UFAFANUZI WA THAWABU ZA SITA KAMA KUFUNGA MWAKA MZIMA

Asalam alaykum

Nataka kujua vipi imekusudiwa kuwa mtu akifunga sita atapata thawabu za mwaka mzima? Maana nimesikia kwamba ikiwa hukutimza Ramadhani basi hupati thawabu hizo je, ni kweli?

Nitashukuru kupata jibu kabla ya mwezi wa sita kwisha.
JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hayo ni kutokana na Hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه

((Atakayefunga Ramadhaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal' itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]

Inavyompasa Muislamu ni kwamba anatakiwa kwanza alipe deni lake la Ramadhaan kisha ndio afunge 'sitatu Shawwaal' ili aweze kupata thawabu za kama kafunga mwaka mzima. Na maulamaa wameona hivyo ni kutokana na dalili zifuatazo katika Qur-aan na Sunnah:

Katika Qur-aan:

Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))

((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An'aam:160]

Katika Sunnah:

Kuna Hadiyth mbali mbali zinazothibitisha kauli hiyo ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala), tutazitaja hapa mbili:

Ya kwanza ambayo kutokana na Imaam At-Tirmidhiy kuwa ni sababu ya kuteremshwa Aayah hiyo:

 ((من صام ثلاث أيام من كل شهر فقد صام الدهر كله))

((Atakayefunga siku tatu katika mwezi atakuwa amefunga mwaka mzima)) [Ahmad, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, At-Tirmidhiy]

Hadiyth ya pili:

((إن الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها الله له عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر حسنات , إلى سبعمائة ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها , كتبها الله عنده حسنة كاملة , فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة واحدة )) متفق عليه ،  

((Allah Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia nia kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya  ataandikiwa dhambi moja)) [Al-Bukhaariy ya Muslim]

Kutokana na dalili hizo, kwamba kila jema mtu anapata mara kumi, hivyo Swawm ya Ramadhaan itakuwa ni hivi:

       30 x 10  = 300

Na funga ya 'sitatu Shawwaal' itakuwa ni 6 x 10  = 60

300  + 60  = 360

Hivyo siku 360 ni sawa taqriban na mwaka mzima. 

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments