaykh ilhali jambo kama hilo ni uzushi kutoka kwa watu. Kufanya hivyo kumewapatia uzito Waislamu wengi na hivyo kuzua maswali kama haya yanayoulizwa.
Kuhusu swali lako la kutia Niyyah kama ni kila siku au inatosha kuiweka siku ya kwanza ya kuanza Ramadhaan, hili hakika wametofautiana Maulamaa kuna waliokwenda na kuona inatosha mwanzo wa mwezi wa Ramadhaan kuiweka niyyah na ukatosheleza mwezi mzima. Lakini Wanachuoni wengi wameonelea Niyyah ni kuwekwa kila usiku wa kabla yake na hi ndio kauli yenye nguvu. Na Niyyah inaweza kuwekwa katika sehemu yoyote ya usiku hata ikiwa ni sekunde chache kabla ya Alfajiri ya kweli (yaani wakati wa adhana ya pili). Maana ya niyyah hasa ni kuazimia kwa moyo kutekeleza 'amali fulani, na kuitamka kwa ulimi ni uzushi usiofaa katika Dini.


Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments