001 - Al-Faatihah

 الْفَأتِحَة
Al-Faatihah[1]: 1
Imeteremka Makkah kwa kauli iliyokuwa Sahihi, na ndiyo kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿١﴾
1. Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.


 الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾
2. AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu.


الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣﴾
3Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.


 مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٤﴾
4. Mfalme wa siku ya malipo.


 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾
5. Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.


اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿٦﴾
6. Tuongoze njia iliyonyooka.[2]


صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ ﴿٧﴾
7. Njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.[3]


[1] 
 Faida: Hii ni Suwrah iliyokuwa Adhimu na bora, kuliko Suwrah zote za Qur-aan, nayo ni miongoni mwa Suwrah zenye majina mengi na miongoni mwa majina yake ni: Al-Faatihah, Ummul-Qur-aan, AlhamduliLLaah, Asw-Swalaah, Ash-Shifaa, Ar-Ruqyah, Sab‘ul-Mathaaniy, Ummul-Kitaab. Haijateremka katika Tawraat wala katika Injiyl wala katika Zaburi mfano wake.
Utukufu na Fadhila za Suwratul-Faatihah unaelezewa katika Hadiyth nyingi, baadhi yake ni hizi zifuatazo:

Hadiyth Ya Kwanza:
Abuu Sa’iyd bin Al-Mu’allaa (رضي الله عنه) amehadithia kwamba:  Nilikuwa nikiswali, akaniita Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikawa sikumuitikia mpaka nilipomaliza kuswali. Kisha nikamwendea akaniambia: “Kimekuzuia nini usinijie?”  Nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah, nilikuwa naswali. Akasema: “Kwani Allaah Hakusema: “Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni kwenye yale yenye kukuhuisheni.” [Al-Anfaal (8: 24)]. Kisha akasema: “Nitakufundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan kabla hukutoka Msikitini.” Akanikamata mkono, alipotaka kutoka Msikitini, nikamwambia: ee Rasuli wa Allaah, ulisema utanifundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan. Akasema: “Naam, AlhamduliLLaahi Rabbil-‘Alaamiyn, hiyo ni (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu niliyopewa.” [Al-Hijr (15: 87) Al-Bukhaariy]

Hadiyth Ya Pili:
Abuu Sa’iyd Al-Khudhriyy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Baadhi ya Swahaaba (wakiwa safarini) walifika karibu na kabila fulani la Waarabu, wakakataa kuwapokea. Walipobakia katika hali hiyo, huku mkuu wao alitafunwa na nyoka (au nge). Wakasema: Je, mna dawa yoyote au tabibu? Wakajibu: Nyinyi mmekataa kutupokea kwa hiyo hatutamtibu mgonjwa wenu hadi mtulipe! Wakakubali kuwapa kundi la kondoo. Mmoja wa Swahaaba akaanza kumsomea Suwratul-Faatihah huku akikusanya mate na kumtemea (mahali alipotafunwa). Mgonjwa akapona kisha watu wake wakawaletea kondoo lakini wakasema. Tusiwachukue mpaka tumuulize Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Walipomuuliza alicheka akasema: “Mmejuaje kuwa Suwratul-Faatihah ni ruqya? Chukueni na nigaieni sehemu yangu.” [Al-Bukhaariy]

Hadiyth Ya Tatu:
Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Jibriyl (عليه السلام) alipokuwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisikia sauti kutoka juu. Jibriyl (عليه السلام) akatazama juu akasema: “Huu mlango wa mbinguni umefunguliwa na haujapatapo kufunguliwa isipokuwa leo.” Malaika akateremka humo akasema: “Huyu Malaika ameteremka ardhini, hajapatapo kuteremka kamwe isipokuwa leo.” Akasalimia kisha   akasema: “Pokea bishara ya nuru mbili ulizopewa ambazo hakuna Nabiy aliyepewa kabla yako; Ufunguo wa Kitabu (Al-Faatihah), na Aayah (mbili) za mwisho wa Suwratul-Baqarah.  Hutosoma herufi humo ila utapewa barakah zake ziliomo.” [Muslim]

Hadiyth Ya Nne:
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayeswali Swalaah bila ya kusoma humo mama wa Qur-aan (Suwratu Al-Faatihah) huwa haikutimia (ina kasoro).” Alikariri mara tatu: “Haikutimia.” Mtu mmoja alimwambia Abuu Hurayrah: (Hata) tukiwa nyuma ya Imaam? Akasema: Isome mwenyewe (kimya kimya) kwani nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Allaah (تعالى) Amesema: Nimeigawa Swalaah baina Yangu na mja Wangu nusu mbili, mja Wangu atapata yale aliyoyaomba. Mja anaposema: Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu, Allaah (تعالى) Husema: Mja Wangu kanihimidi.  Na anaposema: Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu, Allaah (تعالى) Husema: Mja wangu kanisifu na kunitukuza kwa wingi, na anaposema: Mfalme wa siku ya malipo, Allaah (تعالى) Husema: Mja wangu kaniadhimisha. Na mara moja alisema: Mja wangu ameniaminisha. Na anaposema: Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada, Husema: Hii ni baina Yangu na mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba. Na anaposema: Tuongoze njia iliyonyooka, njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea, Husema: Hii ni ya mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba.” [Muslim, Maalik, At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]  

Hadiyth Ya Tano:
‘Ubaadah bin Swaamitw (رضي الله عنه) amehadithia kwamba  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna Swalaah kwa asiyesoma (ndani yake) Ufunguo wa Kitabu.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

  

[2] Faida: Kuhusu njia iliyonyooka:
 Hadiyth Ya Kwanza:
 An-Nawaas bin Sam’aan  (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah(تعالى) Amepiga mfano; Swiraatw (njia) iliyonyooka, imezungukwa pande zote na kuta mbili na kila ukuta una milango iliyo wazi na imefunikwa na mapazia. Na katika lango la swiraatw kuna mlinganiaji akiita: “Enyi watu! Ingieni nyote katika swiraatw na msipite pembeni.” Na juu ya swiraatw, mlinganiaji mwengine anamuonya mtu yeyote anayetaka kufungua hiyo milango akiwaambia: Masikitiko kwenu! Msiufungue! Kwani  mkifungua mtapita ndani! Kwani Asw-Swiraatw ni Uislaam, na kuta mbili ni mipaka Aliyoiweka Allaah. Na milango iliyofunguliwa ni yaliyoharamishwa na Allaah. Na huyo Daa’iy (mlinganiaji) juu ya lango la Swiraatw ni Kitaabu cha Allaah, na Daa’iy juu ya swiraatw ni maonyo ya Allaah yaliyo ndani ya kila nafsi ya Muislaam.”  [Ahmad, ameisahihisha Al-Albaaniy;Swahiyh Al-Jaami’ (3887)]

Hadiyth Ya Pili:
Jaabir (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Tulikuwa tumekaa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), akachora mstari mbele yake, akachora mistari miwili kuliani, na mistari miwili kushotoni kisha akaweka mkono wake katika njia ya katikati akasema: “Hii njia ya Allaah” Kisha akasoma: “Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni, na wala msifuate njia (nyinginezo) zitakufarikisheni na njia Yake.” [Ahmad, Swahiyh Ibn Maajah (11)] 
[3]  Faida:  ‘Adiy bin Haatim (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Walioghadhibikiwa ni Mayahudi, na waliopotea ni Manaswaara.” [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Ghariyb na taz. Silsilah Asw-Swahiyhah (363)]

0 Comments